Serikali yampa pole prodyuza S2kizzy

Thursday October 15 2020

 

By KELVIN KAGAMBO

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas ametembelea studio za muziki za Pluto zinazomilikiwa na prodyuza S2kizzy ambazo usiku wa kuamkia Oktoba 16 zilivamiwa na kikundi cha watu walijitambulisha kama sungusungu na kufanya madhara ikiwemo kuwapiga wasanii waliokuwepo studio hapo na kuvunja vifaa.

 

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio Sinza Dar es Salaam, Dk. Abbas amesema amefika eneo hilo kuwatazama na kuwapa pole waathirika wa tukio hilo ambao ni wasanii mbalimbali wengi wakiwa chipukizi, akiwemo Hanstone aliyeimba wimbo wa Iokote na Maua Sama.

 

“Serikali inatambua na kuziheshimu shuhuli za sanaa, Kwahiyo tumesikia hili tukio, na nafahamu kuna kesi polisi kwa maana ya hao Sungusungu waliokuja hapa wanadai kuwa walikuja kuzuia tukio fulani na nyinyi hawa (wasanii) wanasema walivamiwa, kwahiyo hii ni kesi ya kipolisi zaidi.” amesema Dkt. Abbas.

 

Advertisement

Ameongeza kwa kuwapa pole waathirika wa tukio hilo huku akiwaahidi kuwa serikali itahakikisha inafuatilia kwa ukaribu tukio hilo na kuhakikisha haki inatendeka.

 

Tukio lilivyotokea

Akizungumza na mwandishi wa Mwanaspoti, prodyuza S2kizzy ambaye ametengeneza nyimbo kama Baba Lao, Tetema na Deka ya Billnas amesimulia kuwa tukio hilo lilitokea saa 9 usiku ambapo wasanii walikutana kwake kwa ajili ya kwenda kwenye ‘shooting’ ya video wa wimbo.

 

“Kuna video tulikuwa tunaenda kushuti, na Director alisema inatakiwa tushuti alfrajiri, kwahiyo tukakubaliana watu wote tukutane hapa kwangu (studio) usiku ili tuondoke kwa pamoja.

 

“Sasa ilipofika baadae mimi niliwaacha wenzangu nikaenda kufata gari kwa sababu gari yangu nilimuachia Felix (rafiki yake). Kwahiyo nilivyorudi hapa ndiyo nikakuta tukio limeshafanyika.” ameeleza.

 

Hata hivyo S2kizzy amefunguka kuwa tukio hilo tayari liko mikononi mwa jeshi la polisi hivyo hatakiwi kulizungumzia zaidi.

 

Inaripotiwa kuwa; kundi la watu waliovamia studio hiyo walijitambulisha kama sungusungu na baadhi yao walikuwa wamevalia sare za kampuni ya ulinzi. Watu hao walifika wakiwa na silaha za jadi kama vile rungu na wakaanza kufanya uharibu ikiwemo kuvunja kompyuta na spika za studio lakini pia kuwafanyia matendo ya udhalilishaji waathirikia kama vile kuwalazimisha wavue nguo pamoja na kuwapiga.

 

 

Taarifa zaidi zinakujia, usikae mbali na Mwanaspoti Website na mitandao yetu ya kijamii pamoja na kusoma gazeti la Mwanaspoti.

Advertisement