Muhogo Mchungu: Wasanii waache maisha feki mtandaoni

Muktasari:

Wanajipotosha wenyewe kwa kudanganya maisha waliyonayo, jambo ambalo siyo sawa kwa sababu wanapaswa kubuni vitu vingi vya maendeleo kuliko kujionesha katika mitandao.

Dar es Salaam. Msanii mkongwe Muhogo Mchungu amesema ni wakati wa mastaa na watu wenye majina makubwa kuacha kuonyesha maisha feki katika mitandao ya kijamii.

Muhogo Mchungu alisema wengi wanajipotosha wenyewe kwa kudanganya maisha waliyonayo, jambo ambalo siyo sawa kwa sababu wanapaswa kubuni vitu vingi vya maendeleo kuliko kujionesha katika mitandao kuwa maisha yao ni bomba kumbe hakuna chochote.

“Hakuna kitu ninakichukia kama maisha ya kuigiza kwenye mitandao ya kijamii, ninayachukia kwa sababu ipo siku mtu atakuja kuona maisha yangu halisi ashangae hivyo inapaswa kila mmoja kuishi vile Mungu amempangia na siyo kuigiza, hayo maisha feki tuyatupe kule,” alisema Muhogo Mchungu.

Muhogo Mchungu ametamba na kundi la Kaole Sanaa Group, michezo yao ya runinga kupitia kituo cha ITV akiwa na wasanii kama Nyamayao, Kibakuli, Kisa, Zawadi, Bi Staa, Kipemba, Swebe, na Hindu.