NINACHOKIAMINI: Evra akitaka kupiga mtu aje acheze Simba au Yanga

Tuesday November 14 2017

 

By Frank Sanga

Miongoni mwa mambo yanayokwamisha maendeleo nchini ni jinsi tunavyoshindwa kutofautisha kazi na urafiki.

Ofisi inatakiwa kuheshimiwa kama ofisi, lakini ni mara chache kuliona hilo katika nchi za dunia ya tatu kama Tanzania.

Hivi unadhani viongozi na mashabiki wa Simba wanaamini kama Emmanuel Okwi yupo kazini? Kwamba anahitaji mambo fulani ili afanye kazi yake vizuri? Unadhani wanajua kuwa akikosea anapaswa kufukuzwa?

Usipoangalia vizuri inawezekana kabisa, Okwi licha ya kuwa ameajiriwa na Simba, anaweza kuwa ana sauti kubwa kuliko hao waliomuajiri.

Anaweza akakosea asichukuliwe hatua yoyote, na huyo kiongozi atakayethubutu kumchukulia hatua atashughulikiwa kuanzia na viongozi wenzake mpaka mashabiki wa soka.

Ninajadili hilo huku nikijua kuwa Marseille ya Ufaransa imevunja mkataba na mchezaji wake, Patrice Evra baada ya beki huyo kubainika alimpiga mateke shabiki wa soka mwezi huu.

Klabu hiyo ya Ligue 1, ilitangaza Ijumaa kuwa wameachana na mchezaji huyo mwenye miaka 36 saa chache tangu Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) litangaze kumsimamisha kwa miezi saba.

Sihitaji kurudi kuelezea kwa urefu kilichotokea, lakini kwa kifupi ni kuwa baada ya kuthibitishwa kuwa Evra alimpiga teke shabiki, Uefa imemfungia kwa miezi saba, na baadaye klabu yake ya Marseille ikamtimua.

Turudi nyuma kidogo, wakati Athuman Idd ‘Chuji’ wa Yanga alipoonyesha kidole cha kati kuwatukana mashabiki wa Simba miaka kumi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, alifungiwa na TFF kwa miezi sita kwa kitendo hicho.

Licha ya TFF kumfungia kwa kipindi hicho, Yanga na mashabiki wake waliporomosha lawama kwa shirikisho hilo kuwa linamuonea mchezaji huyo kwa sababu alikuwa hajafanya kosa lolote.

Bahati mbaya zaidi, Chuji alikuwa ndio kwanza amehamia Yanga akitokea Simba, kwa hiyo mambo mengi yalitengenezwa kuonyesha yana uhusiano na uhamisho huo.

Marseille imemfukuza Evra kwa sababu ya kumpiga shabiki wa timu nyingine, Chuji alitetewa na Yanga kwa mbingu na nchi.

Miaka michache baadaye, beki wa kushoto wa Yanga, Stephano Mwasika alimpiga ngumi za uzito wa juu mwamuzi Israel Nkongo katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam.

Lilikuwa ni tukio ambalo lilihusisha wachezaji kadhaa wa Yanga, ingawa sijawahi kuelewa kwanini Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alipewa kadi nyekundu siku hiyo na si Mwasika.

Baadaye Kamati ya Ligi ilikutana na kumfungia Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mechi sita za Ligi Kuu kabla ya kumpiga faini ya Sh500,000.

Mchezaji kiraka wa Yanga, Nurdin Bakari alifungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh 500,000 sawa na ilivyokuwa kwa Omega Seme.

Jerryson Tegete alifungiwa miezi sita na kulipa faini ya Sh. 500,000.

Stephano Mwasika, ambaye alihusika vilivyo katika tukio hilo alifungiwa mwaka mmoja na kupigwa faini ya Sh 1 milioni.

Unadhani Yanga walifanya nini? Waliwatetea na kumgeuzia kibao mwamuzi kuwa aliwatukana wachezaji.

Yanga waliwatetea wachezaji wao usiku na mchana, huku wakijiapiza kwa kulamba mchanga kuwa hawana kosa.

Marseille wametufundisha kitu kikubwa kuwa tunahitaji kuheshimu kazi.

Mchezaji akiwa kwenye klabu ni mfanyakazi kama walivyo wengine. Akifanya vizuri anapongezwa, akikosea anaonywa na kuchukuliwa hatua.

Miezi kadhaa iliyopita, Mwinyi Kazimoto wa Simba alimpiga mwandishi wa kike kwa ngumi na mateke, lakini viongozi wa Simba walikuja juu kusema kiungo wao huyo anaonewa.

Obren Chirwa alitishia kumpiga mwandishi kwenye mazoezi ya timu hiyo, lakini alipata watetezi kana kwamba hastahili hata kuulizwa.

Katika wachezaji hao hakuna hata mmoja anayefikia ubora wa Evra, lakini ameondolewa na klabu hiyo kwa kuitia aibu.

Lakini ninachojua Evra angekuwa anachezea Simba au Yanga, kwa kitendo chake cha kumpiga shabiki angeonekana shujaa.

Angepata watetezi nchi nzima, huyo aliyepigwa angeonekana msaliti na asiyefaa katika jamii.

Hata TFF isingechukua hatua, labda kwa aibu wangemfungia mechi tatu, lakini Simba au Yanga wangemuongeza mshahara ili atulie.