MEZA YA UFUNDI: Uwekezaji mkubwa haumaanishi timu haifungiki

Saturday December 9 2017Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By JOSEPH KANAKAMFUMU jkanakamfumu@gmail.com

BILA shaka klabu ya Simba imeandika historia kubwa na ya aina yake baada ya kubadili aina ya uendeshaji wake uliokuwa umezoeleka kwa miaka mingi na kwenda kwenye mfumo mpya.

Simba ilikuwa ikitumia mfumo wa wanachama katika kufanya uamuzi mkubwa wa namna ya kuiendesha timu, kutafuta viongozi na mengine mengi.

Haya yote yalikuwa yakifanywa kwa mujibu wa Katiba ya klabu. Ingawa bado viongozi waliokuwa wakiiongoza klabu hawakuwa wanapata pesa, bado mfumo huo ulionekana kufanya kazi.

Pamoja na kwamba viongozi wengi walifanya kazi hiyo kwa kujitolea, wapo wengine walioingia kuongoza klabu ya Simba ili kujijenga na kufahamika zaidi mbele ya umma wa Watanzania na baada ya hapo tuliwasikia wakijitosa kwenye siasa. Kwa kifupi ni Simba ilikuwa kama daraja la watu kupandia kwenda mafanikio. Ilimaanisha kwa mtu kuwa kiongozi wa Simba tayari alifahamika nchi nzima.

Pia, wapo waliongia kuiongoza klabu hiyo kwa malengo ya kujijengea maisha yao binafsi huku wakifaidika kwa namna moja ama nyingine na klabu hiyo ya pili kwa  ukongwe nchini.

Kwa muda wote huo Simba imekuwa ikihangaika sana katika kutengeneza kikosi bora ndani ya uwanja licha ya kuwa hata nje ya uwanja klabu haikuwa na cha kujivunia zaidi ya majengo yake katika Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Hata hivyo, sasa klabu ya Simba imeandika historia baada ya kuwa klabu ya kwanza iliyokuwa ikijiendesha kwa mfumo wa wanachama kubadilika na kwenda kwenye mfumo wa hisa.

Katika mfumo huo mpya itakuwa chini ya mwekezaji, Mohamed Dewji aliyenunua nusu ya hisa za klabu hiyo huku wanachama wakibakiwa na nusu nyingine. Dewji alitangazwa kuwa mshindi wa zabuni hiyo wikiendi iliyopita.

Baada ya yote hayo, sasa mashabiki wa Simba wameanza kushangilia kwa sauti kubwa huku wakiwatambia wenzao wa upande wa pili kuwa waanze kuyasubiri mabao uwanjani kwa kuwa pesa haitakuwa tatizo tena kwao.

Inawezekana ikawa hivyo, lakini mimi natoa sababu kadhaa zinazoweza kuwanyima Simba matokeo mazuri, endapo maisha yao yataendelea kuwepo kwenye njia hizo.

Simba inaweza kuwa na pesa nzuri na wachezaji wazuri lakini ikakosa mwalimu bora na mzuri. Kuwa na mwalimu bora atakayekuja kufanya kazi bora ndani ya kikosi cha timu kunahitajika bahati kubwa.

Unaweza kumtafuta mwalimu mzuri anayeonekana bora kule alikokuwa akifanya kazi lakini baada ya kufika na kuanza kuifundisha timu mpya, mambo yakawa tofauti kabisa. Hili linatokea duniani kote.

Waangalie Real Madrid walivyokuwa na matumaini baada ya kumnasa Jose Mourinho mwaka 2010/2011 huku akikikuta kikosi cha Madrid kikiwa na wachezaji bora, na yeye akasajili wengine tena wenye ubora wa juu zaidi.

Bado Real Madrid haikuweza kufanya vizuri. Si kwa Madrid tu, zipo timu nyingi ambazo zimewahi kuwaajiri makocha bora lakini hawakuweza kuleta matokeo bora uwanjani.

Simba inaweza pia kuwa na makocha bora kipindi hiki lakini watu wake wa usajili wakashindwa kupata wachezaji bora ambao wanaweza kuibeba na kuisaidia katika mashindano ya ndani na nje.

Pia Simba inaweza kumleta mchezaji kutoka Ghana au Nigeria kwa sifa tu lakini akaja huku na kushindwa kuthibitisha msaada wake kwenye timu. Hii inaweza kumfanya mwekezaji kuanza kuibadili timu kila baada ya miezi sita ili kuwapata wachezaji wenye uwezo ndani ya uwanja.

Ipo sababu nyingine ambayo inaweza kuwanyima raha Wanasimba na kuwafanya wasipate ushindi walioutegemea kila mara ndani ya uwanja kutokana na Kanuni Moja kubwa inayowahusu wachezaji kutoka nje ya nchi. Kanuni yetu ya Ligi Kuu ya Vodacom inazitaka timu zote kusajili wachezaji wa nje wasiozidi saba tu.

Hii ni tofauti na nchi za jirani na nyinginezo za Afrika kama vile Congo DRC, Tunisia na nyingiezo ambazo zinaruhusu kusajili na kuwachezesha wachezaji zaidi ya 10 wanaotoka nje ya nchi zao.

Hii ina maana hata kama Simba itakuwa na uwekezaji  mkubwa wa namna gani, haiwezi kusajili wachezaji wengi kutoka nje. Kikosi chake cha kwanza lazima kiwe na wachezaji wanne ama zaidi kutoka ndani ya nchi.

Namaanisha kuwa bado Simba itaendelea kuhangaika kwa miaka hii ya awali kuifikia TP Mazembe, Al Ahly, Etoile du Sahel na nyinginezo kwa kuwa inabanwa na mazingira halisi ya nchi. Hata hivyo, mfumo huu unaipa nguvu Simba na huenda ikafanya vizuri kimataifa.