Said Mabera wa Msondo Ngoma afariki dunia

Muktasari:

Mabera ameweza kudumu kwenye Bendi ya Msondo kwa zaidi ya miaka 40 bila kuhama, tangu alipojiunga na bendi hiyo mwaka 1973

Mpiga gitaa la solo wa Bendi ya Msondo Ngoma ‘Mambo hadharani’, Said Mabera maarufu ‘Dokta’ amefariki dunia.

Habari za kufariki kwake zimethibitishwa na Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti leo Septemba 29,2020 alipozungumza na Mwanaspoti Digital.

Kibiriti amesema taarifa za kifo cha msanii huyo wamezipata asubuhi ya leo na msiba upo nyumbani kwake Goba Mpakani jijini Dar es Salaam.

Meneja huyo amesema japokuwa bado hawajajua chanzo cha kifo chake mpaka watakapokutana na familia baadaye, lakini msanii huyo kwa miezi mitatu alikuwa mgonjwa.

“Mzee Mabera ni kweli ametutoka ila bado hatujajua nini hasa chanzo cha kifo chake mpaka tutakapokutana na familia, lakini  ninachojua afya yake haikuwa nzuri, takribani miezi mitatu alikuwa mgonjwa hadi kushindwa kuhudhuria kwenye shoo tulizokuwa tukifanya maeneo mbalimbali," amesema Kibiriti.

“Magonjwa yaliyokuwa yanamsumbua zaidi katika miezi hiyo mitatu ni kisukari na shinikizo la damu, lakini nadhani familia ndio itakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo zaidi.”

Akielezea namna watakavyomkumbuka mzee Mabera, meneja huyo amesema alikuwa kiungo katika bendi yao kwani nyimbo nyingi ameshiriki katika kuzitengeneza.

Kama haitoshi amesema ndiye msanii aliyedumu muda mrefu katika bendi hiyo bila kuhama tangu mwaka 1973.