Simba yaleta straika mpya

WAKATI asubuhi hii, Yanga watakuwa Bwalo la Polisi, Oysterbay ili kutimiza hamu yao ya kumwona bilionea wao Yusuf Manji anarudi kundini, watani wao Simba wanaendelea kufanya yao wakijiandaa kumleta straika Mcameroon, Christian Joel Ntouba Epoupa.

Unaambiwa, mchana nyavu huyo aliye hatua ya mwisho katika mazungumzo yake na Simba ni mkali kuliko Emmanuel Okwi aliyefunga mabao 23 katika msimu uliomalizia hivi karibuni, yakiwamo 20 ya Ligi Kuu Bara na matatu ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Vigogo wa Simba chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji’ wapo katika mazungumzo ya mwisho ya kuhakikisha straika huyo anatua Msimbazi kuja kusaidiana na John Bocco na Okwi.

Mabosi wa Simba wameshatamba usajili wa hapa ndani ni kama umekamilika na hakuna walichobakiza, ila kwa sasa akili yao imehamia kimataifa na jicho lao likatua kwa Epoupa anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Dynamos ya Zimbabwe.

Mwanaspoti linafahamu licha ya msimu huu, straika huyo kushindwa kuwa katika orodha ya wafungaji bora, lakini Epoupa ni mtamu wa kufumania nyavu na jina lake liliachwa na Kocha Pierre Lechatre akitakiwa asajiliwe katika timu hiyo.

Ingawa Simba inafanya siri kubwa juu ya ujio wa Mcameroon huyo, lakini Mwanapoti linafahamu mazungumzo yao na Epoupa yanaendelea vyema yakifanywa na Try Again anayesimamia shoo nzima za usajili akimaliza mwenyewe kibabe.

Tayari bosi huyo, ameshanasa saini tatu mpaka sasa zote zikiwa za washambuliaji wazawa akianza na Marcel Kaheza akitokea Majimaji, kisha Adam Salamba kutoka Lipuli na Mohammed Rashid aliyekuwa Prisons wote wakiwa vinara wa mabao wa timu zao.

Mpango wa Simba ni kumpata Epoupa anayesifika kwa kufunga kwa vichwa na miguu ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Mrundi Laudit Mavugo ambaye uwezekano wa kuvaa jezi za wekundu hao kwa msimu ujao utakuwa mdogo.

Epoupa tayari ameshakubali kila kitu kutua Simba na sasa anasubiri kumalizana na klabu yake ya Dynamo huku pia akisubiri makubaliano ya mwisho na wakala wake anayezungumza na Try Again.

BADO WAWILI

Inaelezwa baada ya Epoupa kutua Msimbazi, zitabaki nafasi mbili za nyota wa kigeni ili kuhitimisha mipango ya Wekundu hao walioelekea kubadilisha mfumo wake wa uendeshaji kutoka mikononi mwa wanachama hadi mfumo wa hisa.

Mabosi wa Simba wanataka kuongeza mashine nyingine mbili za kigeni maalumu kwa ajili ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara, wakilenga kutetea tena taji hilo walililolitwaa msimu huu kutokana mikononi mwa mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Kwa mujibu wa Try Again, nafasi tatu za nyota wa kigeni wanazotarajiwa kubeba mashine mpya ni kiungo na beki wa kati mbali ya straika, nafasi ambayo Mwanaspoti linafahamu kama mipango itaenda vyema itachukuliwa na Mcameroon Epuopa.