Vita ya tuzo Ligi Kuu yafikia patamu

Monday April 3 2017

TSHABALALA: Beki chipukizi wa Simba, ana umri

TSHABALALA: Beki chipukizi wa Simba, ana umri mdogo, lakini anamudu kupanda na kushuka kusaidia mashambulizi na kurudi fasta kwenye nafasi yake      

By GIFT MACHA

NI kipengele kimoja tu katika tuzo za Ligi Kuu Bara kipo wazi mpaka sasa. Ni kile cha Mfungaji Bora ambaye hupatikana kutokana na wingi wa mabao katika msimu mmoja. Tuzo hii haina longolongo hata kidogo.

Msimu huu Simon Msuva wa Yanga anawakimbiza nyota wenzake wa Ligi Kuu akiwa amefunga mabao 12 mpaka sasa. Anafuatiwa kwa karibu na Shiza Kichuya wa Simba aliyefunga mabao 11.

Ukiachana na eneo hilo la wafungaji, kumekuwa na ushindani mkubwa katika vipengele vingine kama makala hii inavyodadavua.

MCHEZAJI BORA

Kipengele hiki ndicho chenye heshima kubwa miongoni mwa wachezaji. Mpaka sasa ni Msuva, Himid Mao na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wameshaingia katika kipengele hicho. Wengine wasubiri msimu ujao.

Msuva amekuwa katika kiwango bora msimu huu, mbali ya kufunga mabao 12, amehusika pia katika mabao mengine karibu 10 ya Yanga. Ikumbukwe alishinda pia tuzo ya Mchezaji Bora wa Oktoba mwaka jana.

Kwa upande wake, Tshabalala ndiye mchezaji pekee aliyecheza mechi zote za Simba msimu huu. Mchezaji Bora Chipukizi huyo wa msimu uliopita, amecheza kwa kiwango cha juu katika kila mechi. Anaweza kuweka heshima kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora.

Kuhusu Himid Mao hakuna maswali. Amekuwa hodari katika kikosi cha Azam na ni wazi kwamba atakuwa ndiye Mchezaji Bora wa timu hiyo msimu huu. Haitakuwa ajabu akiwa Mchezaji Bora wa VPL.

MCHEZAJI BORA WA KIGENI

Kama isingekuwa matatizo ya nje ya uwanja, straika Mzimbabwe Donald Ngoma ndiye, alistahili kuondoka na tuzo hii. Hata hivyo haiwezekani tena.

Kwa sasa beki wa Simba, Method Mwanjali, pia wa Zimbabwe ndiye ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo. Mwanjali amekuwa katika kiwango bora akicheza mechi 22 mfululizo za Ligi Kuu kabla ya kuumia dhidi ya Prisons. Kinachoweza kumnyima tuzo hiyo ni kama atashindwa kurejea uwanjani.

Anayeweza kumpa Mwanjali ushindani ni beki wa Yanga, Vincent Bossou, ambaye hata hivyo hajacheza mechi nyingi. Kuna wakati alipokwenda na timu ya Taifa ya Togo katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

MCHEZAJI BORA CHIPUKIZI

Tuzo hii msimu uliopita ilikwenda kwa Tshabalala. Msimu huu ipo wazi kwa wachezaji watatu; Shiza Kichuya wa Simba, Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar na Raphael Daud wa Mbeya City. Mwingine anayeinyemelea ni Suleiman Mangoma wa Kagera Sugar.

Kichuya ambaye msimu uliopita aliingia katika tatu bora, sasa yupo katika nafasi nzuri zaidi ya kushinda. Msimu huu amekuwa na kiwango bora zaidi. Ameifungia Simba mabao 11 ya Ligi Kuu na kusaidia katika upatikanaji wa mengine kibao.

Kwa upande wa Daud na Mbaraka wamekuwa sehemu kubwa za mafanikio ya timu zao, haitashangaza kama mmoja wao ataondoka na tuzo hiyo.

KIPA BORA

Msimu uliopita ilikwenda kwa Aishi Manula wa Azam. Msimu huu Manula bado ana nafasi kubwa ya kuitetea, lakini atakabiliwa na ushindani kutoka kwa Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga.

Wote wamecheza mechi nyingi bila kuruhusu bao. Dida amedaka mechi chache zaidi kwani alianza kupata nafasi baada ya Ally Mustapha ‘Barthez’ kuondolewa langoni baada ya mechi ya watani Oktoba mwaka jana.

Tangu hapo Dida amecheza mechi 18 na 11 kati ya hizo hakuruhusu bao. Manula amecheza mechi 22 na 12 kati ya hizo hajaruhusu bao. Kazi kweli kweli.

KOCHA BORA

Mpaka sasa ni makocha wawili tu wanaoingia katika orodha hii. Kwanza ni Mecky Maxime wa Kagera Sugar. Ndiye kocha bora zaidi mzawa kwa sasa. Maxime ameibadili Kagera kutoka kupambana kuepuka kushuka daraja hadi timu inayowania ubingwa.

Mwingine aliye katika nafasi kubwa ni Joseph Omog wa Simba. Mtihani kwa Omog ni kushinda ubingwa wa Ligi Kuu, akifanya hivyo ni dhahiri tuzo itamhusu. Kama kocha huyo raia wa Cameroon atashindwa kutwaa ubingwa, ni wazi tuzo itaenda kwa Maxime.

MWAMUZI BORA

Hapa pana kazi. Msimu uliopita ilikwenda kwa Ngole Mwangole ambaye msimu huu tayari amepata dosari na hawezi kuitetea. Kama mechi zilizobaki zitamalizika salama, waamuzi Jonesia Rukya, Elly Sasii na Israel Nkongo wataingia katika kinya-ng’anyiro hicho. Pia Andrew Akrama anaweza kuteuliwa.