Roma aliitaka Zimbabwe akapewa viza ya Marekani

Sunday July 5 2020

 

By LUQMAN MALOTO

AGOSTI 2017, tulikuwa na safari ya mguu kwa mguu na Rapa Ibrahim Mussa Mshana ‘Roma Mkatoliki’, kwenda Zimbabwe. Roma alitoa wimbo unaoitwa Zimbabwe, akionesha kuwa alikuwa na mengi angependa aseme.

Hata hivyo, Roma anajibu kwa verse hoja zote zenye kumtaka aseme kile ambacho kilimtokea alipotekwa na watu wasiojulikana Aprili 2017. Roma anasema kuwa yeye si rapa tu, bali ni baba wa familia. Je, akisema halafu akiuawa nani atakayebeba majukumu yake ya kifamilia? Mama na mtoto wake watalelewa na nani?

Wewe ambaye ulitaka Roma amtaje aliyemteka, anakuuliza kuwa mtekaji angeiteka ripoti ya upelelezi ingekuwaje? Ukifika hapo unapata majibu kuwa Roma aliumizwa sana lakini alishindwa kusema yote hadharani. Ingawa kwenye Zimbabwe Roma anasema yeye haogopi kufa.

Sababu ya kuhofia kusema si nyingine bali ni maisha yake binafsi. Anauliza faida ya kutamkwa tu alikufa mwanaharakati wakati nyuma yake atamwacha mama yake na mtoto wake wakiwa hawana matunzo.

Ni ujumbe unaochoma sana. Tafakari mwandishi na mwanaharakati wa Nigeria, Ken Saro-Wiwa, aliyeuawa kwa kunyongwa mwaka 1995 na Serikali ya Nigeria iliyokuwa chini ya utawala wa Dikteta Sani Abacha, kama si kampuni ya mafuta ya Shell iliyoilipa fidia familia yake kwa msaada wa Marekani, familia yake ingekuwa imeambulia patupu.

Shell walitoa fedha dola 15.5 milioni, sawa na Sh34.7 bilioni kwa familia ya Saro-Wiwa na ndugu wa watu wengine nane jamii ya Ogoni, Niger Delta, Nigeria, waliouawa wakati wa kupigania fidia ya madhara ya kiafya na kimaisha baada ya kuharibiwa mazingira kutokana na kazi ya uvunaji wa mafuta ya Shell.

Advertisement

Roma yeye akiuawa leo nani atailipa familia yake fidia? Ndiyo maana anahoji yule ambaye atamlea mwanaye au mama yake? Hapohapo anakumbusha kuwa alipokuwa anauguza majeraha baada ya kuachiwa na watekaji, watu hawakwenda japo kumjulia hali, je, walisubiri afe waende msibani? Ni maneno ya Roma ndani ya Zimbabwe.

Ipo hoja kwa Roma, harakati bila matumizi bora ya ubongo ni hasara ya mwanaharakati. Dunia imejaa ubinafsi, faida ya mwanaharakati ni vile ambavyo yupo hai na anadunda. Mwanaharakati akishalala watu huwa hawana habari naye kabisa.

Tajiri nambari moja Afrika kwa wakati wake, Chifu Moshood Abiola, aliamua kutojali utajiri wake na kujikita kwenye harakati za kuubadili utawala wa kijeshi Nigeria hadi utawala wa kidemokrasia, matokeo yake alifia jela mwaka 1998 na fedha zake zilichotwa benki na watawala wa kijeshi. Familia yake ikabaki maskini.

Kuna wakati harakati zinakata stimu mpaka basi ndio maana watu wengine huamua kuwa wabinafsi kwa kufanya harakati za matumbo yao na familia zao na kuachana na zile za ukombozi wa jamii. Tafakari, familia za wazee kina Oliver Tambo, Walter Sisulu na wengine zinaishije leo, wakati Rais aliyeondolewa madarakani Afrika Kusini, Jacob Zuma ana kesi ya kufanya ufisadi wa mali za Waafrika Kusini.

Familia ya Bibi Titi Mohamed inaishi vipi leo, wakati ambao kuna kina mama ambao hawajui japo tone la jasho la ukombozi wa nchi, waliposhika nafasi nyeti serikalini waliamua kuwasaliti wananchi na kufanya ufisadi? Wajukuu zake wanajisifu tu kuwa na bibi mwanaharakati na mkombozi wa nchi.

Vema ieleweke kuwa Roma anazo sababu za msingi za mambo mengine kunyamaza, maana viatu alivyovaa siri yake anaijua yeye zaidi kuliko mwingine yeyote. Hatari ya kusema na usalama wa kukaa kimya, mjuzi wa undani zaidi ni yeye.

Yule Roma jasiri, mnyoosha mistari bila hofu. Roma aliyesema hata Ikulu anaipiga chata akiwa amevaa mlegezo kwenye ngoma Mathematics, alisanda na kutangaza kukimbilia Zimbabwe. Roma mpya kabisa toleo la mwaka 2017, alisema bora tu aende zake Zimbabwe.

Ni sanaa tu ilitumika. Ielewe Zimbabwe ya wakati huo chini ya Rais Robert Mugabe. Halafu mtoe Roma, weka neno sisi. Hiyo sisi itumike kwa kutujumuisha sisi Watanzania. Je, Roma alimaanisha tulikuwa tunakwenda kufanana na Wazimbabwe ile ya Mugabe? Mpaka leo hajajibu.

Zimbabwe ni ngoma nzuri. Roma alithibitisha uwezo wake wa kuandika. Hajafyatuka kama alivyofanya kwenye 2030, Viva na nyingine sumu, lakini aliandika kwa tahadhari na ujumbe ulifika. Aliahidi kuwa hata makinikia angeyatengenezea mapini. Mpaka leo kimya.

Roma alifanya kazi bora katika Zimbabwe, ujumbe ulifika kila upande. Aliwaambia wateka watu waache huo uhuni wao wa kishamba. Acheni ushindani wa hoja uchukue nafasi. Sio ukikosolewa kidogo unatuma watu wamteke aliyekukosoa, huo ni uzezeta.

Hapa nasisitiza kuwa yeyote aliyehusika na kumteka Roma na wenzake, aliye nyuma ya kupotea kwa Ben Saanane, Azory Gwanda, Simon Kanguye na wengineo, hata awe mkubwa kama tembo, ajitambue kwamba yeye ni mshamba. Yaani bonge la mshamba!

Ujumbe kwa washabikia mambo na kutaka kilichomo kwenye akili zao ndio hichohicho kifanyiwe kazi na wengine bila kuvaa viatu vya wahusika kujua wanapitia magumu kiasi gani, waache ushabiki maandazi.

Mijeledi aliyopigwa, kisago alichopokea hukumsaidia, kwa hiyo hujui maumivu yake. Usikae tu pembeni na kupaza sauti. Ulimwengu mpya unakataza ushabiki. Siri ya mtungi aijuaye kata.

Hapa mimi sitii neno zaidi ya kukubaliana na Roma kuwa Mungu wa Paulo ndiye huyohuyo Mungu wa Daudi. Hakuna mabadiliko yoyote, kwani Mungu wa Daudi ndiye Mungu wa John ambaye Wayahudi humwita Yohana.

Mungu huyohuyo ndiye wa Roma na wengine wote duniani. Hivyo kila mmoja lazima atambue kuwa hakuna binadamu mwenye leseni ya kuwanyanyasa wenzake. Hayupo binadamu mwenye ubinadamu kipeuo cha pili, hakuna binadamu wa lumbesa na mwingine wa kawaida, wote ni sawa. Mungu ni mmoja, tusinyanyasane na vijibunduki vyenu.

Vuta pumzi; huu ni mwaka 2020, Roma yule aliyeaga anakwenda Zimbabwe, yupo amelowea Marekani tangu mwaka jana. Haonyeshi mpango wa kurejea. Familia yake ipo Tanzania, yeye kwa Trump. Pengine wimbo Zimbabwe ulimsaidia kupata Green Card visa ya Marekani.

 

Advertisement