Kombe la Wanyama laleta neema kwa vijana

Tuesday March 13 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Jumla ya vijana 20 kutoka mikoa nane nchini Kenya wamenufaika na mashindano ya Chapa Dimba maarufu kama kombe la Wanyama.
Vijana hao walipatikana katika mechi takribani 3000 zilizohusisha wachezaji 25,000 wenye umri chini ya miaka 20, kutoka timu 1600, zilizoshiriki michuano hiyo yenye lengo la kuibua vipaji kama sehemu ya mkakati wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF).
Akitaja majina ya vijana hao, katika hafla ya kupanga droo kwa ajili ya fainali ya msimu wa kwanza wa michuano hiyo, Mkurugenzi wa mashindano ya Chapa Dimba, Chris Amimo, alisema vijana sita kati yao wamejiunga na klabu za ligi kuu (KPL) huku wengine wakipata fursa ya kujiunga na kikosi cha taifa cha vijana chini ya miaka 20.
"Tunafuraha kuwa sehemu ya harakati za FKF, shukrani za dhati ziende kwa Victor Wanyama kwa kukubali kuwa balozi wa mashindano. Tangu tumeanza tumecheza zaidi ya mechi 3000, na kushirikisha wachezaji takribani 25,000 kutoka kaunti zote"
Aliwataja vijana waliosajiliwa na vilabu vya kuwa ni Yusuf Mainge kutoka Manyatta aliyejiunga na AFC Leopards, David Majak na Fred Krop (Kapenguria Heroes) waliojiunga na Homeboyz, John Njuguna wa Euronuts na Ahmed Sabri wa Al-Hayat ambao wamesajiliwa na Kariobangi Sharks pamoja na Hassan Iddi wa Bomani Youths aliyetua Bandari.
Aidha, Amino aliwataja wachezaji waliotua kwenye kikosi cha U-20 kuwa ni pamoja na James Omsinde Ashisoma, John Collins Njuguna, Ali Mwakiba na Ezekiel Nyati Mugo.
Wengine ni Yusuf Mainge, Elisha Owino, Jimmy Wafula, Musa masika, Alpha Chris, Patrick Ochieng, Meja Henry, Alvin Mangeni na Mike Odhiambo.
Tayari mikoa saba imeshapata wawakilishi ambao wataungana na wawakilishi wa Jiji la Nairobi ambao watapatikana wikendi hii na kisha wote wataelekea Mjini Kakamega kwa ajili ya fainali ya msimu wa kwanza wa michuano hiyo.
Kutokana na Droo hiyo sasa ni wazi kuwa kutakuwa na mechi nane za kukata na shoka za robo fainali kwa upande wa wanawake na wanaume na mechi zote zitafanyika, Machi 22, katika dimba la Bukhungu na Kakamega High.
Baada ya hapo washindi watakwaana kwenye Nusu fainali itakayotandazwa Machi 24 kabla ya fainali itakayotimua vumbi Machi 25, katika kwenye uwanja wa Bukhungu, mjini Kakamega.

Wanawake:
Waa girls vs Tar Tar Girls (Bukhungu)
Nairobi winner vs Archbishop Njenga (Kakamega High)
Plateau Queens vs Ngakaa Talent Academy (Bukhungu)
Limuru Starlets (ameingia moja kwa moja Nusu fainali)

Wanaume:
Mukumu Boys (Western) vs Simba Hills (Coast)
Al-Hayat (North Eastern) vs Winner Nairobi (Nairobi)
Ombek Red Devils (Nyanza) vs Euro Nuts (Central)
Mwingi Junior Stars (Eastern) vs Kapenguria Heroes (Rift Valley)