Juma Nature analiangalia tu soko la muziki nyuma ya luninga

JUMA Kassim Kiroboto ‘Sir Nature’, kwa wakati wake aliibeba Bongo Fleva kwenye mabega yake. Soko la muziki wa Tanzania likawa ndiyo sebule yake. Kila alipotoa wimbo wanamuziki wenzake waliomba poo kwa jinsi alivyoteka spika za kila redio.

Nature aliwateka ma’DJ wa redio mpaka wale wa kwenye kumbi za starehe. Alikuwa mbabe kwenye nyumba za watu kwa kuwashawishi wapende kusikiliza ngoma zake. Achana na wafalme wa Uswazi wa siku hizi, Nature alikomesha disko vumbi na vigodoro vyote. Mwali anachezwaje bila muziki wa Nature kufunguliwa ili uburudishe?

Unadhani Nature alisimika utawala wake kwenye muziki kwa ngekewa? Jibu ni hapana. Nature a.k.a Kibla ana kipaji kikubwa na nyota kali. Alitoa huduma bora kwa wakati sahihi. Alijua kuwagusa mashabiki wa muziki na wapenda burudani kwa jumla kutokana na tungo zake.

Nature alikuwa na desturi ya kufanya ingizo jipya la maneno ya mtaani hasa ndanindani Uswahilini. Ingizo hilo la maneno lilikwenda pamoja na maneno ya mipasho. Nature ni fundi sana wa kupaka. Ukitaka uthibitisho muulize vetereni wa sanaa za maigizo Bongo, bi mkubwa Sinta.

Sinta na Nature walikwenda sawa kila malavidavi, wakanogesha uhusiano wao kwa kutangaza kuwa wangefunga ndoa. Siku walipokorogana, Sinta aliikoga mipako ya Nature kupitia tungo zake; Sitaki Demu, Sitaki Demu Remix na Inaniuma Sana.

Huyo ndiyo Nature, ambaye Temeke wanamwita Mfalme wa Bongo Fleva. Nature mwenye ujazo mkubwa wa maneno ya shombo. Nature ambaye kama ulikuwa na shughuli yako ya bure halafu wilaya jirani Nature alikuwa na shoo yenye kiingilio, angekudhulumu watu, maana wangesafiri kumfuata tena kwa kiingilio na kukuacha wewe na onyesho lako la bure.

Bado Nature anamiliki rekodi nyingi za huu muziki. Kijana mdogo kutembea akiwa amekaa kwenye ndinga yake, Mercedes Benz macho ya panzi wakati huo. Akawa wa kwanza kumiliki mijengo na magari kadhaa. Zaidi aliwanyanyasa wasanii wenzake walipokutana kwenye shoo, maana aliwafunika.

ILIKUWAJE

WAKATI HUO

Kuhusu Nature kuwa mbabe sana kwenye muziki hilo halibishaniwi. Hata ‘watoto’ wapya wanajua msuli wake. Nature anaweza kuwa mnyonge siku hizi kwenye vituo vya redio na televisheni, hiyo ikiwa ni matokeo ya kazi mpya anazofanya. Hata hivyo, hufundisha adabu sana pindi asimamapo jukwaani na kukamua madude yake ya kale.

Nature ana hazina kubwa ya midude mizito anzia Hip Hop mpaka Kwaito. Huo ndiyo mtaji wa Nature kwenye shoo mpya anazopata. Popote anapopata fursa ya kukamata ‘maikrofoni’ na vijana wapya, akitaka wamwamkie baada ya kushuka jukwaani, basi orodha yake ya nyimbo isheheni yale mapini yake mapya. Lazima atawakalisha.

Kwa nini mtaji wa Nature ni ngoma za zamani? Ilikuwaje Nature alifanikiwa kumiliki njia zote za soko kwa wakati wake? Jibu ni hili; soko la muziki mfano wa luninga, Nature alikuwa akilitazama kwa mbele. Macho yake yalikuwa yanaona vizuri, kwa hiyo alijua wapi apite ili kulipatia inavyotakiwa.

Kama si Nature mwenyewe kuwa mtazamaji mzuri wa soko, basi alikuwa na timu nzuri ambayo ilikuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu wakati na huduma ambayo ilihitajika kutoka kwa mwanamuziki. Bila shaka timu hiyo ikawa inamjenga Nature na kumpitisha kwenye njia sahihi.

Hapa tafsiri ni kuwa muziki unahitaji jicho zuri kulielekea soko. Unaweza kuwa na kipaji kikubwa na ukawa mwenye uwezo mkubwa, lakini ukiwa hufanyi muziki wenye kuendana na soko au ukitoa nyimbo zenye ushawishi mdogo wa kuwafanya watu wahame walipo na kukuelekea wewe, utapata tabu sana.

Hivyo basi, Nature au timu yake ya zamani, walilitazama soko mbele ya televisheni, kwa hiyo huduma ambayo waliitoa ilikidhi mahitaji ya kibiashara kulingana na wakati. Ndiyo maana nilitangulia kusema kuwa Nature alilijua vizuri soko la muziki kama sebule ya nyumbani kwake. Hata taa ikizimika atanyanyuka na kuingia chumbani pasipo kujigonga kwenye meza au ukuta.

ILIVYO SASA HIVI

Nature wa sasa analitazama soko la muziki nyuma ya televisheni, yaani haoni kitu. Anatumia hisia zake kulikabili soko. Hilo ni kosa kubwa. Inaonekana timu yake ya sasa haifanyi utafiti kujua njia ambazo inaweza kumpitisha ili atoe huduma yenye uzani mahsusi.

Na hii siyo kwa Nature tu; miaka ya 1980 alitokea mtawala mkubwa sana wa muziki Marekani. Jina lake ni Stanley Burrell, kwa umaarufu zaidi mwite MC Hammer. Aliibuka na mtindo wake wa kufanya mseto wa Hip Hop na Pop. Hammer akawa bonge la dansa. Basi alinyoosha kweli.

Aliuza nakala nyingi na kufanya shoo zenye malipo makubwa. Hammer aliishi maisha ghali kwa sababu aliingiza fedha nyingi. Soko la muziki alilitazama kwenye televisheni kwa mbele, kwa hiyo alilijulia hasa. Kila alipofyatua albamu ilikuwa sawa na tanzanite kwenye soko la dunia. Iligombewa si polepole.

Ujio wa kizazi cha marapa kama Tupac, Notorious BIG, LL Cool J, Ice Cube, Snoop Dog, Dr Dre, Coolio, Naughty by Nature na wengine mwanzoni mwa miaka ya 1990, ndiyo sababu ya kukatika kwa mrija uliokuwa ukititirisha fedha kwenye akaunti za MC Hammer.

Mara mashabiki wa Hip Hop walianza kumuona MC Hammer ni mzinguaji tu na ile staili yake ya mseto wa Hip Hop na Pop jumlisha uchezaji wake wa mabreka mengi.

Ni wakati ambao watu walitaka kusikiliza mashairi ya harakati na ghani za kigumu kwenye mdundo mzito wa boksi (beat box). MC Hammer akajikuta anaondoka sokoni. Mwanzoni alijitahidi kuuponda muziki wa Hip Hop ya wagumu lakini hakuweza. Kipindi Hammer akijishughulisha kuiponda Hip Hop ngumu, ndiyo hapo alikuwa analitazama soko nyuma ya televisheni. Alikuwa anatumia hisia zake kuliko uhalisia. Angekuwa na vipimo halisi angejua abadilike vipi ili abaki sokoni. Soko litazame mbele, nyuma hutaona kitu.

Kwa miaka kadhaa sasa Nature amekuwa akipuyanga tu sokoni. Akiachia ngoma zinakosa uzito mahsusi. Kama ulivyo mtiririko wake, wiki tatu zilizopita Nature aliachia ngoma mbili mpya zenye majina “Unayumba” na “Nadhani”.

Ni nyimbo ambazo hazina thamani ya soko la muziki kwa wakati huu. Hazibebi hadhi ya Nature kwenye muziki huu kulingana na mahitaji ya wakati uliopo. Zaidi zinamshusha na kumfanya aonekane makali yake ni zilipendwa. Nature hatendei haki jina lake, timu yake ya sasa inaonekana haijui uzito wa jina la Nature. Kuna kitu cha kukumbusha; mwanamuziki akiwa kwenye kilele cha mafanikio yake, anaweza kufanya kazi isiyo na kiwango kisha watu wakaipokea. Mwaka 2003 Nature alitoa wimbo “Inaniuma Sana”, kimuziki haukuwa na sifa za kuitwa bora, ila kwa sababu wimbo ni mali ya Nature ukijumkisha na kisa alichoimba, ngoma ikatamba kweli. Kipindi hiki Nature hayupo kileleni, kwa hiyo anahitaji kutoa ngoma bora ili itambe.