Roma: Nyimbo zangu zinawalenga wasio na sauti ya kusema

Muktasari:

Msanii wa Tanzania, Ibrahim Musa maarufu Roma Mkatoliki amesema nyimbo  zake zinawagusa watu wasio na sauti ya kusema mambo yanayowakabili katika jamii.

Dar es Salaam. Msanii wa Tanzania, Ibrahim Musa maarufu Roma Mkatoliki amesema nyimbo  zake zinawagusa watu wasio na sauti ya kusema mambo yanayowakabili katika jamii.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 19, 2019 katika mahojiano na Mwananchi kuhusu wimbo wake wa ‘Anaitwa Roma’ aliomshirikisha  msanii One Six.

Wimbo huo umekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii huku watu wakihofia  unaweza kumtia matatani wakihusisha na tukio la kutekwa kwake la mwaka 2017.

Aprili 7, 2017 msanii huyo akiwa na wenzake watatu walichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa kwenye studio ya Tongwe Records iliyopo Masaki Dar es Salaam wakifanya kazi ya kurekodi nyimbo.

Msanii huyo na wenzake walikaa mikononi mwa watu hao kuanzia siku ya Jumatano na kuachiwa Ijumaa. Tukio hilo lilihusishwa na aina ya nyimbo anazoimba na ndiyo maana alipotoa wimbo huu umezua mjadala.

Roma ambaye yupo nchini Marekani amelieleza Mwananchi kuwa katika wimbo huo amegusa makundi mbalimbali katika jamii.

 “Nimezungumzia tukio langu la kutekwa ambalo linaweza kuwagusia wengine. Nimeeleza kuhusu  huduma za afya, nimehubiri kuhusu amani mtu asiyependa amani hawezi kuupenda huo wimbo ila anayependa amani ataupenda tu.”

“Roma ni mzalendo ndio maana  aligusia  mambo ya nchi yake kwamba  watawala na wapinzani wakae meza moja wamalize mambo yao kwa kukubaliana na mfano ni lile tukio la Akwilina,” amesema Roma.

Akwilina Akwiline, alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) alifariki dunia Februari 16, 2018 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao walioshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni uliofanyika Februari 17, 2018.

“Nimeongelea  walimu wakidai mafao yao sasa kuna mwalimu atakataa, ninapaza sauti  kwa wale ambao hawana sauti. Mapolisi nimewapigia kelele kuhusu kipato chao kuongezeka, tuna kaka na wajomba zetu ni mapolisi.”

“Nimezungumzia hospitali ziboreshwe na watu wanataka huduma za afya. Nimezungumzia wafanyabiashara na wakulima, viongozi wa kisiasa wanaokutana na masahibu mbalimbali, tukio langu la kutekwa pia nimelizungumzia ndio maana nimewagusa watu mbalimbali,” amesema Roma.

Amesema wasanii wengi wamewahi kutoa nyimbo zenye ujumbe kama wake miaka ya nyuma  na kubainisha kuwa huenda hawakuvuma kama walivyo wasanii wa sasa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo mitandao ya kijamii.

“Niliwahi kutoa wimbo mwaka 2011 na watu waliupokea kama sasa. Mimi nina mashabiki wangu ninaowalenga, ukipita sehemu utawaona madereva bodaboda na Bajaji wanafurahi wanasema wananikubali rais wa geto,” amesema Roma.

 

Amesema nyimbo anazotoa amekuwa akipigiwa simu na viongozi wa dini na wa Serikali wakimpongeza.

 

“Maaskofu, mapadri na masheikh pamoja na viongozi serikalini nilikaa nao meza moja na kunieleza kuwa wanapenda kazi ninayoifanya. Hiki kilikuwa kitu kikubwa maana kuna mashabiki wangu ninawakumbatia wasipotee, “ amesema.

 

Amesisitiza, “ukiwa msanii ukaimba wimbo wa mapenzi unalalamika umekimbiwa na mpenzi wako unataka arudi nyumbani, ukiutoa huo wimbo watu walio kwenye hali hiyo wataipokea na utawagusa, sasa unapaswa kujiuliza wapo wangapi? Mtu akisikiliza wimbo wangu lazima ataondoka na kitu kinachomgusa.”

 

Miongoni mwa mashairi ya wimbo huo pendwa mjini hivi sasa ni

 

‘Wanauliza Roma siku hizi huimbi za kiharakati huku wakisema Ununio ndio kumbukumbu iliyobaki. Aaaaah. ‘Eeh kwani hutaki ‘Mbona hamkumsapoti Mange na ninyi mtakuwa wanafiki, sijui mlikwama wapi. ‘Walinivunja dole la mwisho waliacha dole la kati. Eeh hii si ni nchi ya demokrasi mkimaindi basi mnawajua sasa mbona hamuwakamati. Tuache hayo. ‘Vipi korosho za Mtwara, maana wapiga kura wengi ni wakulima na wafanya biashara. ‘Kumnyima mpinzani ajenda, mtendee tu yaliyo mema. ‘Sio kumpelekea Difenda, mtaani tutie vilema. ‘Machozi ya Watanganyika hayatowaacha salama. Damu zilizomwagika milele zitawaandama. ‘Mwanangu akiwauliza wale waliyoniteka ni nani aliwatuma, mjibuni nimemzaa Mpare ila simchukii Msukuma. ‘Nchi inaangamia viongozi hawana maarifa na hawataki wakosolewe wanafanya kazi kwa sifa. Roma anazidi kushusha mistari kwa kuchana kuwa : ‘Uongozi ni kuacha alama chanya na kuwajibika. Kutekana, kuuwana sio sifa ya Mtanganyika... Msanii huyu wa Hip Hop amewahi kutamba na nyimbo kama ‘Nikifa nichimbieni makaburi matatu’, ‘Mathematics’, ‘Zimbabwe’. Huu ni mwendelezo wa Roma kuimba nyimbo zenye mashairi ya kijamii, baada ya kutoka kidogo na kuimba tungo za burudani.