Mkali wa miondoko ya Kizulu, afariki dunia

Muktasari:

Taarifa hiyo haijabainisha ugonjwa uliopelekea umauti wa Shabalala.
Mwanamuzuiki huyo alifahamika zaidi kama muasisi na muongozaji wa kikundi cha kwaya cha Ladysmith Black Mambazo, kilichoshinda tuzo tano Grammy na kushiriki katika albamu ya Graceland ya Paul Simon.Shabalala alikianzisha kikundi hicho mwaka 1964.

Dar es Salaam. Muasisi wa muziki wa kitamaduni wa Zulu wa nchini Afrika Kusini, Joseph Shabalala amefariki dunia akiwa hospitalini mjini Pretoria.
Shabalala aliyesaidia kuutambulisha muziki wa kitamaduni wa Kizulu ulimwenguni amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 78.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Meneja wa bendi ya Ladysmith Black Mambazo, imesema kuwa Shabalala amefariki dunia katika hospitalini mjini Pretoria nchini Afrika Kusini.
Taarifa hiyo haijabainisha ugonjwa uliopelekea umauti wa Shabalala.
Mwanamuzuiki huyo alifahamika zaidi kama muasisi na muongozaji wa kikundi cha kwaya cha Ladysmith Black Mambazo, kilichoshinda tuzo tano Grammy na kushiriki katika albamu ya Graceland ya Paul Simon.Shabalala alikianzisha kikundi hicho mwaka 1964.
Shabalala alizaliwa mwaka 1941, akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto wanane katika kijiji cha Tugela karibu na mji wa Ladysmith nchini Afrika Kusini.
Alilazimika kuacha shule akiwa na umri wa miaka 12 baada ya baba yake mzazi kufariki dunia na kufanya kazi katika mashamba kabla ya kuingia kufanya kazi katika kiwanda.
Katika muda wake wa ziada alipendelea kuimba na rafiki zake katika kikundi cha watu weusi
Baadaye alikuwa kiongozi na mtunzi mkuu wa kwaya ambaye alijikita katika nyimbo za Zulu waliocheza ngoma ya kikundi cha Afrika Kusini cha muziki wa kitamaduni ambao mara nyingi ulikua na muziki laini na dansi ya kuvutia.
Walijulikana kwa jina la Ladysmith Black Mambazo, jina ambalo limekuwa kama utambulisho likiwa na maana maalum.
Ladysmith iliwakilisha mji wao, Black ikimaanisha dume la ng'ombe lenye nguvu kijijini kwao huku Mambazo kutoka neno la kizulu linalomaanisha shoka, ikiwa ni ishara ya uwezo wa kikundi hicho wa kushinda katika mashindano
Walipata umaarufu duniani baada ya kupewa kazi ya kuimba katika albamu iliyouzwa mamilioni ya pesa ya Paul Simon iliyojulikana kama Graceland, hasa katika wimbo wao wa Homeless, wimbo ulioandikwa na Shabalala akishirikiana na Simon, iliyotokana na wimbo wa harusi ya kitamaduni ya Wazulu.
Shabalala alistaafu kucheza katika matamasha mwaka 2014 muda mfupi baada ya kucheza katioka tamasha lililoandaliwa kwa ajili ya Nelson Mandela.
Lakini aliendelea kufundisha kwaya za muziki wa kitamaduni, huku watoto wake wanne wa kiume na mjukuu wake mmoja wakiendeleza kipaji chake ndani ya kundi la Ladysmith Black Mambazo.
Mbali na muziki, marehemu enzi za uhai wake alitamba pia kwenye filamu na baadhi ya kazi zake ni pamoja na 'On Tiptoe' na 'Gentle Steps to Freedom'.