Kumbe Ne-yo anatiririka Kiswahili Kibongo-bongo

Muktasari:

Katika mwendelezo huo leo anaweka mambo mengine hadharani, ikiwamo kufichua siri kwamba nyota wa muziki wa kimataifa wa Marekani, Ne-Yo kumbe anajua kuzungumza Kiswahili, ki vipi? Endelea naye...!

JANA katika mfululizo wa makala ya nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platinumz tuliona namna alivyofunguka mambo mengi kuhusu maisha yake na muziki, hususan suala la uhusiano wake na baba yake.

Katika mwendelezo huo leo anaweka mambo mengine hadharani, ikiwamo kufichua siri kwamba nyota wa muziki wa kimataifa wa Marekani, Ne-Yo kumbe anajua kuzungumza Kiswahili, ki vipi? Endelea naye...!

 

Muziki unaelekea wapi?

Diamond anaamini kwa sasa muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa kutokana na fursa nyingi ambazo wasanii nchini wamekuwa wakizipata kwenye medani ya kimataifa.

Anasema fursa hizo ni pamoja na kushiriki matamasha makubwa ya muziki, kushiriki tuzo mbalimbali za muziki kimataifa pamoja na kuimba nyimbo kwa ushirikiano na wanamuziki maarufu duniani.

“Soko kijumla limepanda kwa sasa kwa sababu kama unavyoona tunapata fursa ya kuvuka mipaka hadi nje ya nchi na hata nyimbo zetu zinaingia kwenye chati za muziki za duniani kama vile MTV Europe na kadhalika.

Baada ya miaka mitano, naamini tasnia ya muziki nchini itakuwa imepiga hatua kubwa na kufika mbali zaidi. Cha muhimu ni kuangalia soko linaendaje na kuandaa kazi bora zaidi. Lengo langu ni kutengeneza muziki bora kwa jumla,” anasema Diamond.

Majibu hayo ya Diamond yananipa hamu ya kutaka kufahamu zaidi, jambo la nyuma ya pazia, nataka kujua mbona anatumia muda mwingi kushirikiana na wanamuziki wa nje pamoja na kutofanya shoo za nyumbani mara kwa mara.

“Tumeshapiga sana shoo za ndani ya nchi hapo siku za nyuma. Tunapoamua kushirikiana na wasanii wa nje, tunajaribu kufungua milango kwa muziki wa Tanzania kuvuka mipaka zaidi.

Kwa mfano hivi karibuni nimefanya muziki na Ne-yo. Lengo ni kutengeneza njia ili muziki wetu uingie Marekani. Nawashauri tu wasanii wenzangu wasikate tamaa. Ni kujiamini tu na wasiogope wafanye kama mimi ninavyofanya.”

 

Neyo anatiririka Kiswahili!

Katika maongezi hayo ndipo Diamond anapofichua jinsi Ne-yo alivyoweza kuelewa lugha ya Kiswahili kwa haraka.

Anasema kuwa wakati walipokuwa wanajiandaa kurekodi pamoja wimbo wa ‘I Marry You’, msanii huyo alikuwa mjanja na mtundu mno hasa katika kukamata lugha ya Kiswahili kwa haraka.

“Ninapofanya kolabo na wasanii wa nje, wengi wao hupata tabu kushika maneno ya Kiswahili na wakati mwingine huchukua saa kadhaa kukariri na kuelewa maneno wanayofundishwa, ila Ne-yo alishika kirahisi mno na haraka,” anasema Diamond huku akiongeza kuwa kazi ya wimbo huo ilikuwa nyepesi.

 

Nani anaowakubali?

Licha ya muziki wake kupasua katika anga za kimataifa kwa sasa, mkali huyo anafichua kuwa, wapo wasanii kadhaa ambao anapenda na kuvutiwa nao kimuziki na hupenda kusikiliza na kuzitazama kazi zao.

“Sio siri navutiwa na wasanii wengi ila zaidi ni Navy Kenzo yaani Haika na Nahreel,” anasema Diamond na kuongeza kuwa wasanii hao ni kioo na si ajabu wakapiga kazi katika anga za mbali zaidi.

 

Amkumbuka Saida KaRoli

Asikuambie mtu wimbo wa ‘Salome’ umempatia umaarufu mkubwa Diamond katika siku za karibuni. Mpaka kufikia sasa umetazamwa na watu zaidi ya milioni 14 kwenye mtandao wa You Tube.

Hata hivyo, wimbo huo ni marudio ya wimbo wa nyota wa zamani wa muziki wa asili, Said Karoli uitwao ‘Chambua kama Karanga’, uliotikisa ndani na nje ya nchi kwa maudhui yake na namna ulivyopigwa katika mahadhi ya ngoma za Kihaya.

Diamond aliamua kuurudia wimbo huo mwaka jana akitumia jina la ‘Salome’ akiimba kwa kushirikia na na Rayvan na mkali huyo anakiri kwamba, hakumwacha patupu mwanamama huyo (Saida Karoli). Diamond anasema alimlipa na ameahidi kuendelea kumsaidia kwa kadri ya uwezo wake mwimbaji huyo.

“Nilichukua kazi yake halafu nikamlipa. Vitu vingine ni vya ndani sana haviwezi kutoka. Lakini watu wasubiri kumwona mama huyo kwa mara nyingine, bado yuko vizuri. Sauti yake na utunzi bado ni vizuri.

Wamwombee kwa Mungu kwa sababu najua watu bado wana mapenzi na Saida Karoli. Akitoa kazi yake wampokee kwa sababu yupo mbioni kutengeneza nyimbo nyingine, baada ya ukimya wa muda mrefu,” anafichua Diamond.

 

Vipi kuhusu kuigwa

Katika siku za karibuni, wasani mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu wamekuwa wakijifananisha na Diamond. Mwenyewe analichukuliaje hilo?

“Nishazoea ndiyo ukubwa. Mtu hawezi kuibuka na kusema; Jamaa ni mnene kama sisimizi, atakuambia mnene kama tembo. Siku zote kinacholinganishwa huwa ni kikubwa,” anasema na kujiweka sawa.

“Kwa hiyo linapokuja jambo kama hilo, lazima niwe na hekima na kuchukulia kama kitu cha kawaida kwa sababu kila mtu anatafuta riziki kwa njia anayoiona yeye na chochote kinachotoka atakifananisha na mtu aliyefanikiwa,” anasema.

 

Video inayomvutia

Mpaka sasa, Diamond ametoa video nyingi za nyimbo zake, lakini anakiri kuwa video inayomvutia zaidi ni ile ya wimbo wa ‘Nana’.

“Video zangu zote zinanivutia ila naipenda zaidi ile ya wimbo wa Nana. Video hiyo ilitetemesha sana na ndiyo maana imetazamwa na zaidi ya watu milioni 20. Hata hivyo, video ya Salome nayo inakuja juu inaweza kuangaliwa na idadi kubwa zaidi ya watu,” anasema Diamond.

Mashabiki wa muziki na Watanzania kwa jumla wamekuwa akijiuliza juu utajiri mkubwa alionao Diamond na pengine wanataka kujua kitu gani kinachompa jeuri kuweza kununua na kumiliki magari na nyumba za kifahari?

Nyota huyo alitupiwa swali hilo na kufunguka mengi, je unadhani nini chanzo cha jeuri ya fedha aliyonayo?

Ungana naye Jumatatu upate majibu yake kamili.