Ukitaka kuondoa stresi kutana na huyu Senga

Muktasari:

Senga ambaye amefanya vichekesho na wasanii mbalimbali kama Asha Boko, Matumaini, Pembe, Mtanga na wengineo amesema hakuna ambaye alimpa shida na anaweza akafiti kuchekesha na mtu yoyote.

ULIMBOKA Anangisye ndiyo jina halisi la supastaa wa komedi anayevuma kwa jina la Senga. Huyu jamaa buana, amejaaliwa kapawa cha aina yake, hautaacha kucheka ukibahatika kupiga naye stori mbili tatu. Anajiita daktari wa kutibu stresi.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano, lilifahamu mambo mengi ya Senga kubwa zaidi amefichua yupo jiji la Dar es Salaam la kibiashara kwa malengo maalumu.

Katika maisha yake anaamini katika kutumia fursa. Ana vipawa vingi nje ya komedi. Ni mchoraji wa ramani, anaimba nyimbo za Injili pia ni mtalamu wa kupiga ala za muziki.

Licha ya kuwa mkongwe kwenye tasnia ya uigizaji na uchekeshaji, Senga anasema hataki kupitwa na wakati na ndilo jambo linalomfanya wasanii chipukizi kuendelea kujifunza kwake kufanya kazi katika dunia mpya ya mitandao ya kijamii.

Jamaa ni mcheshi kuna wakati eti anajishangaa anapokaa kuangalia komedi zake na anajihoji aliwaza nini kufanya hivyo vituko.

Senga ambaye amefanya vichekesho na wasanii mbalimbali kama Asha Boko, Matumaini, Pembe, Mtanga na wengineo amesema hakuna ambaye alimpa shida na anaweza akafiti kuchekesha na mtu yoyote.

Katika stori za hapa na pale na Mwanaspoti Senga alikuwa na haya ya kuwajuza wadau wa kazi zake na kwamba waendelee kumsapoti hawezi kuchuja leo wala kesho.

MWANASPOTI: Kabla ya kutoa komedi yako nini unazingatia?

SENGA: Hii ni kazi inayotazamwa na watu wenye akili zao, duniani kuna madaktari wa kila aina ambao wanatibu magonjwa mbalimbali, lakini la mawazo ‘stress’ linaonekana bado halijapatiwa uvumbuzi, ndio maana tuliopewa kipaji lazima tuitumie ipasavyo.

“Naamini mdau anayetazama kazi zangu za komedi hata kama alikuwa ana hasira ama stress atacheka na kusahau kwa muda. Hilo linasaidia kuleta afya ya akili kuwa ya utulivu kwa mtu, ndio maana nakuwa najitahidi kufanya ubunifu mkubwa,” anasema.

MWANASPOTI: Umekaa kwa muda mrefu kwenye sekta ya vichekesho nini siri?

SENGA: Asilimia kubwa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam sio Wazaramo. Wengi wametoka mikoa tofauti kwa ajili ya kusaka maisha, nimetokea kijiji cha Mwakaleli mkoa wa Mbeya lengo ni kutengeneza mkwanja.

“Hii ni kazi iliyonipa heshima mbele ya Watanzania, ndio maana najitahidi kuwa mbunifu ili kuendana na wakati huu, najifananisha na daktari wa kupasua kichwa hivyo najifanyia upasuaji mwenyewe kabla ya kumfanyia mwingine ama najikamua jipu mwenyewe ndipo naenda kwa wingine,”

“Kwanza dunia inaendelea nafahamu watu wanahitaji nini, nahakikisha kwamba hii italeta heshima ndio maana licha ya kwamba nilianza zamani kufanya vichekesho lakini bado naendelea kutesa sokoni,” anasema.

MWANASPOTI :Je wasanii chipukizi wanashindwa wapi?

SENGA:Jambo kubwa ninaloliona wakishapata majina kwenye jamii wanajiona wana akili kuliko wale ambao wanashabikia kazi zao, hilo kwao ni tatizo linalowafanya wakaonekana ni wa kawaida sana.

“Yaani wakitoa vichekesho vichache wakavuna wanajiona wamemaliza kila kitu, tatizo hilo tunaliita mabega yanazidi kichwa, sio wao tu hata wanamuziki unakuta anawika halafu baada ya wiki wanamsahau, shida ni kulewa sifa,” anasema.

MWANASPOTI: Je unaweza kuigiza nafasi za siriasi zisizo na komedi?

SENGA: Katika filamu mimi ni kama unga wa ngano ambao unaweza ukatumika kwa kutengenezea vitu vingi, kitu ambacho siwezi kukicheza ni kuigiza kama mama, hilo hapana.

“Naweza nikacheza kama mkurugenzi endapo kama nitaandaliwa mapema ila bado watu watacheka wataanza kusema we Senga hivi wewe kweli ndio wa kucheza kama bosi, ila baadaye wataukubali muziki wangu ingawa bado kuna sehemu watacheka, maana ni karama kuchekesha watu,” anasema.

MWANASPOTI: Kuna komedi ulifanya unapiga chabo chooni, uliwaza nini?

SENGA: Yaani hata mimi mwenyewe nashangaa hasa baada ya kubambwa na yule mwanamke nikamwambia nataka vocha, hiyo inamanisha kufanya vitu vya kufikirika.

“Napenda kuchekesha sana, mfano wanandoa wamenuniana wamekaa sebuleni, mmoja wapo akiangalia komedi zangu ama wakaangalia kwa pamoja itatatua magomvi yao,” anasema.

MWANASPOTI: Vichekesho gani ulivyofanya vinakuchekesha zaidi?

SENGA: Ni vingi kuna wakati mwingine hata mimi mwenyewe ninakuwa ninashangaa kwamba nimewaza nini, hii ni kazi iliopo moyoni na ni kipaji nilichopewa na Mungu.

MWANASPOTI: Unaizungumziaje tamthilia ya Kapuni?

SENGA: Zamani tulikuwa nyuma kwa sayansi na teknolojia, lakini pia kuna wizi ambao ulikuwa unafanyika pamoja na kufanya kazi chini ya kiwango, kwa sasa yapo mambo mengi ambayo yameboreshwa ndio maana jamii imetupokea kwa kishindo.

Kwanza tamthilia hiyo imechezwa na asilimia kubwa wengi wapya na wamechukuliwa wa zamani ambao wanajua thamani ya kazi yao ndio maana unaona kuna mapokeo mazuri.

Katika tamthilia hiyo nimecheza kama mume wa Tausi na Matumaini ni mdogo wangu ambaye hawaelewani na mke wangu, kiukweli nimefurahi kucheza na hao wasanii kwani wanajua kuigiza uhalisia wao.

MWANASPOTI: Nje na kuigiza una fani gani?

SENGA: Naimba pia napiga vyombo vya muziki na nachora ramani, najishugulisha vya kutosha kwani sijaja kushangaa watu Dar es Salaam, ukinikuta eneo hilo utanisahau, kifupi najua kujituma ili kuwa mfano.