MAMBO YA TANGA : Hata hiyo Bongo Movie ndiko ilikozaliwa hapo

Tuesday February 26 2019Mzee Amri Bawji (kushoto)

Mzee Amri Bawji (kushoto) 

By Myovela Mfwaisa

UNAWEZA kushangaa, lakini hivi ndivyo ilivyo. Suala la filamu inayojulikana kwa jina la Bongo movie ilianza rasmi katika Jiji la Tanga wakati huo ikiwa mkoa tu na si Jiji kama ilivyo sasa.

Asili ya filamu za kibiashara zilianzia Tanga na kuja kuvuma jijini Dar es Salaam. Vijana hasa wa kizazi kipya ukisema Bongo movie basi wenyewe wanajua tu ni Dar.

Filamu Tanzania ilianza kutengenezwa tangu miaka ya 1936 na hata baada ya uhuru ziliendelea sinema kutengenezwa lakini zilikuwa ni filamu za hamasa, hakukuwa na filamu za kibishara na kuzagaa kama sasa pamoja na kuwa sheria ya filamu Na. 4 ya mwaka 1976 kuwepo.

Mwaka 1995 filamu ya Shamba Kubwa ilitengenezwa Tanga chini ya Mwalimu El Siagi na kuwashirikisha wasanii kama Kaini, Hassan Master na Jimmy Master, na kupigwa picha na Hakim Bayakub ‘Kim’ hapa kwa mara ya kwanza ndio ilikuwa filamu ya kwanza kutoka, baadae zilitoka nyingine.

Hadi kufikia mwaka 2003 ilipotoka filamu ya Girlfriend bado Tanga walishatengeneza filamu kama Dunia Hadaa (2000), Maskani, Love Story Tanganyika na Unguja (1997), Augua na sinema nyinginezo ndio kijiti kilipopokelewa na Dar es salaam.

“Ukiachilia Dar es Salaam Tanga ndio Mkoa pekee uliokuwa na majumba ya sinema kama Dar es Salaam kila Wilaya kulikuwa na Jumba la Sinema, hicho ndio kichocheo kutengeneza filamu,” anasema Mzee Bawji.

Mzee Amri Bawji anasema Dar es salaam kulikuwa na majumba ya sinema ambayo ni New Chox, Avalone Cinema, Odeon Cinema, Star Light, Drive Inn, Cameo Cinema, Empire Cinema, na Empress Cinema pamoja na kuwa na majumba ya sinema ya kutosha lakini Tanga ilifanyia kazi.

Wakati kwa mkoa wa Tanga kulikuwa na majumba sinema kama Majestick Cinema, Tanga Cinema, Novert Cinema, Legal Cinema, pia katika Wilaya zote ambazo ni Pangani, Lushoto, Muheza na Korogwe kulikuwa na majumba ya sinema tofauti na mikoa yote ilikuwa na majumba mawili tu.

Uwepo wa majumba ya sinema yalikuwa ni kichocheo cha utengenezaji wa filamu kwani filamu kama Shamba Kubwa, Love Story na Tanganyika na Unguja, Dunia hadaa zilionyeshwa katika majumba ya sinema kwa nchi nzima na hadi leo bado hazijatoka katika video na kusambazwa.

Tanga pia ndio mkoa wa kwanza kuingiza filamu za Shamba Kubwa na Love Story Tanganyika na Unguja katika tamasha la kwanza Zanzibar International Film Festival( ZIFF) sinema zilizorekodiwa kwa Kiswahili.

Advertisement