Mastaa hawa walikosa taji Miss Tanzania, Bongo Muvi ikawatoa

Muktasari:

Achana na Wema Sepetu, ambaye aliingia katika tasnia ya ya filamu baada ya kushinda shindano la Miss Tanzania 2006, hawa hapa ni warembo ambao waliingia kwenye Bongo Movies baada ya kushindwa kufurukuta katika Miss Tanzania.

HII sio ya kubisha. Mastaa wengi ambao wanawika kwenye tasnia ya filamu za Bongo chimbuko lao ni kutoka kwenye shindano la urembo la Miss Tanzania.

Achana na Wema Sepetu, ambaye aliingia katika tasnia ya ya filamu baada ya kushinda shindano la Miss Tanzania 2006, hawa hapa ni warembo ambao waliingia kwenye Bongo Movies baada ya kushindwa kufurukuta katika Miss Tanzania.

LULU DIVA

Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ alishiriki Miss Pwani 2013 na kuwa mshindi wa pili. Kisha akawa mshindi wa Miss Kibaha wa mwaka huo huo. Baada ya hapo akawa kwenye listi ya kushiriki Miss Tanzania hakufanikiwa kushinda.

Baadaye Lulu Diva akaibukia katika muziki wa Bongofleva na kufunika na ngoma zake kali kama Usimwache, Homa, Utamu, Nilegeze, ‘Ona’ ft Rich Mavoko, ‘Milele’ ft Barnaba, ‘Naogopa’ ft Mr Blue na ya sasa ‘Come Again’ ft Eddy Kenzo.

Huku akiendelea kubamba katika gemu ya Bongofleva, Lulu Diva amejitosa katika fani ya maigizo akitisha katika tamthilia ya ‘Rebecca’ inayorushwa na DStv.

HAMISA MOBETO

Mwaka 2011 Hamisa alishiriki mashindano ya Miss Dar Indian Ocean na alifanikiwa kushika nafasi ya pili. Mwaka huohuo pia akawa mshindi wa pili wa Miss Kinondoni na kufanikiwa kuingia kwenye nusu fainali ya Miss Tanzania. Mwaka 2012, Hamisa alishiriki kwenye mashindano ya Miss University Afrika na kuingia hatua ya 10 bora.

Baada ya kutoka kapa alitumbukia kwenye Bongo Movies.

Baby mama huyo wa Diamond Platnumz na Majizzo, bosi wa Efm Radio na TV, hivi karibuni pia ameingia katika bongofleva kwa kuachia nyimbo zake kama ‘Madame Hero’ na ‘Tunaendana’.

IRENE UWOYA

Ni miongoni mwa nyota wa Bongo Movies waliopitia kwenye Shindano la Miss Tanzania akitokea Wilaya ya Kinondoni mwaka 2006. Uwoya aliibuka kwenye tano bora, lakini baada ya hapo aliangalia upande wa filamu akakubalika, hadi leo anawika na ana jina kubwa nchini.

Uwoya, mbali na kutamba katika filamu za Bongo kwa muda mrefu pia amekuwa akifunika katika tamthilia mbalimbali za televisheni.

AUNTY EZEKIEL

Alikuwa ni mmoja wa wawashiriki wa Miss Tanzania 2006, lakini hakuweza kufanya vizuri. Aliamua kuangalia upande mwingine wa uigizaji ambapo kwa mara ya kwanza alionekana kwenye Filamu ya ‘Miss Bongo’. Kuanzia hapo alianza kuwika na mpaka leo hii ni staa mkubwa nchini.

FLORA MVUNGI

FLORA Mvungi aliwahi kuwa Miss Pwani 2008, alinyakua taji la Miss Kanda ya Mashariki kwa mwaka huo. Aliposhindwa katika shindano la taifa la Miss Tanzania akageukia kwenye fani ya kuigiza na hadi sasa ana jina kubwa hapa nchini.

JOKATE MWEGELO

Alishiriki shidano la Miss Tanzania mwaka 2006 na kukamata nafasi ya pili. Baada ya kushindwa kutwaa taji hilo aliendelea kufanya mambo mengine ikiwamo ujasiriamali kupitia brandi yake ya Kidoti na pia kujiinguza kwenye uigizaji wa filamu.

Mwaka wa 2007, alipata kucheza filamu yake ya kwanza iliyojulikana kwa jina la Fake Pastors, akiwa na Vincent Kigosi, Lisa Jensen, mshindi wa tatu wa Miss Tanzania 2006 na marehemu Adam Kuambiana.

Mwaka wa 2008, alicheza katika filamu ya ‘From China With True Love’.

Mwaka wa 2010, alionekana katika filamu ya ‘Chumo,’ filamu iliyoandaliwa na Media for Development International, kuhusu elimu juu ya ugonjwa wa malaria. Filamu hii ilimwezesha kupata tuzo ya Zanzibar International Film Festival (ZIFF) akiwa kama mwigizaji bora wa kike kwa 2011 na kuchaguliwa kama mwigizaji wa Pan-Afrika katika tuzo za 2012 Nigeria Entertainment Awards.

Vilevile alipata kuonekana katika tamthilia maarufu ya ‘Siri Ya Mtungi’, iliyoandaliwa na Jordan Riber na kuongozwa na Karabani mwaka 2013. Mwaka wa 2014, alicheza uhusika wa “Ndekwa” katika filamu ya ‘Mikono Salama’, ambayo ilimwezesha kupata tuzo nyingine ya ZIFF akiwa mwigizaji bora wa kike kwa filamu za Kiswahili.

Jokate aliyezaliwa Machi 20, 1987, mbali na uigizaji wa filamu, pia ni mjasiriamali na mwanasiasa. Julai 2018 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.

CHUCHU HANS

Naye alianzia kwenye Shindano la Miss Tanzania mwaka 2005 akitokea jijini Tanga. Chuchu aliibuka kidedea kwenye Miss Talent. Baada ya hapo alijitumbukiza kwenye filamu na mpaka sasa ni mwigizaji mzuri. Alianza kutamba kwenye filamu yake ya kwanza ya ‘Roho Sita’.

Baby mama huyu wa muigizaji Vincent Kigosi, aliyezaa naye mtoto mmoja, kwa miaka mingi sasa amekuwa akitisha katika anga la filamu na tamthilia nchini.

MIRIAM JOLWA ‘JINI KABULA’

Alishikilia Taji la Miss Kariakoo miaka ya nyuma lakini alishindwa kutwaa taji la Miss Tanzania. Baadaye akageukia kuigiza na alianza kuwika kwenye tamthilia ya luninga ya ‘Jumba la Dhahabu’ iliyompa jina la Jini Kabula.

Tangu hapo, Jini Kabula amekuwa mmoja wa wasanii wakubwa wa filamu nchini akifanya yake katika muvi mbalimbali za Bongo.