HISIA ZANGU: Cannavaro ameamua njia tofauti na ile ya Kaseja

Tuesday November 14 2017

 MCL

By Edo Kumwembe

RAFIKI yangu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ananiachia maswali mengi. Kwa sasa sio mchezaji muhimu kama ilivyokuwa katika siku za nyuma pale Jangwani. Inatokea. Wakati ni ukuta. Hauwezi kuwa na nguvu zile zile kwa miaka yote.

Ananiachia maswali mengi. Swali la kwanza, najiuliza kama ameamua kustaafu akiwa Yanga. Hapati nafasi ya kudumu katika kikosi cha Yanga lakini angeweza kwenda kwingineko na kucheza soka la kiwango cha juu kwa sababu ana uzoefu.

Kwa kiwango cha Ligi yetu, Cannavaro anaweza kucheza kwingine na kuendelea kuwa mchezaji mzuri.

Labda tatizo anaipenda sana Yanga. Kuna vikosi zaidi ya sita vya Ligi Kuu nchini ambavyo vinaweza kumuhakikishia Cannavaro nafasi ya kudumu.

Kama Juma Kaseja angeamua kustaafu soka miaka minne iliyopita kwa kile kilichodaiwa kuwa amezeeka basi wote leo tungeamini kwamba siku za Kaseja zilimalizika zamani.

Hata hivyo mwenyewe anapambana kupingana na ukweli kwa kuendelea kucheza timu nyingine mbalimbali za Ligi Kuu.

Hata hivyo inawezekana labda Cannavaro ameendelea kubakia Yanga kwa sababu katika miaka ya karibuni kumeendelea kujitokeza pengo kubwa la kimaslahi kati ya timu nne za Ligi Kuu na wengineo hapa nchini.

Yanga, Simba, Azam na sasa Singida United zinaonekana kutengeneza pengo kubwa la kimaslahi dhidi ya timu nyingine nchini. Wakati mwingine ni wazi kwamba ni afadhali ukae benchi Yanga kuliko kwenda kucheza Kagera Sugar kwa sababu za kimaslahi zaidi.

Lakini hapo hapo unajiuliza kwamba John Terry aliondoka Chelsea kwenda kucheza Aston Villa baada ya mkataba wake kumalizika pale Chelsea. Terry amekusanya pesa nyingi katika soka. Kwanini hakuamua kustaafu? Kwa sababu bado ana kiu ya kucheza soka.

Kwa Cannavaro wetu hadithi ni tofauti. Mchezaji wa Tanzania ni vigumu kukusanya pesa nyingi katika maisha yake ya soka na kuamua kustaafu taratibu katika timu ndogo.

Kila siku wachezaji wetu wanahitaji pesa zaidi na zaidi kwa sababu walichokusanya hakijitoshelezi.

Hata kama mchezaji ana kiu ya kuendelea kupata nafasi katika kikosi fulani cha kwanza Ligi Kuu yetu bado ataendelea kuwepo hapo hapo kwa sababu za kimasalahi. Labda hili ndilo linalomtokea Cannavaro kwa sasa.

Kwa vyovyote vile ilivyo, kuna baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga ambao wanafupisha sana maisha yao ya soka kwa kuamini kwamba klabu hizi mbili ni mwisho wa safari. Miaka ya karibuni hata Nsajigwa Shadrack aliamua kustaafia Yanga wakati angeweza kucheza klabu nyingine za Ligi Kuu.

Mussa Hassan Mgosi aliona afadhali kuwa Meneja wa Simba kuliko kwenda kucheza katika klabu nyingine ambayo ingeweza kumpatia nafasi katika kikosi cha kwanza Ligi Kuu. Kuwa Meneja Simba ni nafasi yenye maslahi kuliko kuwa mshambuliaji wa Kagera Sugar.

Tusipopunguza pengo la kimaslahi baina ya timu fulani za Ligi Kuu dhidi ya nyingine basi tutegemee wachezaji wetu wengi kustaafia Simba na Yanga hata kama wana uwezo wa kwenda kujitutumua kwingine. Wakati mwingine maslahi haya sio lazima yawe mshahara binafsi au posho za mchezaji. Wakati mwingine ni malezi ya wachezaji wetu katika timu tofauti.

Kwa mfano, kama Cannavaro akienda Kagera Sugar anajua kwamba hataweza kupanda Ndege kwa msimu mzima.

Akiwa na Yanga anajua kwamba safari za kwenda Kanda ya Ziwa atapanda Ndege. Anajua kwamba safari za mechi za kimataifa atapanda Ndege. Hili ni tatizo jingine la msingi.

Suala jingine ambalo lipo nje ya mada halisi ni namna ambavyo kuondoka taratibu kwa Cannavaro katika soka letu kunavyotumalizia wachezaji mahiri wa Zanzibar katika Ligi Kuu ya Tanzania bara na pia katika timu ya taifa.

Katika miaka ya karibuni, achilia mbali Aggrey Morris, kulikuwa na wachezaji wawili ambao walikuwa wana uhakika wa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars. Hawa walikuwa ni Cannavaro na Abdi Kassim. Kwa sasa wapo wachezaji wa Zanzibar wanaokuja bara kupambana lakini bahati mbaya hawajafikia viwango vya Abdi na Cannavaro.

Kuna nini katika soka la Zanzibar? Tujiulize.