Diamond kurekebisha nyumba zote Tandale

Wednesday October 21 2020
tandale pic

Staa wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz amesema atazifanyia ukarabati nyumba zote za mtaa aliokulia wa Tandale jijini Dar es Salaam kama shukrani kwa wakazi wa mtaa huo kuishi naye vizuri.

Diamond amefunguka hayo leo kwenye mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwao Madale, Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni ya ‘Nguvu ya Rangi’ inayoendeshwa na moja ya kampuni ya kutengeneza na kuuza rangi ambayo Mondi anaihudumia kama balozi.

“Nataka ile Tandale ile, nyumba zote nizifanyie ukarabati pamoja na kuzipiga rangi ziwe za kisasa. Nimezungumza na wadau wanipe upendeleo huo na wamekubali.” alisema Diamond.

Ameongeza kuwa anatoa shukrani hiyo kwa sababu yeye na familia yake wamekulia mtaa wa Tandalae kwahiyo huenda hata anachokifanya sasa hivi kimechochewa na majirani aliokuwa akiishi nao na watoto wenzie aliokuwa akicheza nao.

Hii si mara ya kwanza kwa Diamond kurudisha shukrani kwa mtaa wa Tandale kwani mwaka 2019 alitoa msaada wa mikopo kwa kina mama, bodaboda za biashara kwa vijana pamoja na bima ya afya. Wakati nyuma ya hapo, mwaka 2018 aliachia Albamu yake ya tatu aliyoipa jina la ‘A Boy from Tandale’

Advertisement