Wametoboa SZIFF Wema,Monalisa,Johari wakosa tuzo

Muktasari:

  • Hata hivyo, matokeo yalionekana kuwastaabisha baadhi ya mashabiki kutokana na kile kilichodaiwa baadhi ya wasanii wasiotarajiwa kutangazwa washindi.

HAYAWIHAYAWI hatimaye yamekuwa baada ya washindi waliochaguliwa kuwania Tuzo za Sinema Zetu International Festival Film (SZIFF 2019) kupatikana usiku wa kuamkia jana.

Mchakato wa tuzo hizo ulianza tangu Septemba mwaka jana kwa waandaaji kuzunguka nchi nzima kukusanya kazi za wasanii mbalimbali huku wa mikoani wakionekana kung’aa zaidi.

Kilele cha tuzo hizo kilifanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na mwenzake wa Zanzibar, Balozi Ali Karume.

Wengine ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri, Dk Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Katibu wa Bodi ya filamu, Joyce Fisoo.

Hata hivyo, matokeo yalionekana kuwastaabisha baadhi ya mashabiki kutokana na kile kilichodaiwa baadhi ya wasanii wasiotarajiwa kutangazwa washindi.

Mmoja wa mashabiki aliyejitambulisha kwa jina la Maimuna, alisema hakuamini matokeo hayo kwani matarajio yake msanii wa kike angeibuka ama Johari, Wema au Monalisa.

Wasanii walioibuka ni; Flora Kihombo (11) na Rashid Msigala (10), wanaolelewa katika Kituo cha Watoto wanaotoka katika mazingira magumu cha TAG Lwanga Student kilichopo mkoani Iringa. Filamu iliyowabeba inafahamika kwa jina la “Kesho”.

Wakati vipengele vilivyokuwa vikiwaniwa ni 30, macho na masikio zaidi yalikuwa katika kipengele cha msanii wa bora kike na wa kiume ambapo ushindi ulitwaliwa na Flora na Rashid.

Flora alikuwa akishindanishwa na wasanii wengine tisa kati yao ni wenye majina makubwa katika tasnia ya filamu akiwemo Blandina Chagula ’Johari’, Ivyonne Cherry ’Monalisa’ na Wema Sepetu.

Wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni; Jennifer Temu, Zaudia Rajabu, Sifa Matanga, Asha Mussa, Rhoida Richard, na Sasha Sebastian.

Msanii bora wa kiume, Rashid alikuwa akipambana na Hemed Suleiman, Salum Ahmed ‘Gabo’ ambaye mwaka jana ndiye alitwaa tuzo hiyo.

Wengine waliokuwepo katika kipengele hiki ni Maulid Ali (Mau), Peter Paul, Mack Daim, Sango Johanes, Salum Mpoyoka na Hassan Kazoa na Madebe Lidai ambaye alitangazwa kuwa mtangazaji bora katika tuzo hizo.

Johari, Wema Gabo,Monalisa wazungumza

Baadhi ya wateule ambao hawakubahatika kushinda akiwemo Johari katika maoni yake anasema kilichofanywa kwa wasanii wakongwe kuwekwa kundi moja na wasanii chipukizi si sahihi na kama waliamua kuwapa basi wangesema wasanii wakubwa wapo lakini wamefanya hivyo kwa ajili ya kuwatia.

Johari anasema kilichofanyika kinaweza kuua tasnia, kwani hata wawekezaji wataona kama nchi haina wasanii.

Naye Wema Sepetu anakiri kwamba kukosa tuzo kumemuumiza lakini anachoshukuru ni kwamba watu wanajua kwamba wanajua, lakini anaona ni wakati wa watoto nao kupewa nafasi.

Kwa upande wake, Gabo hakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema anashukuru kwa madai kuwa kuwa kusema hivyo ni kuonyesha uungwana uliotukuka mbele za watu.

Naye Monalisa ameandika: “Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wote mliochukua muda wenu na kupigia kura, ahsanteni sana kwa bahati mbaya kura zetu hazikutosha.

“Hongera sana mtoto mzuri Kamwene (utanisemehe sijalishika jina lako) kwa kushinda Tuzo ya Mwigizaji Bora.”

Wasanii povu

Hata hivyo, ushindi huo umeonekana pia kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii na kati ya watu waliokuwa wa kwanza kutoa maoni yao ni msanii Jacqueline Wolper, ambaye anasema ana filamu tisa zipo ndani na kutokana na hela aliyoitumia kutengeneza zitaendelea mpaka watakapokuja watu wenye uchungu wa sanaa hiyo.

Wolper alienda mbali zaidi na kueleza kuwa kama itashindikana kuziuza watakuja kuangalia wajukuu zake na kueleza kwamba katika tasnia hiyo kama huwaendekezi waandaaji wa tuzo pale wanapokuita ndio umekwenda na maji

Steve Nyerere, anasema kuwa juzi kila unayempigia simu alikuwa yupo saluni akijiandaa kupokea tuzo huku akihoji ni kweli Johari, Monalisa, Gabo ni watu wa kukosa kura?

Hata hivyo, baadaye Steve aliweka picha za wasanii hao watano maarufu akiwemo Gabo, Hemed, Wema Monalisa pamoja na Johari, na kuandika kuwa mwakani mkiitwa tena nendeni.

Naye Rose Ndauka, alitupia picha ya mtoto wake na kuandika ‘Haya jamaniii mwakani msanii bora wa kike ni Naveen Ndauka, najua mtabisha ila hadi mimi ananikimbiza.”

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji, Elia Mjata, alisema ushindi wa watoto hao umefungua fursa kuzalisha vipaji vipya vyenye umri mdogo.

Mjata alisema anaamini hata waliocheza filamu za watoto hao hawakufikiria kama siku mmoja wangepata tuzo hiyo kubwa.

Msanii Rammy Galis, alisema ilikuwa lazima mshindi apatikane, na kama majaji wameona watoto ndio wlaikuwa wanafaa basi hakuna kipangamizi, na kuwatakla wasanii walioshindwa wajipange kwa ajili ya mwakani kurudisha heshima yao.

Jaji kiongozi afunguka

Rais wa jopo la majaji wa SZIFF, Martin Mhando, anasema: “Matokeo hayawezi kumridhisha kila mmoja kwnai hata mwaka jana, pamoja na wasanii wakubwa kushinda bado kulikuwa na malalamiko.”

Badala yake Martin anawashauri Watanzania kuangalia filamu ambayo imetoa washindi na kuangalia uwezo ulioonyeshwa na washindi ambao baadhi wanasema hawakustahili.

Majuto akumbukwa

Pamoja na kwamba mwaka jana msanii maarufu wa vichekesho, kushiriki tuzo hizo ambazo zilikuwa zikifanyika kwa mara ya kwanza hawakumtambua kwa kumpatia tuzo.

Kutokana na hilo, msanii huyo alitoa onyo kutoshirikishwa kwenye tuzo zozote kwa kile alichodai hakuna anayeiona thamani yake leo.

Hata hivyo malalamiko hayo yameonekana kufanyiwa kazi na waandaji wa SZIFF kwa mwaka huu kumpa tuzo ya heshima ambayo hata hivyo ilipokewa na mwakilishi kwani famila yake haikuwepo.