Jaydee, FA, Mr Blue sasa mbona mnatufokea!

Sunday August 02 2020
blue pic

MAISHA ya sasa vijana wanasema ni bora ukose kula kuliko kukosa bando. Japo kauli hii haina uhalisia, lakini inabeba picha kamili ya umuhimu wa kuwa internet katika maisha ya zama hizi.

Watu wanapiga pesa kupitia internet na taarifa zote za dunia zinapatikana haraka na ‘live’ kupitia mtandao huo unaoileta dunia pamoja. Unathubutu vipi kukaa mbali na internet?

Lakini wengi wanaosema ni bora ukose chakula kuliko kukosa bando la internet wanamaanisha hawako tayari kukosa umbea na vituko visivyoisha kwenye mitandao.

Moja ya vitu vinavyovutia kuhusu internet ni misemo na trendi za mambo yanazoibuka kila uchao na kuwakaa sana watu.

Moja ya trendi ya sasa ni huu msemo wa “Sasa mbona unatufokea.” Kila utakachofanya utaulizwa “sasa mbona unatufokea?” Iwe umeulizwa swali, ukawa unalijibu ama unatolea ufafanuzi jambo, ilimradi video yako ikipostiwa kwenye mitandao utaulizwa “mbona unatufokea?” Utaulizwa hivyo hata kama haujajibu kwa ukali. Iko hivyo hata ukiandika ujumbe tu, Insta kwa mfano, comments zitakazofuata utaulizwa “mbona unatufokea?”

Kuna mambo sana kwenye mitandao, ndio maana watu watadai ni bora ukose kula kuliko kukosa bando la internet.

Advertisement

Ndio maana katika safu yetu hii leo tunawauliza hawa kina Lady Jaydee, MwanaFA, Dully Sykes na Mr Blue, mbona wanatufokea?

Wanatufokea hawa wazee. True nakwambia. Kama hauamini angalia mambo wanayofanya hivi sasa katika shoo ya Tv E inayokwenda kwa jina la ‘Homa’. Wanatufokea.

Komando Jide ana miaka 20 kwenye game ya Bongofleva. MwanaFA ana miaka 19 kwenye muziki huu wa kizazi kipya. Babylon Bysar ana miaka 18 tangu alipoachia wimbo wake kwa kwanza aliouita ‘Mr Blue’ mwaka 2002.

Miaka 20 au 19 au 18 ni umri wa mtu mzima. Anazaliwa hadi anakuwa mtu mzima na pengine kuanzisha familia yake kabisa. Lakini hawa jamaa wapo tu kwenye gemu.

Kuwa katika gemu kwa muda mrefu kunasababisha mengi kuzungumzwa. Wengine watasema zama zimewapita, muziki umebadilika sana.

Ndio, muziki umebadilika sana. Ndio sababu wasanii wengi walioanza kutamba miaka hiyo, asilimia kubwa hawasikiki tena. Wameshapotea.

Hali hiyo inaweza kutufanya wengi kuingiwa na fikra wasanii wanaomudu kufanya muziki kwa wakati huu ni vijana wa sasa tu.

Lakini ukiangalia shoo za wakongwe hawa wa Bongo Fleva kina Jide, FA, Dully Sykes, Bysar wanachofanya kwa kutumbuiza na ‘live’ band, utaona hawa jamaa wanatufokea.

Wanatufokea kutuamsha usingizini. Jamaa wanapiga shoo za hatari na wanathibitisha kwenye hii game bado wapo wapo sana tu.

Dully anaweza kuwa ndiye msanii aliyetoa wimbo wake wa mwisho siku nyingi kidogo nyuma ukilinganisha na wakongwe wenzake hawa, lakini jamaa anatisha bhana.

Baada ya kufanya shoo yake ya nguvu kwenye ‘Homa’ kupitia tungo zake nyingi zilizompa umaarufu kama ‘Salome’ hadi ‘Inde’ aliyoirekodi na Harmonize ndani ya Wasafi Records mwaka 2017, Dully alienda kukaa kwenye drums na kuanza kuzidunda kwa umahiri mkubwa, akipiga sebene la wimbo ‘Selfie’ wa Koffi Olomide.

Shoo ya FA akitumbuiza na bendi ‘live’ kwa ngoma zakè kibao kuanzia ngoma ya ‘Mabinti’, ‘Mfalme’ hadi mpya ya ‘Gwiji’, hautataka amalize shoo.

Mr Blue ambaye ana umri wa miaka 32 sasa, anasema baada ya miaka minane ijayo, atapumzika muziki akijaaliwa kufikisha umri wa miaka 40 ili aweke nguvu katika ibada.

Lakini hadi wakati huo, kwa wanachoendelea kufanya sasa hawa wakongwe, wanatufokea.

Advertisement