DRAKE: Muziki umempa pesa za kutesa mjini

Muktasari:

Drake baada ya kuonekana mara mbili kwenye shoo za mrembo Jennifer Lopez maarufu kwa jina la J-Lo, kukaibuka stori. Oooh! jamaa sijui nini, sijui kitu gani, lakini mmoja wa marafiki wa Drake akaibuka na kujibu, ni kweli ila haiwahusu, halafu haikuwa siriazi kihivyo.

JENNIFER Lopez. Si unamjua? Basi hiyo ndio stori iliyokuwa ikimhusu rapa, Aubrey Drake Graham aka Drake.

Drake baada ya kuonekana mara mbili kwenye shoo za mrembo Jennifer Lopez maarufu kwa jina la J-Lo, kukaibuka stori. Oooh! jamaa sijui nini, sijui kitu gani, lakini mmoja wa marafiki wa Drake akaibuka na kujibu, ni kweli ila haiwahusu, halafu haikuwa siriazi kihivyo.

Stori ikaishia hapo, lakini watu wakaendelea kuhoji, Drake kwa J-Lo? Mmh! Wamesahau kuwa kijana ana pesa ndefu.

Kwa taarifa yako tu, Drake ameingia kwenye orodha ya marapa wenye pesa ndefu baada ya kuwa na kipato kinachoripotiwa kuwa ni Dola 85 milioni. Kuna baadhi ya mitandao inamtaja Drake kuwa ni pato la Dola 60 milioni. Dola hizo amempiku hata 50 Cent, lakini P Diddy, mpenzi wa zamani wa J-Lo bado anaongoza na utajiri wake wa Dola 750 milioni. Kwenye pesa, mambo mengine yanayotokea, hupaswi kushangaa.

 

PESA ZA DRAKE

Muziki na filamu ndizo fani zinazompatia kipato Drake, ambaye ni mzaliwa wa Toronto, Canada kwa baba Mmarekani Mweusi. Alizaliwa Oktoba 24, 1986.

Majina yake ya utani ni Young Angel na Drizzy Drake. Bado hajaoa na ndio maana anakuwa na uhuru tu wa kutanua na warembo kama J-Lo mara moja moja.

Pesa nyingi za Drake ameziingiza kwa mauzo ya albamu zake na ziara na shoo zake za kimuziki. Lakini, pia rapa huyo ana dili nyingi za kibiashara. Ziara zake za kimuziki zimempa pesa nyingi. Tangu mwaka 2010 alipoanza kuingia rasmi kwenye muziki, Drake anaripotiwa kuingiza Dola 9 milioni kila mwaka kabla ya makato ya kodi. Shughuli zake za kimuziki zimemfanya rapa huyo kuingiza Dola 150 milioni kabla ya makato ya kodi na matumizi mengine.

Si kitu cha mchezo kwa rapa mwenye umri wake kuwa na pesa ndefu kiasi hicho.

Mwaka 2013, Drake aliliambia Jarida la Forbes kwamba anataka kuhakikisha kila mwaka anaongeza pato lake na alikifanya hivyo mwaka 2015, alipoingiza Dola 39.5 milioni.

Dili nyingine za kibiashara zinazomletea pesa ndefu ni pamoja na Wiski ya Virginia Black na Apple Music, huku pia akipiga pesa kwa dili zake huko Toronto Raptors, Nike NKE +2.69% na Sprite.

Shoo zake 54 alizofanya pamoja na Rapa Future zilimwingizia Dola 84.3 milioni kwa kipindi cha miezi mitatu tu na kupiku shoo ile ya Jay-Z na Kanye West ya Watch The Throne iliyofanyika mwaka 2011 na kuwaingizia Dola 75 milioni.

 

MAKAZI BORA NA USAFIRI WA NGUVU

Drake anamiliki jumba moja matata huko Yolo Estate, Hidden Hills lenye thamani ya Dola 7.7 milioni. Ndani ya jumba hilo kuna bwawa na kuogelea, uwanja wa kuchezea tenisi, Jacuzzi, Sauna, Gym, Pool Table, ukumbi wa sinema, chumba cha michezo ya kompyuta, baa, maktaba na sehemu ya kufanyia mazoezi.

Ukiweka kando jumba hilo, pia anamiliki magari ya maana likiwamo Malibu LS, linalotengenezwa na Chevrolet kuuzwa Dola 18.682. Anamiliki Veyron inayotengenezwa na Bugatti na pia ana Bentley aliyonunua kwa Dola 286,695. Gari zake nyingine ni Rolls-Royce (Dola 398,970), Limousine (Dola 269,000) na Bentley - Continental GTC V8 (Dola 193,300).

 

MAISHA YA MAPENZI

Bado hajaoa, lakini katoka na mabinti mbalimbali. Moja ya uhusiano wake uliozua gumzo ni ule wa mwimbaji wa Pop, Rihanna.

Drake ametajwa pia kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwimbaji mwingine wa Pop, Selena Gomez pamoja na mrembo Dollicia Bryan. Hivi karibuni alihusishwa na na J-Lo kabla ya swahiba wake mmoja kudai kwamba uhusiano huo haukuwa siriazi.

Marafiki zake wa karibu zaidi Drake ni Kanye West, Eminem na Jay Z.