Yanga yapelekwa Arusha, Azam Mwanza nusu fainali Shirikisho

Muktasari:

  • Mchezo wa nusu fainali ya kwanza itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Mei 18, 2024 kati ya Coastal Union na Azam, mchezo utakaoanza saa 9:30 alasiri.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa ratiba ya mechi za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo Yanga imepelekwa jijini Arusha wakati Azam ikitupwa jijini Mwanza.

Mchezo wa nusu fainali ya kwanza itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Mei 18, 2024 kati ya Coastal Union na Azam, mchezo utakaoanza saa 9:30 alasiri.

Coastal Union ikiwa hatua ya robo fainali ilikata tiketi yake kwa kuichapa Geita Gold kwa bao 1-0 huku Azam ikishinda kwa kishindo mchezo wake wa robo fainali kwa kuichapa Namungo kwa mabao 4-1.

Nusu fainali ya pili itapigwa Mei 19 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha muda huo huo kati ya Ihefu na Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa taji hilo.

Ihefu ilikata tiketi hiyo baada ya kuiondoa Mashujaa hatua ya robo fainali kwa penalti 4-3 wakati Yanga iliindoa Tabora United kwa mabao 3-0.

Tayari TFF imeshatoa ratiba ya mchezo wa fainali ambao utapigwa Juni 2, 2024 kwenye Uwanja wa Tanzanite mkoani Manyara ambapo mechi hizo mbili zitaamua nani atatinga hatua inayofuata.

Yanga na Coastal Union ambazo zilicheza fainali ya msimu uliopita zimo hatua ya nusu fainali ya msimu huu zikisaka rekodi ya kurudi fainali ya pili kwa Coastal Union wakati Yanga inasaka fainali yake ya nne mfululizo ikiwa pia inaongoza kwa kulichukua taji hilo mara nyingi zaidi (saba).