Eeh! Yaani hadi Wema Sepetu?

WEMA SEPETU

Muktasari:

  • Makonda alimtaja Wema na mastaa wengine wanaotakiwa kujisalimisha Polisi akiwamo TID, Recho, Chid Benz, Babu wa Kitaa, Dogo Hamidu na Mr Blue, huku akila kiapo cha kuwa tayari kupoteza uhai wake

NI ngumu kuamini, lakini ndivyo ilivyo. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana Alhamisi ametaja orodha ya mastaa na watu mbalimbali aliowatuhumu kujihusisha na utumiaji dawa za kulevya akiwamo mwanadada aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu.

Makonda alimtaja Wema na mastaa wengine wanaotakiwa kujisalimisha Polisi akiwamo TID, Recho, Chid Benz, Babu wa Kitaa, Dogo Hamidu na Mr Blue, huku akila kiapo cha kuwa tayari kupoteza uhai wake ili tu kupambana na biashara hiyo. “Sitaki kufika mbinguni nikiwa sina jibu, niko tayari kupoteza uhai ili tu nikifika kwa Mungu niwe na cha kumjibu,’’alisema Makonda jana katika mkutano na waandishi.

Katika orodha yake pia amewataja maofisa polisi wanaodaiwa kukwamisha kesi za ‘unga’, huku akiwataja wengine waliopo ndani kwa sasa akiwamo Petit Man aliyekuwa mtu wa karibu zaidi wa Wema.

Wema ametajwa katika orodha hiyo wakati ikielezwa kuwa yupo katika harakati za kuhamishia maskani yake Kenya na hata jana aliposakwa na gazeti hili hakupatikana, simu yake ilikuwa imefungwa.