Muda wa simba kumsahau boli zozo ndio huu!

Kuna kumbukumbu moja ilianzia mwaka 1993, inaliumiza sana soka la Tanzania miaka na miaka, hasa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi, Simba.

Simba ilipokonywa tonge mdomoni kwenye ardhi ya nyumbani na Stella Abidjan ya Ivory, baada ya kuchapwa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya Fainali ya Kombe la CAF mwaka huo.

Kinachoumiza na kushangaza zaidi ni Simba ilipoteza mchezo huo wa pili ambao ilicheza nyumbani, ikiwa imetoka kufanya kazi nzuri ugenini huko Ivory Coast baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza wa fainali.

Mshambuliaji wa Stella Abidjan, Boli Zozo ndiye alizima ndoto za Simba na Watanzania kwa jumla za kutamani kuona timu ya hapa inatwaa ubingwa wa mashindano makubwa ya soka barani Afrika.

Tangu hapo Boli Zozo ni kama aliacha nuksi kwa timu za Tanzania kuanzia zile za klabu hadi za Taifa.

Mara kadhaa zimekuwa zikijikuta katika mkosi kama wa Simba ule wa kumla ng’ombe halafu zikashindwa kuumaliza mkia hata pale zinapoonekana zipo kwenye nafasi nzuri ya kutamba.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika harakati za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2018 ilijikuta ikikutana na mzimu wa Boli Zozo ambao Simba waliupata mwaka 1993.

Ikiwa na nafasi nzuri ya kufuzu AFCON kama timu iliyoshika nafasi ya pili ikiwa na matokeo bora kama ingeifunga Msumbiji kwenye mechi ya mwisho uwanja wa nyumbani wa Taifa jijini, Stars ilijikuta ikizamishwa na kukosa nafasi hiyo baada ya kuchapwa bao 1-0 na kushindwa kufikia pointi 11 ambazo zingeifanya iwe sawa na Senegal iliyoongoza kundi. Mkosi huo wa Boli Zozo mwaka huo haukuwatesa Stars tu kwani hata Simba uliwarudia katika mashindano ya klabu Afrika mbele ya Textil do Pungue ya Msumbiji pia.

Ikiwa na nafasi kubwa ya kufuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya timu hiyo, Simba ilijikuta ikilala nyumbani kwa mabao 4-2 na kutupwa nje ya mashindano hayo.

Mwaka mmoja baadaye Yanga nao walikumbana na nuksi hiyo ya mwaka 1993 ambayo watani wao wa jadi Simba waliipata baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mechi ya pili nyumbani licha ya kupata matokeo mazuri ugenini.

Baada ya kwenda Libya na kulazimisha sare ya bao 1-1, Yanga ilikuwa na nafasi kubwa ya kufuzu raundi inayofuata ya Kombe la Shirikisho kwani ilihitajika kuibuka na ushindi wa aina yoyote nyumbani au kutoka sare ya bila kufungana na Walibya hao.

Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kwenye mechi ya marudiano hapa nchini ambapo Yanga ilijikuta ikipoteza nechi ya marudiano iliyochezwa uwanja wa Taifa kwa bao 1-0 na kuaga mashindano hayo.

Kuna idadi kubwa ya mifano ambayo unaweza kuitoa kuonyesha ni kwa namna gani timu za Tanzania zimekuwa zikishindwa kutumia vyema fursa muhimu za kusonga mbele kwa kupoteza mechi zinazoonekana zina nafasi kubwa ya kupata matokeo hasa zile inazocheza hapa nyumbani.

Safari hii Simba ipo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Al Ahly Jumanne iliyopita.

Hesabu zinaonyesha kuwa kama Simba ikiwa itaibuka na ushindi wa mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya AS Vita na kisha Al Ahly ikaifunga JS Saoura huko Misri, Simba itakuwa imejihakikishia kufuzu robo fainali.

Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo katika mechi nne ilizocheza, imeibuka na ushindi kwenye michezo hiyo yote huku ikiwa imefunga mabao 14.

Kitendo cha kuibuka na ushindi dhidi ya Ahly kwa kiasi kikubwa kimeamsha molali ndani ya Simba na kila mmoja anaamini AS Vita atafungwa mechi ya mwisho akija hapa nyumbani na Simba itafuzu hata kama atapoteza mechi yake dhidi ya Saoura inayofuata.

Hata hivyo, wakati imani ya Watanzania na mashabiki wake imekuwa kubwa kwamba itafuzu robo fainali, Simba itambue dhamana kubwa iliyopo mbele yake kwenye mechi zilizobakia.

Rekodi ya kupata ushindi nyumbani ni wazi kwamba itazifanya timu kujiandaa vilivyo kuikabili Simba zikiamini kuwa sio mpinzani mwepesi jambo litakalozidi kuzipa ugumu mechi ilizobakiza.

Wachezaji na benchi la ufundi la Simba wanatakiwa kufanya maandalizi makubwa ya kimbinu na kiufundi ili waweze kukabiliana vyema na wapinzani wao na kupata ushindi ambao utawavusha.

Kuwa kwenye nafasi nzuri ni jambo moja na kufuzu kwenda hatua nyingine ni jambo lingine hivyo pasipo maandalizi, ndoto yao inaweza kutotimia.

Wazitazame mechi zilizosalia kama za kuanza moja na ikiwa wataingia kwa mawazo kwamba wapo kwenye nafasi nzuri, watajikuta wakirudi kwenye historia ya Boli Zozo.

Kilichotokea mwaka 1993 kilikuwa ni zao la kuuanza kutoa jina kabla mtoto hajazaliwa. Wasipokuwa makini, kilio cha Boli Zozo na Tico Tico watakutana nacho tena.