Dj Sinyorita yuko hivi tuzo za AEAUSA

Friday October 9 2020

By NASRA ABDALLAH

DJ Sinyorita sio jina geni masikioni mwa watu, licha ya msichana huyo kuwa na miaka michache kwenye kazi hiyo ya kuchezesha santuri.

Sinyo, ambaye jina lake halisi ni Mwanaisha Said, mbali ya kufanya kazi hiyo katika shughuli mbalimbali ikiwemo kwenye kumbi za burudani, pia ni mwajiriwa wa kituo cha redio Clouds.

Hivi karibuni amekuwa miongoni mwa wateule katika tuzo za African Entertainment Awards, USA (AEAUSA), ambazo zitatolewa Desemba 12 mwaka huu nchini Marekani.

Kwa upande wa Tanzania jumla ya wasanii kumi wameingia kuwania akiwemo DJ Sinyorita katika kipengele cha DJ bora wa mwaka ambapo atachuana na maDJ wengine kumi kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumzia hilo, Dj Sinyorita, alisema ni furaha kwake kuona waandaji wa tuzo hizo bado wanathamini kipaji alichonacho.

“Hii sio mara ya kwanza kutajwa katika tuzo hizo, kwani mwaka 2017 pia niliingia lakini bahati haikuwa yangu, hivyo mwaka huu naomba Watanzania wanipigie kura kwa wingi ili niweze kushinda, kwani nitakaposhinda ushindi hautakuwa wangu peke yangu bali wa Watanzania wote,” alisema.

Advertisement

Katika tuzo hizo zilizoanza kutolewa 2015, wengine waliotajwa ni Diamond, aliyeingia katika vipengele vitano, Harmonize, Nandy, Maua Sama, Navy Kenzo, mtangazaji Lil Ommy, Rayvanny, Ali Kiba na prodyuza Abba kupitia wimbo wa Chibonge.

 

Advertisement