Kesi ya Aveva, Kaburu kusomwa Aprili 5

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kuwasomea maelezo ya Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ Aprili 5, 2018.

Ni baada ya Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga kueleza mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika  na akaomba ipangiwe tarehe kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH).

Hata hivyo, Katuga aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa Aveva hayupo mahakamani hapo kwa kuwa ni mgonjwa amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao,Steven Mwakibolwa aliiambia mahakama kuwa wapo tayari kuendelea na kwamba hali ya Aveva inaimarika ila siyo nzuri sana.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambaye kesi hiyo kwa sasa itasikilizwa mbele yake badala ya Hakimu Victoria Nongwa aliyekuwa akiisikiliza awali, alisema kama hali ya Aveva itakuwa imetengemaa kesi hiyo wataisikiliza mfululizo.

Alisema kesi hiyo ilifunguliwa Juni 26, 2017 na wajitahidi isikilizwe na kumalizika ndani ya miezi 12.

Godfrey Nyange maarufu Kaburu ambaye ni Makamu wa Rais wa Klabu ya Simba yeye alikuwapo mahakamani.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano ya  uhujumu uchumi ikiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha wa Dola za Marekani (USD) 300,000.

Washtakiwa hao wapo mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.