Hawa wanapiga fedha ndefu 2020

SOKO la filamu limeyumba sana mwaka huu kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona. Muvi nyingi zilizotakiwa kutengenezwa 2020 zilisitishwa, hata zile kubwa ambazo zilishakamilika na kupangiwa siku ya uzinduzi pia zilipigwa kalenda kwa kupelekwa tarehe za mbele. Hii ni kwa sababu zisingeweza kupelekwa kwenye majumba ya sinema kwa kuwa watu wangerundikana sehemu moja ambayo ni kinyume na tahadhari zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata hivyo, hiyo haina maana biashara ya filamu ilikufa kabisa, hapana wataalamu wa sekta mbalimbali zinazohusika na uandaaji wa filamu waliendelea kupiga madili na kuingiza mpunga kama kawaida na kwa kuthibitisha hilo hii hapa listi ya wacheza filamu waliopiga pesa nyingi zaidi mwaka huu.

Hapa chini ni orodha 10 bora ikiwa kwenye mpangilio wa nani ameingiza zaidi ya mwenzie. Lakini pia, mjumuisho wa pesa unatoka kwenye vyanzo mbali mbali ikiwemo mishahara ya kuigiza kwenye filamu na matangazo. Fedha hizo zipo kwa dola za kimarekani ambazo ukijumuisha kwa fedha za Kitanzania ni nyingi kwelikweli.

1. The Rock 87.5M

Kwa mwaka wa pili mfululizo Dwayne Johnson anaendelea kuwa kinara kwenye listi hii. Mwaka jana pesa yake nyingi aliipata kupitia malipo ya kucheza filamu ambapo alilipwa kuigiza takriban filamu 8 huku tatu zikiwa tayari zimeshaachiwa ikiwemo Hobbs & Shaw na Jumanji The Next Level

Mwaka huu haijatoka filamu yoyote ambapo The Rock ameigiza ndani, lakini nyuma ya pazia ameshakula mipunga ya kuigiza filamu kubwakubwa ikiwemo hit inayoandiliwa na kampuni ya kutengeneza na kuuza filamu mtandaoni ya Netfilx inayoitwa Red Notice. Na kwa mujibu wa jarida la Forbes walisema alilipwa dola za kimarekani 23 milioni. Pesa zaidi amepata kwenye madili mengine ikiwemo la kuuza viatu vya mazoezi vya Projekt Rock. Kiwango cha fedha alichoingiza mwaka huu ni Dola 87.5 milioni ambazo ni kama Sh 202.9 bilioni.

2. Ryan Reynolds 71.5M

Staa huyu ya movie za DeadPool ameshalamba dola za kimarekani 20 milioni kwenye kazi mbili kutoka Netflix, movie ya 6 Undergrounds iliyotoka mwaka jana pamoja na Red Notice ambayo iko jikoni. Kiwango chake alichoingiza 2020 ni Dola 71.5M (kama Sh 165.8)

3. Mark Walhberg 58M

Jina lisikuchanganye, umemuona jamaa huyu kwenye movie kama vile Ted, Shooter na Pain & Gain aliyoigiza na The Rock mwaka 2013. Jamaa anashika nafasi ya tatu akiingiza Dola 58Milioni ambacho ni kama Sh 134.5 bilioni.

Mbali na uigizaji Mark ni mzalishaji wa filamu ambapo kwa mwaka huu ameingiza pesa nyingi sana kwa kuzalisha filamu-makala mbili ambazo ni Wahl Street na McMillions. Na kama hiyo haitoshi, movie yake ya komedi ya Spenser Confidential inashika rekodi ya movie ya tatu iliyotazmwa zaidi Netflix.

4. Ben Affleck 57M

Ben Affleck ambaye amewahi kuigiza movie za Batman pia ameingia kwenye listi ya waigizaji waliopiga pesa ya kutisha 2020 huku movie pekee alizoigiza mwaka huu zikiwa ni The Last Thing He Wanted na The Way Back. jamaa amevuta Dola 57milioni (kama Sh 132.2bilioni)

5. Vin Diesel 54M

Wote tunamjua, staa wa movie pendwa za magari na ushushushu za Fast and Furious. Mwaka huu, yeye na timu yake walitakiwa waachie movie ya Fast and Furious namba 9, lakini imeshindikana.

Hata hivyo Diesel ameendelea kupiga pesa kupitia filamu yake ya Bloodshot iliyotoka mwaka huu pamoja na kuprodyuzi series ya vikatuni ambayo stori yake imechomolewa kutoka kwenye movie za Fast Furious, series inatwa Fast & Furious Spy Racers. Jamaa kavuta Dola 54milioni ambazo ni kama Sh125.2 bilioni).

6. Akshay Kumar 48.5M

Muigizaji pekee kutoka nje ya Marekani kwenye listi hii. Staa huyu wa filamu kutoka Bollywood ameingiza pesa zaidi kupitia tamthilia yake ya kwanza kuandaa ya The End ambayo aliiuza kwa kampuni ya kuonesha filamu mita ndaoni ya Amazon Prime. Jamaa kaingiza dola 48.5 ambazo ni kama Sh112.5 bilioni).

6. Lin Manuel Miranda 45.5M

Ameigiza movie zisiozozidi 5 mpaka sasa na nyingi ni za muziki. Anaingia kwenye listi hii kwa mara yake ya kwanza kwa sababu ya dili nono alilopewa na kampuni kubwa zaidi ya kutengeenza filamu Marekani ya Disney. Jamaa ameingiza Sh 45.5 milioni ambazo ni kama Sh105.5 bilioni.

8. Will Smith 44.5M

Ukiachilia mbali kwamba amekuwa muigizaji anayelipwa pesa nyingi kama mshahara wa kuigiza, kwa mwaka 2020 jamaa amepata zaidi pesa kupitia dili alizosaini na mtandao wa kijamii wa Snapctah. Mwaka huu ameigiza kwenye movie mbili, kubwa ikiwa ni Bad Boys sehemu ya tatu. Kwa mwaka huu jamaa kavuna Dola 44.5 milioni ambazo ni sawa na Sh103.2 bilioni)

9. Adam Sandler 40M

Baada ya filamu yake ya Murder Myster kuwa filamu iliyopendwa zaidi kwenye mtandao wa Netflix, kampuni hiyo ikampa jamaa dili la kutengeneza movie zingine nne.

Kama hiyo haitoshi, Sandler ndiye muigizaji anayepata mgao mkubwa zaidi wa mapato kwenye mtandao huo licha ya kwamba mitandaoni kuna kundi kubwa la mashabiki wanaodai kutokumkubali.

Jamaa kaingiza Dola 40 Milioni ambazo ni sawa na Sh 92.8 bilioni.

10. Jackie Chan 40M

Haishangazi kumuona mtu kama Jack kwenye list hii, bado uigizaji wake umebaki kuwa pendwa. Hata hivyo pesa nyingi mwaka huu ameingiza kupitia madili yake mengine na kwenye orodha ya The Forbes jamaa kaingiza dola 40 milioni sawa na Adam ambazo ni sawa na Sh 92.8 bil.