Miss Utalii Morogoro yashika kasi

Muktasari:

  • Zawadi za Miss Utalii zitakazotolewa ni pamoja na vinyago vya thamani, washindi kupata ajira katika hoteli za kitalii na kuingia mikataba ya matangazo katika kampuni makubwa

Morogoro. Zaidi ya walimbwende 35 kutoka vyuo vikuu vinne mkoani Morogoro wanatarajia kuchuana kugombea taji la Miss Utalii 2018 likalofanyika Desemba 22 mwaka huu mkoani hapa.

Vyuo hivyo ni pamoja na chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), St Joseph Kihonda, Mzumbe na St Jordan.

Mkugenzi wa kituo cha taarifa za utalii Morogoro, Samson Kahabuka alisema kuwa shindano la kumsaka Miss Utalii 2018 litashirikisha zaidi ya warembo 35 na mshindi wa kwanza ataibuka kwa kupata ajira katika kituo cha taarifa za utalii Morogoro.

Kahabuka alisema kuwa lengo la kuwashindanisha warembo hao sio kuwapatia zawadi kama gari isipokuwa ni kupata mabalozi watano kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Morogoro.

“Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi vya kitalii ambavyo vingi vyao havijapata fursa mzuri ya kutangazwa na ujio wa shindano hili ni kupata mabalozi wataotangaza vyema vivutio hivyo.”alisema Kahabuka.

Kahauka alisema zawadi zitakazotolewa ni pamoja na vinyago vya thamani, washindi kupata ajira katika hoteli za kitalii na kuingia mikataba ya matangazo katika kampuni makubwa.

Mmoja wa shindano hilo, Joaniter Ernest alisema matarajio yake endapo ataibuka kidedea kuwa atatumia kutangaza vivutio vya mlima Udzungwa.

Joaniter alisema kuwa safu ya milima ya udzungwa ina vivutio vingi ikiwepo aina 11 ya nyani ambapo aina tano za wanyama hao hawapatikana sehemu yoyote duniani zaidi ya milima hiyo.

“Udzungwa kuna vivutio vingi kwani kuna aina 11 ya nyani na aina tano za nyani hao hawapatikani sehemu yoyote dunia na kuna aina 400 za vipepeo na aina tatu za vipepeo hao hawapatikani sehemu yoyote dunia,” alisema Joaniter.

Naye Berita Mdachi alisema kuwa kuna baadhi ya vivutio havijulikani kutokana na kutotangazwa huku jamii ikiwa na mawazo kuwa Arusha ndio mkoa wenye vivutio vikubwa kumbe na Morogoro una vivutio vikubwa pia.

Kiongozi wa warembo hao, Neema Mathayo alisema kuwa warembo hao wataingia kambini kesho Jumanne (Desemba 11) na kufundishwa vitu mbalimbali.

Neema alisema kuwa wakiwa kambini anahakikisha anasimamia nidhamu na watatembelea vivuti mbalimbali vilivyopo Morogoro.