Danny Mrwanda awaza soka la kimataifa

Wednesday January 10 2018

 

By OLIPA ASSA

Kiungo JKT Mlale, Danny Mrwanda ameelezea namna ambavyo ligi ya madaraja ya chini inavyowapa changamoto nyota waliotoka Ligi Kuu, kwamba endapo wakienda na akili ya ustaa basi mchango wao utakuwa finyu.

Mrwanda ameelezea uzoefu aliouona katika ligi ya madaraja ya chini, kwamba wachezaji ambao wanatoka Ligi Kuu, wanapaswa kuwa kioo kwa wale ambao wanatamani kufikia mafanikio hayo la sivyo watakuwa wamepeleka picha mbaya.

"Nimeichezea Lipuli kabla ya kupanda daraja, ndiyo maana nasisitiza wachezaji ambao wamewahi kucheza Ligi Kuu wakashuka huku chini, watalazimika kuonyesha soka na ufundi wa hali ya juu na sio ustaa.

"Ukiliheshimu soka litakuheshimu, vinginevyo itakuwa ni aibu kwa mchezaji kuonekana huelewi ulichokifuata katika ligi ya madaraja ya kwanza, mpira ni uleule, kuanzia Ligi Kuu mpaka ligi ya madaraja ya chini,"anasema.

Anasema kucheza kwake JKT Mlale, hakuna maana kwamba ndio mwisho wa soka, bali ana mipango ya mbali na ana malengo maalumu. "Naweza kucheza hapa nikaibukia nje ya nchi, mimi nacheza kwa malengo na ndio maana utasikia nipo hapa mara kule," anaeleza.