Mabadiliko kanuni za filamu yafyeka tozo kibao za vibali

Muktasari:

Mabadiliko ya kanuni ni matokeo ya kikao kati ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wadau wa filamu kilichoketi Aprili, 2019 ambapo alikubali maombi ya kufanyika maboresho ya kanuni zilizopo ili ziendane na mazingira.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amezindua kanuni mpya za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza za mwaka 2020 zikionyesha kukata gharama nyingi za uendeshaji katika tasnia hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumanne Agosti 4,2020 katika ukumbi wa habari (Maelezo) ambapo ni matokeo ya kikao kati ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wadau wa filamu kilichoketi Aprili,2019 ambapo alikubali maombi ya kufanyika maboresho ya kanuni zilizopo ili ziendane na mazingira.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Katibu wa bodi ya filamu, Kiagho Kilonzo na mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Frowin Nyoni na viongozi wa vyama vya wasanii wa filamu.

Akizungumza katika hafla hiyo,Waziri Mwakyembe amesema kanuni hizo zimelenga kuikuza na kuboresha sekta ya  ndani ya filamu

Katika mabadiliko hayo ameelezq kuwa wamejitahidi kubadilisha asilimia 80 ya kanuni za mwaka 2011 zilizokuwa zimepitwa na wakati huku gharama nyingi walizokuwa wakitozwa wasanii zikiondolewa.

Gharama hizo amezitaja kuwa ni pamoja na tozo za kila mwaka kwa upande wa uhakiki na utoaji madaraja.

"Kuanzia sasa filamu itahakikiwa mara moja tu na haitakuwa ikihuishwa tena kama ilivyokuwa  awali ambapo tozo zilikuwa ni kwa kila mwaka.

"Pia tumepunguza ada ya kibali cha kutengeneza filamu kutoka Sh500, 00 hadi Sh50,000 huku uhakiki kwa upande wa tamthiliya  sasa itakuwa Sh500 kwa dakika badala ya Sh1000 iliyokuwa awali,"amesema Waziri Mwakyembe.

Jingine amesema katika kanuni hizo tozo ya wasambazaji wadogo imekuwa Sh36,000 badala ya Sh500,000 ya awali.

Awali Mwenyekiti bodi ya filamu, Profesa Frowin Nyoni amesema imewachukua muda mrefu kufanya mabadiliko katika kanuni hizo kwa kuwa walitaka kuifanya kazi hiyo kwa weledi na kitaalam zaidi.

Kwa upande wao wasanii, akiwemo Dennis Sweya maarufu Dino, ameishauri serikali kuangalia pia suala la malipo kwa kazi wanazozipeleka katika vituo vya televisheni.

Katika maelezo yake Dino, amesema wakati awali wasambazaji wa kazi hizo ndio walikuwa wakilalamikiwa kwa unyonyaji was kazi zao lakini sasa hivi vituo hivyo ni zaidi ambapo kazi uliyotengeneza kwa Sh3 milioni unaweza kujikutwa unalipwa Sh900,000.

Naye Ahmed Olotu (Mzee Chilo) amemuomba Waziri huyo mwenye dhamana na sanaa kuangalia nna gani wataweza kupata maeneo halisi ya serikali na sare wanazovaa watumishi ili kuleta uhalisia kwenye filamu zao.