Irene Uwoya aiomba serikali iwatumie vita ya corona

NYOTA wa filamu nchini, Irene Uwoya amesema wasanii wana jukumu la kukaa mstari wa mbele kuongoza mapambana dhidi ya ugionjwa wa covid-19 unaoenezwa na virusi vya corona na kuiomba serikali kuwatumia ili nao waishiriki vita hiyo.
Irene ameyasema hayo alipozungumza na Mwanaspoti baada ya kuulizwa kitu gani kinawafanya wasanii wa Tanzania wamejiweka nyuma kwenye vita hii kulinganisha na wale wa mataifa mengine hasa Ulaya na Marekani.
Kisura huyo amesema wasanii mara nyingi huwa mstari wa mbele kwenye vita ya majanga mbalimbali kwa vile hutumiwa na serikali na akaiangukia kwamba wasiwaache kipindi hiki kwa vile ni wajibu wao kuishiriki vita hiyo.
"Tumekuwa tukifanya mambo mengi sana katika kuhamasisha vitu vingi kwa jamii Ikiwemo kwenye makampeni, hivyo hata kwenye matatizo kama haya tunahitajika tutumike ili tushiriki nasi kutoa elimu ya ugonjwa huu unaosababishwa na corona," amesema Irene.
"Sasa ombi langu kwa Serikali na Wizara ya Afya, sisi wasanii tumejaa na tupo tayari kutumika kufanya kitu chochote ambacho mashabiki au watanzania Wanahitaji kupata elimu ya ugonjwa huu, mashabiki wetu tukiongea sisi wanaweza kusikiliza, kuangalia au kuchukua maneno yetu wakayafanyia kazi, kwani si unajua msanii ni kioo cha jamii," amesema, huku akisema hata hivyo wapo baadhi ya wenzao hasa waimbaji wametumia sanaa yao kutunga nyimbo za kuelimisha kitu ambacho ni kizuri na wengine kama wao wanatumia mitandao ya jamii kutoa elimu pia.
Irene aliyeanzia kwenye fani ya urembo mwaka 2006 kabla ya kuingizwa kwenye filamu akitambulishwa na kazi iitwayo Yolanda na kupata ujiko zaidi kupitia Oprah aliyoigiza na Steve Kanumba na Vincent Kigosi 'Ray'.
Kwa sasa mwanadada huyo ameshiriki zaidi ya filamu 50, huku kazi yake binafsi iitwayo Apple ikitajwa kama moja ya filamu bomba kuwahi kuigizwa nchini.