NIPE NIKUPE: Mo Salah, Dybala kuhusishwa kwenye dili la kubadilishana wachezaji

Monday February 18 2019

 

TURIN, ITALIA, JUVENTUS ipo siriazi kwenye mpango wake wa kumsajili supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah. Thamani ya Mo Salah inatajwa kuwa ni Euro 200 milioni, lakini Juventus inamtaka kumtumia Paulo Dybala kwenye dili hilo ili kumpata Mo Salah, ambaye inataka aende akaungane na Cristiano Ronaldo kwenye chama lao.

Juventus inataka kuipa Liverpool, mchezaji Dybala pamoja na pesa, Euro 50 milioni ili kumsajili supastaa huyo wa kimataifa wa Misri, ambaye anasakwa pia na Real Madrid kutokana na huduma yake bora kabisa anayotoa uwanjani.

Hata hivyo, kama dili hilo litatiki, Dybala na Mo Salah hawatakuwa wa kwanza kuhusika kwenye dili za kubadilishana wachezaji pamoja na pesa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka ya karibuni.

Andy Cole kwa Keith Gillespie

Hili ni dili lililofanyika baina ya Manchester United na Newcastle United. Man United ilimtaka Andy Cole wa Newcastle na hivyo ikaamua kumweka Gillespie na Pauni 6 milioni juu kumnasa mtu wake. Hiyo ilikuwa kwenye msimu wa 1994/95 na Kocha Sir Alex Ferguson alionekana kama amechanganyikiwa vile wakati alipokuwa akifanya mabadiliko hayo, lakini mwisho wa jambo hilo Andy Cole amekwenda kuwa staa mkubwa sana Old Trafford na kuisaidia timu hiyo kubeba mataji kibao. Gillespie maisha yake huko Newcastle hayakuwa matamu kama alivyokuwa Man United, hivyo mwaka 1998 akaondoka.

Zlatan Ibrahimovic kwa Samuel Eto’o

Barcelona na Inter Milan waliketi mezani kufanya dili la kubadilishana wachezaji Ibrahimovic na Eto’o. Barca ilimtaka Ibra kutoka Inter na hivyo ikaweka mezani ofa ya mchezaji Eto’o pamoja na Paunni 35 milioni juu.

Kipindi hicho, Inter ilikuwa chini ya Jose Mourinho na Barca ilikuwa ikinolewa na Pep Guardiola. Hakika dili hili lilikuwa bora kabisa kwa Inter, kwa sababu ilimpata Eto’o na Pauni 35 milioni juu, ambapo straika huyo wa kimataifa wa Cameroon alikwenda kuipa mataji matatu makubwa kwa msimu mmoja Inter, wakati Ibrahimovic huko Nou Camp maisha yalikuwa magumu kwelikweli na kutibuana na Kocha Guardiola.

Roberto Carlos kwa

Ivan Zamorano

Fowadi wa Chile, Ivan Zamorano alikuwa mmoja kati ya mastraika hatari kabisa huko Ulaya mwaka 1995 ambapo alifunga mabao 28 katika mechi 38 kuisaidia Real Madrid kubeba ubingwa wa La Liga. Lakini kuibuka kwa Raul kulitibua mambo na Inter Milan chini ya Roy Hodgson ikamtaka Zamarano na kufanya hivyo, ikaamua kuipa Los Blancos ofa ya kuipa beki wa kushoto, Roberto Carlos pamoja na Pauni 1 milioni. Real Madrid ilikubali, ikamchukua Roberto Carlos na Pauni 1 milioni kisha ikamwaachia Zamorano kwenda Inter. Dili hilo lilikwenda kuwa na manufaa kwa Madrid kwa sababu ilipata huduma bora kutoka kwa Carlos, wakati Inter inachokumbuka kuhusu Zamarano ni jezi yake tu kuandikwa namba 1 jumlisha 8 ili tu jumla yake iwe namba 9.

Ricardo Quaresma kwa Deco

Kiungo fundi wa mpira, Deco alikuwa kwenye kiwango bora kabisa na ilipofika mwaka 2004, akitoka kuipa ubingwa wa Ulaya, FC Porto, Barcelona ikavutiwa na huduma yake na kumtaka akajiunge na kikosi chake.

Hapo Barca ikaona ni vyema kufanya biashara na Porto na ofa yake ilikuwa kumtoa mchezaji Ricardo Quaresma pamoja na Pauni 13.2 milioni nayo ikamchukua Deco akakikipige Nou Camp. Quaresma alikuwa Barcelona kwa mwaka mmoja tu, akatibuana na Kocha Frank Rijkaard na hivyo kuhusishwa kwenye dili hilo la kumleta Deco Nou Camp. Mwisho wa biashara hiyo, Barca ilipiga bao kwa sababu Deco alikuja kuipa mataji mawili ya La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mengine, huku Qauresma akiende kuchemsha tu FC Porto.

Nemanja Matic kwa

David Luiz

Chelsea sera yake ya kusajili kila kinda mwenye kipaji ilisababisha kufanya kutokea kwenye dili hili la kubadilishana wachezaji. Mwaka 2011 iliamua kumtumia kiungo wake Nemanja Matic pamoja na Pauni 20 milioni juu kuishawishi Benfica ili imchukue beki wa kati Mbrazili, David Luiz. Lilikuwa dili la ajabu hakika, kwani miaka michache baadaye, Chelsea ilienda kumsajili tena Matic na kumleta Stamford Bridge kuja kucheza timu moja na Luiz. Baada ya muda, Chelsea ilimuuza Luiz kwenda PSG na baadaye ikamnunua tena kumrudisha kwenye kikosi chake. Matic kwa sasa anakamatia kwenye kiungo ya Manchester United, wakati Luiz akiendelea kubaki Chelsea na mkataba wake unakwenda kufika tamati mwishoni mwa msimu huu.

Francesco Coco kwa Clarence Seedorf

Mahasimu wawili huko kwenye Serie A, AC Milan na Inter Milan waliwahi kufanya biashara ya kubadilishana wachezaji wakati walipofanya hivyo kwa Francesco Coco na Clarence Seedorf. Mwaka 2002, Inter ilikubali kumwaachia Seedorf aende kujiunga na AC Milan kisha ikamchukua beki Coco, ambaye kipindi hicho alikuwa akidaiwa kuwa ni Paolo Maldini mpya, lakini matokeo yake beki huyo alistaafu soka akiwa na miaka 30 tu na kwenda kuendelea na mambo yake huko huko Hollywood. Seedorf alikwenda kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Serie A mara mbili akiwa na Milan. Coco amekuwa akivumishwa kwa sasa amekuwa dalali wa nyumba.

Ashley Cole kwa William Gallas

Wachezaji hao wawili hakuna hata mmoja aliyehama timu yake katika hali nzuri. Cole aliwatibua mashabiki wa Arsenal hali ilikuwa hivyo kwa Gallas. Dili hilo lilizihusisha klabu za Arsenal na Chelsea. Chelsea ikiwa chini ya Kocha Jose Mourinho ilionekana kuvutiwa na huduma ya Cole huko Arsenal na hivyo kufanya mchakato wa kumnasa na kuona hivyo iliona ni vyema kumpelekea Arsene Wenger ofa ya beki wa kati, Gallas pamoja na Pauni 5 milioni ili kumchukua beki huyo wa kushoto, Cole. Dili likafanyika, lakini mwisho wa siku, Chelsea ndio iliopiga bao kwa kupata huduma ya Cole, ambaye alikwenda kuwapa taji la Ligi Kuu England, Kombe la FA mara nne na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Gallas alikwenda kuwa shida tu huko Arsenal na mara kadhaa alitibuana na wachezaji wenzake kabla ya kuwakomoa kabisa kwa kuhamia Tottenham Hotspur.

Jermain Defoe kwa Bobby Zamora

Mara chache kuona dili la kubadilishana wachezaji na kila timu ikawa na faida bora kabisa kwa mchezaji iliyemchukua. Tottenham Hotspur na West Ham United zilifanya dili la kubadilishana wachezaji Jermain Defoe na Bobby Zamora. Defoe alikuwa kwenye kikosi cha West Ham United na hakika huduma yake ilisakwa na karibu kila timu. Tottenham ilikwenda na ofa yake ya kuipa West Ham United mshambuliaji Bobby Zamora pamoja na Pauni 7 milioni ili kumchukua Defoe.

Maisha yalikuwa magumu kwa Defoe huko Spurs, lakini mambo hayakuwa poa kwa Zamora huko kwenye West Ham United, lakini alifunga bao kwenye siku ya mwisho ya msimu kuirudisha kwenye kwenye Ligi Kuu England.

Alexis Sanchez kwa Henrikh Mkhitaryan

Hadi sasa ngoma droo, si Manchester United wala Arsenal iliyonufaika sana kwenye dili la kubadilisha wachezaji wakati zilipofanya hivyo Januari mwaka jana zilipobadilishana wachezaji Alexis Sanchez na Henrikh Mkhitaryan.

Man United ilikuwa ikiitaka huduma ya Sanchez na kuona hivyo, Kocha Jose Mourinho aliyekuwa Old Trafford kwa kipindi hicho akamfuata Arsene Wenger, aliyekuwa na Arsenal na kumpa ofa ya kubadilishana staa huyo wa Chile na mchezaji Mkhitaryan. Dili likafanyika na kila mmoja alikwenda alikokwenda, Sanchez ambapo huko Old Trafford bado anapambana na hali yake, sawa na ilivyo huko Emirates ambapo Mkhitaryan bado hajatuliza daluga zake ndani ya uwanja huku akisumbuliwa sana na majeruhi.