Mabeki wakali wa kutupia Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Utamu wa michuano ya mwaka huu ni kwamba klabu zimepania kumaliza ubabe wa Real Madrid, ambayo imebeba taji hilo mara tatu mfululizo na kuifanya iwe imebeba taji hilo mara 13.

LIGI ya Mabingwa Ulaya msimu huu wa 2018/19 itaanza mwezi ujao tu hapo. Mechi za awali za mchujo tayari zinaendelea na kesho Jumanne zitapigwa kadhaa ili kupata zile zitakazoingia kwenye makundi.

Mwaka huu, klabu zote za juu kwenye ligi nne bora zitafuzu moja kwa moja kwenye hatua ya makundi.

Utamu wa michuano ya mwaka huu ni kwamba klabu zimepania kumaliza ubabe wa Real Madrid, ambayo imebeba taji hilo mara tatu mfululizo na kuifanya iwe imebeba taji hilo mara 13.

Wakati mashabiki wa soka wakisubiri kwa hamu michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani Ulaya, hii hapa orodha ya mabeki wanaoongoza kwa mabao kwenye michuano hiyo tangu ilipoanzishwa.

5.Sergio Ramos- mabao 11

Beki wa kati na nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos amecheza mechi 114 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mhispaniola huyo siku zote amekuwa akicheza kwa kiwango kikubwa sana inapokuja michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akifunga mabao ya kutosha pia. Rekodi zake zinaonyesha Ramos amefunga mabao 11 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kuwa kwenye orodha ya mabeki waliofunga mabao mengi zaidi katika michuano hiyo.

Akiwa bado mchezaji, Ramos anaweza kuboresha zaidi rekodi yake ya mabao na kufunga mara nyingi zaidi kwenye michuano hiyo ya kibabe Ulaya kwa ngazi ya klabu.

4.Gerard Pique- mabao 12

Barcelona inatarajia itafanya kila inaloweza kuvuka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya misimu kadhaa ya karibuni kukomea kwenye nafasi hiyo. Kwenye msimu uliopita, iliduwazwa kwenye mechi ya marudiano dhidi ya AS Roma licha ya kushinda mechi ya kwanza iliyofanyika Nou Camp kwa mabao 4-1.

Katika mechi hiyo, beki wa kati Gerrard Pique alifunga bao la tatu kwenye mechi hiyo ya nyumbani kumfanya afikishe mabao 12 kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

3.Dani Alves- mabao 12

Paris Saint-Germain ilimsajili Dani Alves mwaka jana akitokea Juventus. Beki huyo wa zamani wa Barcelona na Sevilla ni hatari sana anapopanda mbele kwenda kushambulia.

Ni mzuri kwenye kuzuia, lakini anaifanya timu kuwa na makali zaidi anapopanda mbele kwenye goli la wapinzani. Ndio maana, Mbrazili huyo, ambaye ni beki wa kulia, amefunga mabao 12 katika mechi 152 alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu uliopita, kikosi chake cha PSG kilikomea hatua ya 16 bora kikitupwa nje na Real Madrid.

2.Ivan Helguera- mabao 15

Mabeki wa Real Madrid wanapenda sana kushambulia na hilo ndilo linaloweza kuwa sababu kwanini wamekuwa wengi kwenye orodha hii.

Beki, Ivan Helguera aliichezea Los Blancos kuanzia mwaka 2000 hadi 2007. Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alicheza mechi 97 na kufunga mabao 15. Kutokana na hilo, beki wa kati wa Real Madrid kwa sasa, Sergio Ramos ana kibarua cha kuvunja rekodi za magwiji wawili waliofunga mara nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa mabeki kwenye kikosi hicho cha Bernabeu.

1.Roberto Carlos- mabao 16

Roberto Carlos bado anahesabika kuwa mmoja kati ya mabeki bora kabisa wa kushoto waliowahi kutokea duniani.

Beki huyo wa Kibrazili alifunga mabao 16 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati alipokuwa Real Madrid na msimu wake mmoja Inter Milan. Alikuwapo pia kwenye kikosi cha Brazil kilichobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2002.

Rekodi zake nyingine ameshinda mataji matatu ya Ulaya na La Liga mara nne. Ameichezea Brazil mara 125 na kufunga mabao 11.