NINACHOKIAMINI: Simba, mechi ya kirafiki katikati ya ligi ni maajabu

Tuesday October 3 2017

 

By Frank Sanga

NIDHAMU ni jambo la msingi sana katika maisha ya binadamu. Katika kila jambo nidhamu ni kitu cha kwanza ili kufikia mafanikio.

Ukiwa mfanyabiashara unatakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa sababu bila hivyo unaweza kujikuta unashindwa kuheshimu muda wa kuwahudumia wateja.

Katika jambo ambalo watu wengi wameshindwa kuheshimu ni kuzingatia muda; uwe wa kukutana na mtu mwingine au hata kufungua na kufunga biashara jioni.

Mwanafunzi mwenye nidhamu atakuwa na ratiba ya shule, ya kujisomea binafsi na kupumzika. Mara nyingi hawa hufaulu na kuendelea na masomo.

Niliandika hapa hivi karibuni kuwa, miongoni mwa sababu kubwa ambazo zinasababisha timu zetu za Ligi Kuu Bara kufanya vibaya ni kukosekana kwa nidhamu kuanzia kwa mashabiki, wachezaji mpaka viongozi.

Kukosekana kwa nidhamu kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara, kumesababisha wengi wao kustaafu soka mapema.

Badala ya kuheshimu kazi yao ya soka, waliendekeza pombe, kukesha kwenye klabu za usiku na starehe za aina tofauti.

Nidhamu imeziangusha klabu nyingi na ndio maana baadhi ya timu zinakuwa na wachezaji wazuri, lakini kwa sababu ya kukosa nidhamu zinajikuta zikiishia kulalamika tu na kukosa ubingwa.

Na ndio maana huwezi kushangaa ukiambiwa kuwa eti Simba baada ya kuifunga Stand United katika mchezo wa kirafiki juzi Jumapili, imepanga kuwa na mchezo wa kirafiki mjini Dodoma.

Simba itacheza na Dodoma FC kesho Jumatano katika Uwanja wa Jamhuri.

Naambiwa pia, Simba ilicheza mechi ya kirafiki na Milambo ya Tabora wakati ikisubiri kucheza na Stand United. Yaani ilitoka Mwanza ilikocheza na Mbao FC hadi Tabora kucheza na Milambo!

Ni jambo la kusikitisha na utovu wa nidhamu. Siamini kama huu ni uamuzi wa kocha, siamini kama ni uamuzi wa benchi la ufundi. Ninaamini huu ni mpango wa viongozi kujipatia fedha za viingilio.

Sababu kubwa ambayo wataisema ni kuwa timu haina fedha kwa hiyo wanatafuta fedha kwa ajili ya kujikimu. Mtu mwenye nidhamu huzingatia maadili kwanza badala ya fedha.

Unaichukuaje timu ambayo ipo katika mashindano makubwa ya ligi, unaipeleka kucheza mechi ya kirafiki ambayo haiwezi kuisaidia Simba kwa lolote.

Mechi za kirafiki hufanyika wakati wa ‘pre season’ au wakati wa maandalizi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya nchi yoyote.

Huwezi kusikia Arsenal au Chelsea na timu nyingine yoyote katika nchi zilizoendelea ikipanga kucheza mechi ya kirafiki na timu nyingine yoyote wakati ligi ikiendelea.

Simba ni timu kubwa, inaheshimika ndani na nje ya Tanzania, ina mashabiki wengi, haiwezi kujidhalilisha na kukubali kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Dodoma FC wakati ligi ikiwa inaendelea.

Ligi inapoanza hata aina ya mazoezi huwa inabadilika kutoka mazoezi magumu mpaka mazoezi ya kawaida tena kwa muda mchache kwa sababu ya kulinda afya za wachezaji.

Lakini kwa Tanzania, naona nidhamu hiyo inataka kupotea na ndio maana unaona timu yenye jina kubwa kama Simba inakubali kudhalilika kwa kutafuta pesa kwa njia ya mechi za kirafiki.

Simba itasingizia kuwa kuna wachezaji hawapati nafasi wangependa kucheza katika mechi za kirafiki. Huko ni kulea wavivu na wazembe makazini.

Kama kuna wachezaji hawapati nafasi katika kikosi cha kwanza, waanze kuangalia jinsi ya kuondoka na si kuwatafutia wavivu kazi ya kufanya.

Ni kweli kuna wengine wanajituma na wanakosa nafasi kwa sababu ya ushindani, lakini tukumbuke kuwa kuna mashindano mengine kama ya Kombe la Shirikisho ambalo kwa timu nyingi hutumia wachezaji wasiopata nafasi kwenye ligi.

Utetezi wowote ambao Simba watautoa kwa kucheza mechi ya kirafiki iwe dhidi ya Dodoma FC au timu nyingine yoyote, siwezi kuukubali. Huo ni udhaifu mkubwa.

Huwezi kuwa na tajiri kama Mohammed Dewji ‘Mo’ anayewapa kila kitu, udhamini wa Sportpesa halafu bado ukaendekeza njaa.

Ningeelewa kidogo kama wangefanya hivyo Njombe Mji kwa sababu naelewa mazingira waliyonayo, lakini sio klabu kubwa kama Simba.