Mwendwa: Mitandao ya Kijamii inapotosha soka letu

Tuesday March 13 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa, amewataka wadau wa soka kuacha kueneza siasa za chuki kwenye mitandao ya kijamii na badala yake kuunga mkono juhudi za kuhuisha soka la Kenya.
Tamko la Mwendwa linatokana na hoja ambazo zimekuwa zikiibuliwa na wadau wa soka ambao wamekuwa wakihoji utendaji kazi ya ofisi ya Mwendwa.
Akizungumza katika hafla ya kupanga droo ya michuano ya Chapa Dimba iliyofanyika Jijini Nairobi katika ukumbi Safaricom, Mwendwa alisema licha ya kazi kubwa ya kuendeleza soka inayofanywa na ofisi yake hasa soka la vijana, kumekuwa na kundi la watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuishambulia ofisi ya FKF.
"FKF iliahidi mambo mengi na moja wapo ni kuwawezesha vijana. Tuliahidi kukuza vipaji na kwa kushirikiana na Safaricon kupitia Chapa Dimba kila Mkenya anashuhudia matokeo ya ahadi zetu."
"Tatizo letu ni kukataa kwa makusudi kuona mazuri yanayofanyika. Kenya sasa hivi mitandao ya kijamii inatumika kuwahatibia watu. Kila kukicha nashambuliwa, natukanwa lakini hakuna hata mmoja anayezungumzia mazuri haya"
Mwendwa alisema mafanikio ya Chapa Dimba ni fahari ya kila mkenya mwenye nia nzuri na soka la Kenya na kuongeza kwamba, FKF bado ina mikakati ya kukuza soka la vijana kuanzia miaka 6-20 pamoja na kuendeleza soka la wanawake.
Alisisitiza kuwa kesho ya Kenya kama taifa ipo mikononi mwa vijana na sio wachezaji wenye majina makubwa huku akiongeza kuwa lengo sio kupata matokeo ya muda mfupi bali ni kujenga kikosi imara kitakachovaa viatu vya Victor Wanyama, Michael Olunga na mastaa wengine pindi watakapo tundika daluga.
"Uhai wa soka letu liko mikononi mwa hivi vipaji, tunategemea wachezaji kama John Njuguna kuibeba Kenya kesho sio Wanyama au Olunga, Harambee stars, inaweza isifanye vizuri leo lakini kesho na keshokutwa tutakuwa na hadithi tofauti", alisema.