JIACHIE: Zari ana balaa nyie!

Friday December 29 2017

 

By RHOBI CHACHA

ZARINAH Hassan ‘Zari The Boss Lady’, ambaye ni mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz, amechafua hali ya hewa huko mtandaoni na sasa pameanza kuchimbika kwelikweli.

Zari, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanawake wachache shupavu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, amelizua baada ya kusema Diamond amezaa na mwanamitindo, Hamisa Mobetto, kwa mbaya tu yaani ni kama vile mtoto anavyovunja glasi.

Mama huyo wa watato watano (wawili wa mwisho ndio wa Diamond), amesema hayo wakati akihojiwa na AyoTV kwenye maandalizi ya sherehe ya mwanaye, Nillan, iliyofanyika siku chache zilizopita.

Mwanadada huyo, ambaye hutumia muda wake mwingi kwenye mtandao wa Snapchat, amesema amemsamehe Diamond kwa kitendo hicho kwani, anajua amezaa na Hamisa kwa bahati mbaya.

Hata hivyo, Zari alisema pamoja na kumsamehe Diamond, endapo atarudia tena kuchepuka, basi itakuwa ndio mwisho wa mapenzi yao.

Alikwenda mbali na kusema atachukua watoto wake na kuwalea mwenyewe kama ilivyotokea kwa aliyekuwa mumewe, Ivan, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Kauli hiyo ndio iliyozua kizaazaa katika mtandao wa Instagram, ambapo mashabiki wengi wamemshambulia Zari wakimwambia hakuna mtoto wa bahati mbaya katika mapenzi.

Wengine wamemtaka aweke akiba ya maneno wakidai kwamba, asilimia kubwa ya wanaume hawachungiki hasa wanapokuwa katika umri kama wa Diamond, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa mastaa wenye mkwanja mrefu nchini.

Pia, wengine wamemshauri Zari aachane na mambo ya kuanika maisha ya familia yake katika mitandao badala yake apambane na hali yake na kulea familia.