Bandari yatikisa kikosi timu za Taifa

Wednesday March 14 2018

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. MASHABIKI wa Bandari FC wameanza kujivunia ukali wa timu yao hasa kutokana na baadhi ya wachezaji wake kutambuliwa na kuchaguliwa kwenye vikosi vya timu za taifa za umri mbalimbali.
Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo ya Bandari FC, Ken Odhiambo ameeleza furaha yake kwa timu yake inacheza soka la hali ya juu na ndio maana wateuzi wa timu za taifa wamewaangazia na kuwatambua wanasoka wake watano walioko katika timu za taifa wakati huu.
Kipa Faruk Shikhalo yuko katika kikosi cha timu kubwa ya Stars, hali mabeki Siraj Mohamed na Nicholas Meja wamechaguliwa kwa kikosi cha Stars U-23. Mshindi wa tuzo la mchezaji bora wa Februari, kiungo Anthony Wambani na straika Keegan Ndemi wako kwa timu ya Stars U-20.
“Ninajivunia sana wachezaji wangu watano wako kwa timu za taifa na sababu hiyo, timu yetu inaonyesha wazi imeimarika na itafanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Kenya msimu huu wa 2018,” akasema Odhiambo.
Alisema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sony Sugar Jumamosi iliyopita, umewapa motisha wachezaji ambao wana hamu ya kucheza mechi yao ifuatayo dhidi ya Vihiga United hapo Jumamosi Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega.