Couple matata zinazobamba Bongo

Friday April 13 2018

 

By RHOBI CHACHA

HUKO Ulaya na Marekani kuna couple matata sana kama ile ya Jay Z na Beyonce, Brad Pitt na Angelina Jolie, P Diddy na Jenifer Lopez (JLO) pamoja na ile ya Justine Bieber na Selena Gomez.

Lakini, kwa taarifa yako hata hapa Bongo hakujalala kabisa kwani kuna couple zinazobamba kinoma hasa katika kipindi cha kuanzia miaka mitano iliyopita mpaka sasa.

Hata hivyo, katika couple hizo zipo zilizotemana lakini bado zimeendelea kubamba kutokana na kuwa na mvuto ama matukio yaliyokuwa gumzo kwa mashabiki.

Sasa hapa Bongo kuna mastaa wa Bongo Flava, Bongo Movie ambao couple zao zilibamba kwelikweli na mpaka sasa zimeendelea kuwa gumzo kwa mashabiki.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya couple matata kabisa ambazo zilinaendelea kubamba kinoma.

Diamond Platnumz na Zari

Mpaka sasa bado gumzo unaambiwa, japo wenyewe wamekuwa kimya baada ya kutemana tena kupitia ujumbe kwenye mtandao wa Instagram.

Penzi lao lilianza kuchipuka kama utani vile, lakini baadaye mambo yakawa hadharani na sasa wana watoto wawili, Tiffah na Nillan.

Nguvu kubwa ya penzi lao ilikuwa kwenye kundi kubwa la mashabiki huko kwenye mitandao, ambapo walikuwa wakinogesha penzi la wawili hao hadi kubamba kila kona ndani na nje ya Tanzania.

Kwa sasa wametemana na kila mmoja yuko kimya, lakini shughuli iko huko kwenye mitandao ambako, makundi yao yamekuwa yakipambana kila kukicha. Kuna Team Zari halafu kuna Team Diamond akisaidiwa na Team Mobeto na Team Wema, ambazo zimekuwa zikimponda Zari.

Japo Team Diamond yenyewe ipo kibiashara zaidi na kuendeleza kazi za Sanaa, hainaga sana mambo ya kuchambana kama hizo zinazomuungana mkono. Team hizo ndio zimeifanya couple hii kuendelea kubamba japo wamepigana chini.

Idris Sultan na Wema Sepetu

Hii couple unaambiwa ilikuwa na cheche kwelikweli, Idris Sultan ambaye ni mshindi wa Big Brother Africa 2014, alitua kwenye penzi la Miss Tanzania 2006 na supastaa wa Bongo Movie, Wema Sepetu.

Wawili hawa walinoga kwelikweli unaambiwa na kila shabiki wao aliufurahia kwani, walikuwa wanavutia kinoma. Idris alijikuta akizidiwa na nguvu ya umaarufu wa uhusiano wao na kuahidi kutouweka hadharani tena uhusiano wake kimapenzi. Wema na Idris walikaribia kufikia kwenye hatua ya kuanzisha familia tena watoto mapacha, lakini haikuwa hivyo. Bado suala la Wema kutopata mtoto limeendelea kuwa kidonda kibichi kinachotoneshwa mara nyingi.

Idris na Wema wamepitia majaribu mengi ambayo wakati mwingine huyashindwa kuyahimili na kuachana, lakini bado wanaonekana kupendana.

Kuna wakati video ya Wema ilisambaa mitandaoni akimbusu mwanaume mwingine, na hapo penzi la wawili hawa likavunjika kwa muda, lakini baadaye wakarudiana.

Alikiba na Jokate Mwegelo

Kama kuna uhusiano ambao umegubikwa na usiri mkubwa basi ni huu wa Jokate na Ali Kiba. Yaani unaweza kubisha mwaka mzima kuwa, mastaa hawa hawana uhusiano wa kimapenzi kwani kila mmoja alikuwa akiangalia mambo yake na hawakuwa na majigambo kama wengine.

Majizzo na Hamisa Mobetto

Majizo Dj maarufu aliyewika zamani, kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa EFM, Hamisa Mobetto na kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike.

Couple yao ilikuwa na nguvu sana hadi kufikia Majizo kutaka kumuoa Hamisa, lakini baada ya muda ikafahamika kuwa wametemana na Majizo kujiweka kwa muigizaji wa Bongo Movie, Elizabeth Michael (Lulu), ambaye kwa sasa anatumikia adhabu ya kifungo gerezani.

Kuachana kwa Hamisa na Majizo imekuwa simulizi hadi leo mashabiki zao wanaendelea kuitajataja na kukumbushia picha zao za kimapenzi pindi wako wapenzi.

Harmonize na Jacqueline Wolper

Kwanza watu hawakuamini kabisa, lakini baadaye kila kitu kikawa hadharani. Mmakonde akatangazia umma kuwa staa wa Bongo Movie, Jacqueline Wolper ndio vile tena.

Simulizi tamu za uhusiano wao zilikuwa zinavutia sana, japo wachache walikuwa wakiuponda kwenye mitandao ila wenyewe ilikuwa poa tu unaambiwa.

Ni kama ilivyo kwa Irene Uwoya na Janjaroo, hata kwa Wolper na Harmonize wapo waliodhani ni kiki tu ya kutafuta mashabiki.

Hata hivyo, baada ya wawili hawa walikuja kutemana na maneno ya shombo yakashika kasi kwenye mitandao huku baadhi ya nyimbo zikitungwa na watu kudai zina maana yake.

Wolper alizama kwenye penzi lingine na Haemonize naye akatua kwa mzungu wake, Sarah lakini bado mashabiki wanaikumbuka couple hiyo kwani, ilibamba kinoma.

Wema na Diamond

“Diamond Platnuzm ila mimi nimezoea kumuita Naseeb, yes hivyo tu,” aliwahi kusikika Wema akizungumza na kituo kimoja cha redio kuhusiana na uhusiano wake na Diamond.

Penzi hili halikuwa na kificho kabisa na kila kitu kilikuwa wazi huku kwenye mitandao ndio usiseme na kila wakati walikuwa wakizunguka pamoja.

Mashabiki wao waliamini muda wa Diamond kuoa na Wema kuolewa na kuanzisha familia ndio ulikuwa umefika, lakini kilichokuja kutokea Mungu ndio ana majibu yake.

Lakini, hakuna couple iliyobamba kama ya Wema Sepetu na Diamond. Uhusiano wao ulipoyumba ghafla tu Penny akaibuka na baadaye Zari akabeba mzigo mazima. Vita haikuwa rahisi hata kidogo na ndio mwanzo wa Team kibao huko kwenye Instagram.

Kwa sasa Diamond na Zari ndio hivyo kila mmoja ameshika hamsini zake, lakini ishu za Wema na Diamond ndio kama mnazozisikia wenyewe.