A.K.A zilizogombanisha wasanii

Friday October 09 2020
AKA PIC

Baada ya kuachia wimbo wake mpya wa Mediocre, Alikiba alifanya intavyuu na media moja hapa Bongo. Mtangazaji akamuuliza ulikuwa unajaribu kuzungumza nini kupitia wimbo huo? Akajibu;

“Nimeona vitu vinatokea, watu wanajipa mavyeo. Kila mtu anataka kujiita King wakati tayari King nipo, na kwa kawaida mfalme huwa mmoja na siku zote huwa huyo huyo, habadiliki mpaka afe.”

Kwa maana nyingine, Alikiba anaamini jina la King au cheo cha mfalme wa Bongofleva linamfaa yeye kuliko msanii yeyote mwingine anayejaribu kujiita hivyo.

Sasa sio jina la King tu lililowahi kuwaingiza wasanii kwenye msuguano. Wasanii wengi maarufu wamekuwa wakijipa majina yenye kuelezea ukubwa wao au sifa wanazoamini wanazo. Majina kama Jeshi, Komando, Simba, Mnyama ni baadhi yao. Hata hivyo, mara kadhaa imetokea kuwa majina haya yameshatumika na wasanii wengine na hapo ndipo tatizo huanzia.

Hii hapa list ya majina au A.K.A zilizowahi kuwaingiza wasanii kwenye mgogoro.

RAIS WA MANZESE

Advertisement

‘Nickname’ hii iliwaingiza kwenye kivumbi wasanii Ney wa Mitego na Madee. Majamaa wote wamekulia Manzense Dar es Salaam, kwahiyo kutokana na umaarufu walionao, kila mmoja hujichukulia ndiye anastahili kuwa mwakilishi wa watu wa Manzense, kwa maana ya Rais wa Manzese.

Hata hivyo, Madee ndiye aliyeanza kutumia jina hilo, lakini mwaka 2009 Ney wa Mitego aliachia wimbo wake wa kwanza wa Itafahamika na akapata umaarufu na tangu hapo akaanza kusikika akijinasibu kuwa yeye ndiye Rais wa Manzese.

Mgogoro bado upo hai mpaka leo, wote wanaendelea kutumia A.K.A hiyo kwa sababu labda hakuna namna rasmi ambayo inaweza kufanyika na kuamua kuwa yupi anastahili kuwa Rais wa Manzese — labda mpaka zipigwe kura.

SHAROBARO

Kabla ya mwaka 2010 alikuwepo sharobaro mmoja tu Tanzania, prodyuza Bob Junior. Na yeye na timu yake walikuwa wakilitumia jina hili kumaanisha kwamba wao ndio vijana wasafi, watanashati, wanaojua kuvaa, mabishoo, mabitozi, na zaidi.

Lakini baada ya jina hilo kuvuma sana, akaibuka muigizaji mchekeshaji Hussein Ramadhani Mkieti maarufu Sharo Milionea (Mungu ailaze roho yake pema peponi) na akaanza kuigiza kama mtu mwenye miondoko ya kisharobaro huku akitumia jina hilo pia.

Jina Sharobaro likaanza kuonekana kumpendeza zaidi Sharo Milionea kuliko Bob Junior, na hapo ndipo jamaa akamaindi, akaanza kuhoji kwanini mchekeshaji huyo anatumia brandi yake tena kibiashara?

Kwa sababu hiyo, mchekeshaji huyo akaamua kubadilisha jina kutoka Sharobaro na kujiita Sharo Milionea, jina ambalo alilipata kutoka kwenye moja ya filamu zake — filamu ambayo aliigiza kama Sharobaro anayejifanya ana pesa nyingi sana.

Kwa sasa jina Sharobaro limebaki chini ya umiliki wa Bob Junior huku kielelezo pekee kwamba ni mali yake ikiwa ni studio yake ya kurekodia muziki ambayo bado inaendelea kuitwa Sharobaro Records kama zamani.

WASAFI

Jina hili liliwaingiza vitani Diamond na Bob Junior na matokeo yake yanafahamika na kila mtu leo hii.

Ilikuwa hivi: Bob Junior alikuwa ndiye prodyuza wa Diamond mwaka 2009, kwahiyo walikuwa ni washikaji, walikuwa wanatumia muda mwingi wakiwa pamoja, na Bob Junior alikuwa akijiita Rais wa Masharobaro, huku kwa mujibu wake akifafanua kwamba cheo hicho kin maanisha yeye ndiye Rais wa vijana wasafi, watanashati, wanaojua kuvaa, mabishoo, mabitozi, na zaidi — kwahiyo kwa lugha rahisi hata Diamond alikuwa Sharobaro pia.

Lakini baadaye wawili hawa wakaja kutibuana, wakawa maadui, wakaacha kufanya kazi pamoja, Diamond akachukua hamsini zake akasepa, Bob Junior akabaki na hamsini zake, na huko alipoenda Diamond akaanzisha ukoo wake wa kisanii na kuuita Wasafi.

Kupitia kwenye intavyuu nyingi Bob Junior ambaye pia amewahi kutamba na ngoma alizoimba za Oyoyo na Nichumu amewahi kuweka wazi kuwa jina analolitumia Diamond la Wasafi ni la kwake yeye kwa sababu linaishi ndani ya jina la Sharobaro.

Hata hivyo, ni kama Diamond aliziba masikio, akaendelea kutumia jina hilo na mpaka sasa limetengeneza mamilioni ya pesa huku likimiliki uwekezeaji mkubwa kama vile lebo kubwa ya muziki na kituo cha televisheni na redio hapa nchini.

MAMBA

Mchezo uko hivi, Shetta ambaye ametamba sana na ngoma kali kama Shirokobo na Namjua aliamua kujipa jina la mnyama na akajiita Mamba — jina ambalo taratibu likaanza kuzoeleka na raia mtaani.

Hata hivyo kabla yake, jina hilo lilikuwa linatumika na Dudu Baya, kwahiyo ghafla kuna siku ikasambaa video inayomuonesha mkongwe wa muziki wa kizazi kipya Dudu Baya akilalamika kuhusu kuibiwa jina la Mamba na Shetta.

 

Advertisement