Stori ya kitabu cha Hawa haipaswi kuishia hapa

Sunday September 23 2018

 

By LUQMAN MALOTU

FILAMU huandikwa, huandaliwa, huongozwa, huchezwa na huhaririwa na wengine. Hata hivyo, mtazamaji huumba mwisho anaoupenda. Kuna mahali ikiishia, mtazamaji anaweza kufurahi au kukasirika. Furaha huja kwa kuupenda mwisho wake, kukasirika ni kutopenda mahali ilipoishia.

Unakuta mtazamaji anasonya na kulaumu. Misonyo na lawama ni tafsiri yake kuwa stori ya filamu husika haikupaswa kuishia ilipoishia. Hii inahusu tamthiliya au hata kitabu. Msomaji wa kitabu cha stori, akishiba vilivyo simulizi, mwisho wa stori usipomkuna atalaumu.

Stori ya Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, ingeishia kwa kufia kitandani kipindi alipoumwa uti wa mgongo miezi nane, isingependeza kabisa. Angekumbukwa kwa kuwa wakili wa Mahakama Kuu aliyefuzu bila kufika chuo, isipokuwa kwa kujielimisha kupitia kusoma vitabu.

Ilibidi Lincoln awe Rais wa Marekani baada ya kunyanyuka kitandani kisha kushindwa majaribio mengi ya kuwania uongozi. Ndipo akawa Rais aliyeweka misingi ya utu ambayo inamfanya leo atamkwe kuwa Rais namba moja kwa ubora Marekani. Hapo stori ya Lincoln imemalizika vizuri.

Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, maisha yake yangeishia gerezani Robben Island alipokuwa amefungwa kifungo cha maisha na Serikali ya ubaguzi wa rangi, kitabu chake kingejaa masikitiko tu. Kila msomaji au kwa filamu, kila mtazamaji angesonya na kulaumu, maana stori haikupaswa kuisha hivyo.

Ilibidi Mandela awe Rais, aoneshe namna uongozi wenye kulingania makundi yote unavyopaswa kuwa. Adhihirishe kwamba kupigania haki kunaweza kukufanya upewe majina mabaya. Ukifanikiwa kupewa rungu la kusimika haki, unatenda kazi bora. Mwisho waliokwita magaidi, wanaamua kukutukuza kwamba wewe ni shujaa wa dunia. Stori ya Mandela imeisha vizuri sana.

Hii inapaswa kuwa funzo kwa kila mmoja, kwamba ajitahidi kitabu chake kisomeke vizuri. Ongeza kurasa nzuri za kuipamba stori ya maisha yako. Pambana kadiri uwezavyo juu kabisa ya uwezo wa binadamu. Mengine unamwachia Mungu aamue.

Risasi tisa zingemchukua 50 Cent mwaka 2000, angeishia kutambulika kama haramia wa dawa za kulevya na underground wa Hip Hop. Alipopona majeraha ya risasi na kutokea kuwa supastaa wa Hip Hop, filamu na mwandishi wa vitabu, ni dhahiri stori yake inajitengeneza vizuri.

Hata nilipomwona Hawa. Msichana mrembo aliyefanya vizuri kwenye wimbo Nitarejea wa Diamond Platnumz, akiwa amevimba tumbo, ikielezwa ana matatizo ya ini. Akitakiwa kubadilishwa ini. Fedha za kumudu matibabu hana. Bado nikasema stori ya Hawa haipaswi kuisha hapo. Ipo kazi inatakiwa kufanyika.

NAMFAHAMU HAWA

Namfahamu Hawa kama msichana mwenye kipaji kikubwa cha muziki. Ana sauti ya kipekee na anajua kuimba. Nilimfahamu takriban miaka 10 iliyopita akiwa anafanya kazi kwenye maduka ya Zizzou Fashion. Kipindi hicho alikuwa rafiki hasa wa mwanamuziki mwingine fundi, Maunda Zorro. Hawa na Maunda walikuwa wakiishi pamoja Kijitonyama wakati huo. Nakumbuka nyakati za jioni walikuja ofisi niliyokuwa nafanyia kazi na tulizungumza mambo mbalimbali, kuhusu muziki wao, malengo yao na mengineyo kuhusu kiwanda cha muziki na burudani kwa jumla.

Kipindi hicho Hawa alikuwa mwenye afya njema sana. Urembo wake wa asili haukuwa ukijificha. Ndiyo maana nilipomwona Hawa mwenye afya dhaifu, tumbo limevimba, mama yake akilia kuomba msaada ili kumwokoa binti yake, nikasema hapana, stori ya Hawa haipaswi kuisha hivi. Kitabu cha Hawa kinahitaji kurasa nyingi nzuri ili kuipamba stori yake.

Nilikuwa Mhariri kwenye chombo kimoja cha habari. Na nilikuwa msimamizi wa masuala yote ya burudani. Aliyekuwa bosi wangu (mmiliki wa kampuni hiyo) alivutiwa kuwasaidia Maunda na Hawa. Bosi wangu ndiye alimtambulisha Hawa kwangu. Baada ya hapo Maunda na Hawa wakatokea kuwa marafiki kwangu. Tulipigiana simu, tulikutana, tulipiga stori, tulitaniana na kucheka pamoja.Kipindi hicho pia Hawa na Maunda walikuwa THT. Hawa alirekodi wimbo unaitwa Mwanamke Hapigwi. Alimpa yule bosi wangu ambaye alinipa niusikilize ili kama unafaa aweze kumsaidia promosheni. Niliusikiliza mara nyingi. Ulikuwa wimbo mzuri sana. Nikamjibu bosi wangu kuwa wimbo ni mzuri. Kazi ikabaki kwake.

Sikujua kilichofuata. Na sikumuuliza bosi wangu nini kiliendelea kuhusu wimbo wa Hawa. Nilishangaa baadaye nasikia wimbo wa Linah, Bora Nikimbie. Maudhui ya Bora Nikimbie na Mwanamke Hapigwi ni aina moja. Ujumbe ni malalamiko ya mwanamke kuchoshwa na vipigo kutoka kwa mpenzi wake.

Mwanzoni niliposikiliza maneno ya wimbo na kwa sababu nilianza kuusikiliza katikati nilijua ndiye Hawa mwenyewe. Niliposikiliza vizuri nikagundua siye yeye. Nilijua tu mawazo ya waandishi wa nyimbo yaligongana. Hata hivyo, sikuacha kushangaa maana Linah na Hawa wote walikuwa THT, iweje mawazo yafanane vile?

Baada ya hapo Mwanamke Hapigwi wa Hawa haukusikika popote. Bora Nikimbie wa Linah ukawa bonge la wimbo. Mpaka leo hisia za kibadamu huniambia kuna kitu kilifanywa mpaka Mwanamke Hapigwi ukapotea. Nakumbuka pia wakati huo Hawa na Maunda waliondoka THT (sijui sababu). Hawa aliacha kazi Zizzou Fashion. Nikawa siwaoni mara kwa mara kama zamani.

SAFARI MBAYA YA HAWA

Mawasiliano na Hawa yalikata. Maunda niliwasiliana naye kwa simu. Kipindi hicho Maunda na Hawa hawakuwa karibu tena. Sikumbuki kipi kilianza, kati ya kumwona Hawa mwenye mtoto au Hawa kuimba Nitarejea na Diamond Platnumz. Ninakumbuka alikuja ofisini akiwa na mtoto, akimtafuta yule bosi wangu.

“Luqman baba yupo?” Hawa aliniuliza. Ndivyo Hawa na Maunda walizoea kumwita yule bosi wangu. Alikuwa anahitaji msaada, mtoto wake alikuwa anaumwa. Nilimwona mara mbili au tatu ofisini, baada ya hapo sikumwona tena. Wimbo Nitarejea ukiwa mkubwa, Hawa ndiyo akawa anafifia. Hawa alipishana na nyota ya wimbo.

Mwaka 2012, nilipokea simu kutoka kwa mapromota ambao huandaa shoo za Waafrika nchini Uingereza, waliomba niwaunganishe na Hawa pamoja na Diamond. Nitarejea ulikuwa umetoboa vizuri kwenye himaya ya Malkia. Hata hivyo, sharti nililopewa ni kwamba lazima wote wawili waende Uingereza. Si Diamond peke yake wala Hawa.

Kipindi hicho kwa sababu za kikazi Diamond nilikuwa nawasiliana naye kwa ukaribu, ila kumpata Hawa ilikuwa shughuli, hakuwa na simu tena. Nilimpigia Maunda tusaidiane kumpata Hawa. Niliamini tungefanikisha kumpeleka Uingereza, pengine malipo yangemsisimua, hivyo kumpa mwanga wa kuheshimu kipaji chake na kazi yenyewe ya muziki. Hatukufanikiwa kwa Hawa. Iliniuma sana kupata taarifa za mabadiliko yake ya kitabia kwamba, aligeuka mlevi wa pombe kali. Vile wimbo wa Nitarejea ulivyopata umaarufu mkubwa, basi haikuwa siri. Yote aliyofanya yalivuma. Hawa akawa mwenye kutamkwa kwamba, hakuwa binadamu wa kawaida tena. Alijikatia tamaa ya maisha. Nilikuwa na matumaini kwamba kuanzia pale angeendelea kupata matibabu na baada ya kupona angerejea kwenye ubora wa kipaji chake. Kinyume chake nikashangaa kumwona Hawa mgonjwa zaidi. Kwamba sasa hivi anaishi kwa msaada wa kufyonzwa maji. Tiba kamili ni kwenda nje akabadilishwe ini.

Advertisement