Kipemba: Kifo Bongo Movie kimetuvuruga tu

Muktasari:

Mwanaspoti ilifanya mahojiano maalumu na Kipemba na kumsukumia swali ili kuchochea mahojiano, swali lenyewe ni:- Ni kitu gani kilichowafanya wakongwe wa Bongo Movie wajikite kwenye tam-thilia katika siku za karibuni?

ISSA KIPEMBA ni kati ya wasanii wenye ufahamu mkubwa. Unapozungumza naye lazima akufikirishe kutolichukulia jambo kawaida. kiufupi ni mtu unayeweza kupata ufahamu wa mengi kutoka kwake.

Kimuonekano, nyota huyu wa filamu nchini ni wa kawaida sana na ni mcheshi. Hachoshi kumsikiliza. Ana njia nyingi za kumfanya mtu asimchoshe katika maongezi yake na wakati mwingine kusahau dhiki zake na kuja kuzikumbuka ukiachana naye. Bila ya kuzungumza naye huwezi kujua madini yaliyopo kichwani mwake. Naiona kesho ang’avu kwa Kipemba kama hazina kwa taifa letu kama atatumika.

Mwanaspoti ilifanya mahojiano maalumu na Kipemba na kumsukumia swali ili kuchochea mahojiano, swali lenyewe ni:- Ni kitu gani kilichowafanya wakongwe wa Bongo Movie wajikite kwenye tam-thilia katika siku za karibuni?

Analijibu swali hili kwa kirefu, kubwa zaidi ametaja mazingira kuwa ndiyo yanawalazimu kukimbilia katika tamthilia hizo za televisheni baada ya soko la Bongo Movie kuporomoka.

Anamkubali sana Mwalimu Shaban Robert hasa aliposema ‘Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajinyima ushirika wa milele unaotarajia kutokea baada ya kushindwa uongo”.

Kisha akafafanua kwamba ukweli ni lazima usemwe kuhusu kitu gani kimekwamisha filamu za Kiswahili. “Napenda sana kusoma na kujifunza na huo msemo wa Shaban Robert unaishi kwenye maisha yangu,” anasema.

Anasema: “Ujuaji wa tusichokijua kwetu wasanii ni moja ya sababu ambazo zinafanya sanaa ishindwe kwenda mbele, kwamba tunashindwa kujifunza vitu vipya kila siku kwa maana ya mazingira yanavyobadilika.”

Msemo wake ambao anapenda watu wajifunze ni huu ‘Kuna tofauti kubwa kati ya uwezo wa kufikiri na maendeleo ya sayansi na teknolojia’.

Anatanabaisha kuwa ipo haja ya wasanii wengi kuwekeza kwenye kufikiri kwa kuwa teknolojia ipo na inabuniwa kila siku, ni vema kuwekeza kwenye kujiweka sawa kwa matumizi ya teknolojia hiyo.

Kipemba amefunguka mengi yenye funzo ndani yake, endapo yakifanyiwa kazi basi anaamini kuna hatua zinaweza kupigwa kwenye fani ya burudani nchini.

KUHUSU FILAMU

Kipemba anasema wasanii wengi hawazingatii vitu vinavyotakiwa kwenye filamu, akisisitiza zaidi kwenye utafiti.

“Ili filamu iwazungumzie wahusika kwa maana ya uliowalenga kwa kuzingatia eneo la kijiografia, elimu, jinsia, umri, imani na hata kiwango cha uelewa, lazima ufanyike utafiti kujua hali halisi huku ukilinganisha na hali halisi kwenye nyanja zote za uchumi, siasa na jamii kwa ujumla, kiufupi walaji wa bidhaa yako wajione wao kupitia waigizaji,” anasema huku akicheka kwa bashasha.

Kisha akachomekea ‘Watanzania wanapenda ‘tuvitu tuzuri tuzuri.’

Anataja kukosekana kwa ubunifu wa kweli kuwa ni sababu mojawapo ya Watanzania kuhamisha mapenzi yao, yamehamia kutazama sinema za Kihindi, Kikorea, Kinigeria ambao wanaigiza maisha yao halisi.

“Fanya utafiti, pita mitaani uone kama kuna Watanzania wanazungumzia sinema za hapa nyumbani, utakuta wanabishana ama kuelezea za nje hasa zilizotafsiriwa, ina maana kwamba wanapenda uhalisia na tuvitu tuzuri tuzuri.”

“Kimsingi tunategemea zaidi soko la ndani, sinema zetu tunapenda kuigiza kwenye majumba ya kifahari, magari ya kifahari ambapo mtiririko wa hadithi hauwiani na vitu hivyo, Mtanzania akijitazama hajioni na wala haioni hadithi au kisa na mkasa anachokifuatilia na mbaya zaidi ni kwamba filamu ikianza tu anakuwa keshajua itaishaje, halafu tunataka kuwapelekea kazi zetu! Nani atanunua ama kutazama? Watanzania wajanja,” anasema.

ANAZIITA HOME VIDEO

Anasema: “Wasanii wengi tunaigiza ‘Home Video’, video za kuangalia majumbani na sio filamu za kibiashara na ndio sababu haziwezi kufika popote. Hiyo ni moja ya sababu ya sanaa kuporomoka na hadhi ya wasanii kushuka.”

Japokuwa wasanii wengi wanalalamikia kutowekewa mazingira mazuri ya kibiashara ma serikali, Kipemba anasema serikali haitengenezi filamu, Filamu hutengenezwa na wasanii, bado wasanii tuna jukumu la kutengeneza filamu nzuri zinazoweza kushindana kwenye soko ili kuishawishi serikali kuona sababu ya kuharakisha Sera ya Filamu nchini.

WANAOTAMBA MAKOMEDI

Anasema kazi zinazotamba sokoni kwa sasa ni za wasanii wa vichekesho baadhi yao amewataja ni Joti, Mbotonyo, Mpoki, Kingwendu, Madebe Lidai ‘Nabii Mswahili’, Senga, Pembe, Mau Fundi na wachekeshaji wote wanaoigiza uhalisia wa Watanzania. “Kama huamini nenda Kariakoo Mtaa wa Likoma ukajionee.

“Hao nimewataja baadhi, ukipita kila sehemu ndio unaona kazi zao zinanunulika sana, pia wanazungumzwa mitaani kwani wanagusa maisha ya Watanzania,” anasema.

FASIHI KWA KISWAHILI/FASIHI YA KISWAHILI

Anasema kuna utofauti kati ya fasihi kwa Kiswahili, aliyoielezea ndio zile sinema ambazo sio za Kitanzania lakini zimetafsiriwa kwa Kiswahili “Ndio maana unakuta filamu za nje ambazo zimetafsiriwa kwa Kiswahili zinapendwa na wengi, kwa kuwa zina simulizi nzuri na zimeandaliwa kimuktadha, Filamu na Tamthilia zilizotafsiriwa ziwe chachu ya kutuzindua kutengeneza kitu kizuri na sio kulalama zizuiliwe.

“Fasihi ya Kiswahili, hii ni sanaa ya Waswahili kwa Muktadha wa Waswahili kwa lugha na utamaduni wa Waswahili, inamaana kwamba wasanii Tunatakiwa kuchukua maisha ya ukweli ya Watanzania, halafu unayawasilisha kwa njia ya fasihi kwa ulaini ambao wataelewa kwa kutumia wahusika wenye weledi wa kubeba dhamira husika,”anasema.

Ametolea mfano wa uingizwaji fenicha nchini miaka ya nyuma kidogo uliwadhoofisha sana mafundi seremala, ila baadhi yao walitafakari wakagundua kuwa inawapasa kuwa wakweli na kubwa zaidi Watanzania wanapenda ‘tuvitu tuzuri tuzuri’. (Anacheka) mafundi seremala wajanja wanashindana sokoni na bidhaa toka nje, hawalalamiki fenicha za kutoka nje zizuiliwe.”

UWEZO WA KUFIKIRI/SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Kipemba anasisitiza kukuhusu kutumia akili zaidi. Anaitaja kuwa ni sababu nyingine inayoangusha filamu za Kitanzania kwamba asilimia kubwa ya wasanii wanajikita kwenye vifaa badala ya fikra.

Anahoji filamu ya Andhaa Kanoon toka India ilirekodiwa na kamera ya 4K? au Light zake ni za LD? Mbona mpaka leo waangaliaji wapya wanalia?

“Unakuta wanafikiri wadada wazuri ambao kila mwanaume akimtazama anatikiswa lakini hana kipaji cha sanaa, kila anaeongea sana basi msanii, nani kakwambia kuongea sana nikuwa msanii? Kwani ndugu zetu wasiosikia unadhani hawafuatilii kazi zetu? Makamera mazuri, majumba ya kifahari hayafanyi filamu kuwa nzuri.”

Inaendelea Jumapili.