Sapraizi kibao shoo ya Davido

KAMA hukuwa miongoni mwa waliohudhuria shoo kali ya supastaa wa Nigeria, David Adedeji Adeleke a.k.a Davido, basi utakuwa umejipunja sana na kuikatili nafasi yako.

Yaani wajanja wa mjini walikuwa pale Next door, Masaki jijini Dar es Salaam, kusuuza nafsi baada ya kupiga kavu kwa takribani mwezi mmoja bila bata ili kupisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sasa mpango mzima ulikuwa usiku wa kuamkia jana Jumapili, ambapo Davido akipigwa kampani na mastaa kibao wa Bongo Flava, akiwemo Aslay, Nandy a.k.a Sauti Kinanda, Kundi la Mafik na Rubby walikuwa ndani ya jukwaa moja.

Kama unavyojua Wabongo wanapenda sana bata, ndani ya saa tatu tu za usiku ukumbi ulikuwa umeanza kufurika mashabiki huku muziki laini wa kopi ukianza kuburudisha.

Mzuka ulikuwa mkubwa kwelikweli kwani, mwenye mkoa wake, Paul Makonda alikuwa ndani ya nyumba kushuhudia burudani hiyo, akigoma kabisa kusubiri kuhadithiwa. Pia, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza naye hakutaka kumiss kabisa, alitia timu ukumbini mapema tu.

Saa 5:25 mastaa watinga ukumbini

Wakati nyimbo za wasanii wa Bongo Flava na zikiendelea kuburudisha mashabiki waliokuwa wakiingia ukumbini hapo, kama kawaida wale wapenda picha na kuuza sura walikuwa wakipiga stori mbili tatu kwenye redi kapeti. Ndio! Kwani nani hapendi kuuza sura kwenye redi kapeti bana. Mida hiyo pia, wasanii wa Bongo Movie, Bongo Flava nao walikuwa wakizama kwenye ukumbi huku wakitokelezea kinoma noma.

Mwana FA alizama eneo la tukio mishale ya saa 5;20 usiku huku dakika chache baadaye Shilole a.k.a Shishi Baby akiwa na ubavu wake, Uchebe walikuwa wakiingia. Bila kumsahau malkia wa filamu, Irene Uwoya, Miriam Ismail wakifuatiwa na Ruby, Aslay na The Mafiki waliingia ukumbini hapo saa 5:55 usiku. Hata hivyo, Uwoya aliibuka ukumbini hapo bila mumewe, Janjaroo.

Kapo matata mjini hapa kwa sasa, Jux na Vanessa haikuwa nyuma kabisa kwenye shoo hiyo, Gigy Money naye hakubaki nyumbani huku Hamisa Mobetto, aliamua kucheki shoo hiyo akiwa na mama yake.

Hata hivyo, achana na ishu ya mastaa kuingia ukumbini, hivi unajua shoo hiyo ilimuibua mkali wa freestyle, marehemu Albert Mangwea kutokana na nyimbo zake kupigwa kinoma kwenye shoo hiyo ikiwa ni amsha amsha kabla ya wasanii kuanza kupanda jukwaani.

Ngoma za Mikasi na She gotta ziliwapa mashabiki mzuka kwelikweli.

Mbali na ngoma za Mangwea, mkali mwingine wa Bongo Flava, Juma Kassim Kiroboto a.k.a Sir Nature, japo hakuwepo kwenye shoo hiyo lakini ngoma zake zilikinukisha kinoma.

Hakuna Kulala iligongwa ile mbaya na kuzidi kuwapa mashabiki mzuka kabla hata ya shoo yenyewe unaambiwa.

Saa 6 usiku shoo ilianza rasmi kwa Kundi la The Mafiki kupanda na ngoma zao za Passenger na Carola kisha wakafuatiwa na Ruby aliyepiga ngoma za Yule, Are You Ready, Hallo wa Beyonce na kumaliza na Niwaze ambao amewashirikisha The Mafiki, ambapo muda wote mashabiki walikuwa wakipandwa mzuka na mikono ikiwa hewani.

Ishu za Bill Nas tena

Saa 7:20 ilianza kusikika sauti ya Nandy, ambaye alianza kwa kuachia ngoma ya One Day kisha Ninogeshe.

Shughuli ilikuja pale alipompandisha Aslay kuimba naye ngoma ya Sabalkheri, ambao umewapa kiki kinoma kwenye game. Sasa bana, wakati wanaimba si Aslay akachomeka kijembe kwa Nandy akimuuliza anayempenda yeye ama Bill Nas.

Baadaye Aslay alipanda jukwaani na nyimbo za Pusha, Hauna, Nibebe, Nyakunyaku, Natamba na kumalizia na ngoma ya Angekuona.

Pia, Aslay aliibuka na staili mpya ya kutoa lundo la pesa na kuzirusha kwa mashabiki ambao, walikuwa na kazi moja tu ya kuzigombea.

KWA DAVIDO SASA

Baada ya mashabiki kusubiri kwa hamu kubwa, muda ukafika wa Davido kupanda stejini ambapo, saa 9:20 usiku alianza kwa ngoma yake ya Like Dat ’kisha akapiga Fia, ambazo zimeonekana kama ngeni kwa baadhi ya mashabiki.

Hata hivyo, Davido alimiliki vyema jukwaa na wakati akiendelea ghafla tu Diamond Platnumz akafanya saprize moja matata sana kwa kuibuka ukumbini hapo na kupanda stejini.

Iko hivi. Wakati Davido akirusha mashabiki na ngoma yake ya Fia, Diamond ambaye inaelezwa walikuwa na bifu na dogo huyo wa Nigeria, alipanda stejini na wakaimba pamoja wimbo wao wa My Number One Remix.

Diamond aliendelea kutoa burudani na ngoma ya Kwangwaru ambayo amefanya na Hamornize na kuwateka kabisa mashabiki.

Hata hivyo, kabla hajamaliza kuimba wimbo huo, meneja wake Salam alipanda jukwaa kumtoa na kumuacha Davido akiendelea na ishu zake jukwaani.