Masogange apumua

Muktasari:

  • Mshtakiwa huyo alipaswa kuanza kujitetea jana Alhamisi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, lakini ilishindikana kwa sababu alikuwa hajaandaliwa

ANGALAU Masogange atapumua ale Krismasi na Mwaka Mpya kwa raha zake. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwambia kuwa, ataanza kujitetea dhidi ya shtaka la kutumia dawa za kulevya linalomkabili Januari 17, 2018.

Mshtakiwa huyo alipaswa kuanza kujitetea jana Alhamisi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, lakini ilishindikana kwa sababu alikuwa hajaandaliwa.

Wakili Nehemia Nkoko alieleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya Masogange kuanza kujitetea, lakini hawakumwandaa. “Tulipanga kumwandaa Masogange Jumamosi, lakini ilishindikana kwa sababu alipata msiba, kwa hiyo tulishindwa kumwandaa na kuomba kesi iahirishwe ili kupata muda wa kutosha,” alisema.

Hakimu alikubaliana na hoja hiyo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2018 atakapoanza kujitetea. Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Hakimu Mashauri kumwona mshtakiwa huyo kuwa ana kesi ya kujibu na anapaswa kujitetea na kuwaita mashahidi wa kumsaidia na anatarajia kuwaita mashahidi watatu.

Katika kesi hiyo, Masogane anatetewa na Mawakili Nehemia Nkoko na Ruben Simwanza.

Kesi hiyo inaendeshwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula ambaye kwa upande wao waliwaita mashahidi watatu wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na kuufunga.

Masogange anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam. Anadaiwa kufanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015. Katika kesi hiyo namba 77 ya mwaka 2017, Masogange anadaiwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine). Pia, anadaiwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam, wakati ni kunyume cha sheria.