Unabisha! Hawa ndio wanasepa

Monday November 5 2018

 

By Thomas Ng'itu

KATIKA mchezo wa soka inakuwa ni baraka kubwa kuona mchezaji akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kuweza kuendeleza kiwango chake na kufungua njia za kucheza soka la kulipwa kwenye ligi kubwa duniani.

Lakini, ndani baadhi ya klabu za Ligi Kuu Bara, tangu kuanza kwa msimu huu kuna wachezaji hawajapata nafasi ya kucheza na kuna kila dalili wakati wa dirisha dogo wakajongea mlango wa kutokea ili kusaka malisho sehemu zingine.

Mwanaspoti limeangalia orodha fupi ya wachezaji waliokuwa wanafanya vizuri lakini hivi sasa hata kuonekana wakicheza ni nadra baada ya kwenda katika klabu ambazo hawapati nafasi.

WAZIR JUNIOR

Straika huyu akiwa na kikosi cha Toto Africa alionyesha umahiri wake katika kufumania nyavu hali ambayo iliwatoa udenda klabu nyingi na kuonyesha kuvutiwa na huduma yake.

Alinukia Yanga na kufanikiwa kufanya naye mazungumzo mpaka kupiga picha na kombe la Ligi Kuu ya klabu hiyo na asubuhi ya kesho yake alisajiliwa na Azam.

Tangu aende Azam msimu uliopita alikumbana na majeraha, hata anapopona bado hajapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza licha ya kwamba anafanya vizuri katika mechi za kirafiki anazopewa nafasi.

Kivyovyote vile Junior atatafuta timu ya kutoka kwenda kucheza kwa mkopo ili aonekane kwasababu mkataba wake na Azam upo ukingoni, hivyo anahitaji miezi sita tu kuonyesha kiwango chake na kupandisha thamani ya mkataba wake.

IDD KIPAGWILE

Ujio wa kocha, Hans Pluijm ni kama umepoteza nafasi za vijana wengi ndani ya klabu hiyo, Kipagwile ni mchezaji aliyetamba na kikosi hicho kwenye msimu uliopita lakini hivi sasa hasikiki kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Akiwa katika kombe la Mapindzui Cup alionyesha kiwango kikubwa mno hali ya kubatizwa jina la ‘Mtoto Idd’ baada ya kuifunga Simba kwani jina hilo liliimbwa na Msanii, Juma Nature kwamba ni mtu anayezua balaa eneo lolote lile.

Kipagwile akiwa kama mchezaji mwingine, lazima atatafuta timu ya kuichezea kwa mkopo katika dirisha dogo ili aweze kuonyesha kile ambacho alikuwa nacho msimu uliopita na kufanikiwa kujizolea umaarufu kwa mashabiki wa soka nchini.

SALIM MBONDE

Alikuwa ni mchezaji ambaye hakosekani katika kikosi cha Mtibwa Sugar kutokana na uwezo wake katika kukaba anapokuwa kwenye safu yake ya ulinzi.

Uwezo wake ukawashawishi mabosi wa Simba wamsajili na kweli walifanya hivyo na kufanikiwa kumpeleka katika kikosi chao, lakini tangu amefika ndani ya kikosi hicho amekutana na mkasa wa majeraha mfululizo.

Leo hii Mbonde jina lake limepotea katika masikio ya mashabiki wa soka nchini, hata akiwa fiti ni ngumu mno kuona kama anaweza kufiti katika mfumo wa Mbeligiji, Patrick Aussems kwani hata, Yusuph Mlipili aliyekuwa anacheza msimu uliopita amejikuta akipoteza namba mbele ya Juuko Murshid na Pascal Wawa.

Mbonde ana kila sababu ya kurejea katika kikosi chake cha Mtibwa Sugar kutokana na kwamba aliondoka vizuri lakini pia kikosi hicho kina kawaida ya kuwapokea wachezaji wake wanaoondoka na kukutana na changamoto.

SAID MOHAMMED ‘NDUDA’

Jina lake maarufu zaidi ni Nduda katika masikio ya wapenzi wa soka, alisajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar na hiyo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika kikosi hicho cha sukari.

Tangu amejiunga na Simba ameshindwa kuonyesha makali yake hali ambayo uongozi wa Simba walibidi kumuongeza, Deogratius Munish katika kikosi hicho.

Ujio wa Dida ndio ulizidi kumpoteza kabisa Nduda kwasababu hata katika benchi haonekani, taswira zinaonyesha kabisa kwamba mchezaji huyu dirisha dogo kuna kila dalili za kuchomoka.

EMMANUEL MARTIN

Winga mmoja matata sana ndani ya kikosi cha Yanga, alikuwa anapata nafasi msimu uliopita lakini msimu huu amejikuta akikalia kuti kavu mbele ya kocha, Mwinyi Zahera.

Martin ni mchezaji mwenye spidi ya juu na uwezo wa kumiliki mpira, hiko ndicho kilichowafanya Yanga wamtoe Visiwani Zanzibar na kumsajili katika klabu yao.

Winga huyu kuna asilimia chache sana za kuendelea kubaki katika kikosi hiko kwasababu mkataba wake unatajwa unaelekea ukingoni hivyo anahitaji kuonyesha kiwango sehemu nyingine ili mkataba wake ukiisha dau lake liweze kuwa zuri.

MARCEL KAHEZA

Msimu uliopita alikuwa mfalme ndani ya kikosi cha Majimaji na hii imetokana na namna ambavyo alikuwa akiisaidia timu hiyo katika kupata matokeo.

Marcel hata timu yake ikipoteza alikuwa na uwezo wa kutafuta namna yoyote ya yeye kuweka mpira wavuni na alikuwa akifanikiwa katika hilo mpaka kutoa udenda klabu nyingi nchini.

Alihusishwa Singida, Azam, Yanga lakini mwisho wa siku aliamua kutua zake Simba, sio kama uwezo hakuna lakini kilichotokea kakutana na watu ambao tayari ni wafalme na wamemfanya asionekane wala kupata nafasi ndani ya kikosi hiko.

MOHAMMED RASHID

Aliibeba Prison mabegani kutokana na magoli yake ambayo alikuwa akiyafunga hivyo Simba na Yanga wakavutiwa na huduma yake na Simba walifanikiwa kumsajili.

Tangu ametua katika kikosi hicho amejikuta akikalia kuti kavu, taarifa zingine zinasema kwamba jina lake tayari limetolewa kwa wachezaji watakaocheza Mashindano ya CAF, inaonyesha dhahiri maisha yake ndani ya Simba sio marefu.

Hata hivyo ametajwa kwenda kwa mkopo katika kikosi cha KMC wakati huo huo Prison nayo imeonyesha ipo tayari kumpokea.