Patcho: Afunguka yote kwa nini CP AcademiA sio FM Academia

Muktasari:

  • Swali limebaki kwa wadau wa muziki wa dansi, kwa nini CP Academia na sio FM Academia? Hapa wameanza tena maneno ya kuhisi ila Patcho amewaka wazi kwa Mwanaspoti kwa nini jina limebadilika.

NANI amekwambia Bendi ya CP Academia zamani FM Academia inayoongozwa na mwanamuziki Patcho Mwamba imekufa? Basi wewe unayesema hivyo utakuwa sio mhudhuriaji mzuri wa shoo zao au si mfatiliaji wa bendi hiyo.

Iko hivi. Baadhi ya watu waliamini baada ya mwanamuziki Nyoshi El Saadat kujitoa katika bendi ya FM Academi, bendi hiyo itakufa, lakini kadri siku zinavyozidi kwenda bendi bado inadunda na kuendeleza shoo zao kwenye kumbi mbalimbali za starehe jijini Dar es Salaam na mikoani.

Wengi walimtupia lawama Patcho Mwamba hataweza kuiongoza bendi hiyo, kutokana na kuwa na hasira za karibu na hata kujikontroo katika nidhamu kwani ni mmoja wa waliokuwa hawana nidhamu kwenye uongozi uliopita.

Hata hiovyo, Patcho Mwamba Lukusa amewaza kufanya vizuri na kuwaziba midomo wadau waliokuwa wakimtupia lawama ya kuwa atashindwa kuongoza bendi.

Mwanaspoti ni miongoni mwa kufatilia sana shoo za CP Academia na kushuhudia bendi hiyo katika shoo zao na kuonekana bado iko imara na ina ubunifu mpya pindi wanapokuwa jukwaani.

Swali limebaki kwa wadau wa muziki wa dansi, kwa nini CP Academia na sio FM Academia? Hapa wameanza tena maneno ya kuhisi ila Patcho amewaka wazi kwa Mwanaspoti kwa nini jina limebadirika.

Kwa nini CP Academia, sio FM Academia

“Unajua CP Academia ndio bendi tunavyojiita sasa hivi na hii ni kutokana na Mzee Martin Kasyanju ambaye alikuwa mmiliki wa Bendi ya FM Academia kufariki dunia. Walioachiwa bendi walishindwa kuendesha, ikawa vyombo vimechakaa na wanamuziki walikuwa hawapati haki zao, ndio maana nikaamua kuachana na jina la FM Academia na kuunda jina la CP Academia,” anasema Patcho Mwamba.

“Bendi ya CP Academia ipo chini yangu na tunashukuru tayari tumeshapata vyombo vipya, kama ulivyoona katika shoo zetu hakuna tatizo la vyombo kuharibika kama zamani kabla hatujabadilisha jina la CP Academia, hivyo tunashukuru sana na mashabiki zetu wasiwe na wasiwasi na sisi kuwa tunaweza ishia njia, labda niwaambie tu tumejipanga bendi yetu ya CP,” anasema Patcho.

wanamuziki kuhama

“Mimi nashangaa hizi habari zinazosemwa CP Academia kuna wanamuziki wamehama bendi, sijui zinatoka wapi? Ndio maana wakati mwingine huwa sipendi kujibizana na watu wanaounda unda maneno ili mradi tu kukuchafua.

“Ukweli, tangu bendi ya CP Academia kuanzishwa hakuna mwanamziki tulieanza nae alie hama, isipokua mpiga drum, Bally ndio hatupo nae tena kutokana na utovu wa nidhamu na hasa kuzidisha ulevi na matusi kwa wanamuziki wenzake,” anasema Patcho.

CP Academia imepania

“Tunatarajia kuzindua bendi pamoja na album mwezi ujao (Februari) tarehe ya uzinduzi tutawajulisha, pia lengo letu ni kwenda mbele zaidi na sio kurudi nyuma. Hata baadhi ya wadau wakiturudisha nyuma kwa maneno ya kashfa na dharau, sisi hatukati tamaa, tena ndio wanatupa akili ya kupiga kazi,” anasema Patcho.

Ampa makavu ‘live’ Toto Ze Bingwa

Huko mtaani Rapa Toto Ze Bingwa anasema amejitoa CP Academia kwa kuona sio sehemu sahihi kwa uwezo aliokuwa nao, huku akitupia maneno ya kashfa kwenye mtandao wa kijamii Facebook. Patcho Mwamba anasema mwanamuziki aliyeondoka CP ni mpiga drum, Bally Tempo tu, hii imekaaje? Hapa anafafanua kwa nini asimtaje na Toto Ze Bingwa ameondoka?

“Yaani nikisikia habari za Toto Ze Bingwa huwa nacheka sana na kuzidharau, naona kabisa anatafuta kiki ili imbusti asionekane kapotea katika muziki, ila ukweli Toto Ze Bingwa hakuwa rasmi CP Academia na amejiondoa mwenyewe baada ya kudai Rapa mwenzake Hitler anamroga sababu ya Hilter kutunzwa sana kuliko yeye.

“sasa inshu ilikuwa hivi: kulikuwa na shoo pale Coco Beach, siku hiyo kuna mdau (Mwanaspoti jina tumelihifadhi) akaenda mbele kutunza, akamtunza Toto Ze Bingwa elfu thelathini huku Rapa mwenzake Hitler akatunzwa laki mbili, hapo hapo akaanza kutamka kwa kumtaja jina huyo mdau sikuimbi tena kwa kuwa umenipa pesa ndogo, kama inavyoeleweka Toto Ze Bingwa ni mbinfasi, mbishi na hapendi kukosolewa, wenyewe mnamwona huko katika mitandao ya kijamii basi hata katika bendi yuko hivyo, mimi nikamchukua nikamtoa nje kuongea nae, lakini tulishindwa elewana na hadi kufikia hatua ya kunivunjia maiki aliporudi ndani.

“Ndio maana mimi nawasoma tu baadhi ya wadau wanaompa sapoti Toto Ze Bingwa pindi anapoongelea vibaya CP Academia, kwani hawajui walijualo, labda niwaweke wazi leo kwa nini Ze Bingwa alifika CP Academia. Ze Bingwa alikuwa anaishi kwa mwanamke akafukuzwa na kwa kuwa wanaelewana na Mule Mule, ndio akaja kumwombea kwangu ili ajiunge na CP Academia, mimi nikamwambia Mule Mule unazifahamu lakini tabia za Ze Bigwa, je amebadirika? Mulemule akaniambia amebadirika, basi nikamwambia aje tumwangalie kwanza, sasa hata miezi mingi haijafika ndio akazua hilo la ugomvi na rapa mwenzake.”

Hata hivyo Patcho Mwamba aliendelea kusema, Wakati tunamwangalia Toto Ze Bingwa hakuwa na sehemu ya kulala baada ya kufukuzwa na mwanamke, hivyo mimi nikamchukua kwenda kumlipia hoteli, lakini bado akawa ananitolea maneno ambayo hayana nidhamu huku akiniambia nimpeleke kwa bosi wa bendi ya CP Academia ili akamwelezee matatizo yake ya kurogwa na rapa mwenzake na mambo mengine. Mimi nikamwambia bosi ni mimi wa bendi hakuna bosi mwingine, hapo ndipo akaamua kuondoka na kuanza kuandika maneno ya kashfa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wanamsapoti kwa kutojua ukweli.”

Aidha Patcho anasema kama yeye ni mbaya na CP Academia ina matatizo, anaomba watu wamwangalie Toto Ze bingwa kwa nini atulii kwenye bendi na kuacha kuonekana katika baadhi ya video anaziomba Audio?

“Hivi wakati mwingine haina haja ya kutumia nguvu, sawa Ze Bingwa anaisema vibaya CP Academia kuwa tuna tatizo, embu kaangalie ile wimbo wa Binadamu binadamu, Ze Bingwa alirapu katika ule wimbo, kwa nini hakuonekana katika video akaondoka?

“Ze Bingwa alikuwa katika bendi ya Christian Bella, kuna nyimbo amerap, watu wajiulize kwa nini katika video haonekani na aliondoka katika bendi? Sasa ije kuwa CP Academia alipokuwa katika majaribio? Acha watu waongee ila wakitaka ukweli waje kama wewe ulivyokuja kuuliza na hata ukienda kumuuliza Ze Bingwa haya ninayosema najua atabisha japo ukweli anaujua.”