Mawinga hawa weka mbali na watoto

Sunday April 15 2018

 

By THOMAS NG’ITU

KULIKUWA na mawinga wengi wengi kama Beya Simba wa Pamba akaondoka, Sunday Juma (Simba) akaondoka yaani wengi tu Edibily Lunyamila akaondoka.

Akaja Tom Kipese, Dua Said wakaondoka, kwa sasa wapo lakini tunamwona naye Mrisho Ngassa naye anakaribia kuondoka. Akaja pia Saimon Msuva ambaye sasa anajiachia pale Morocco.

Hao ni baadhi tu ya mawinga hatari zaidi kuwahi kutokea nchini. Lunyamila alikuwa na kasi, uwezo wa kupiga chenga na kufunga. Aliibeba Yanga yote mwenyewe kwa nyakati fulani.

Alitisha Afrika Mashariki na hata Uganda daladala ziliandikwa Lunyamila kwa kufanya mambo mwaka 1999 wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Ngassa akiwa kwenye ubora wake naye alitisha Afrika Mashariki yote. Alikuwa na kasi ya ajabu. Angeweza kuwapunguza wachezaji wawili ama watatu na kufunga. Haishangazi kuona Yanga, Azam na Simba zilikuwa zikimgombea.

Ni kama ambavyo alikuwa Msuva. Kasi yake ilikuwa siyo ya nchi hii. Angeweza kufanya anachojisikia.

Haishangazi kuona amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu mara mbili.

Baada ya mastaa hao, umewaza kujiuliza ni mawinga gani wenye uwezo wa juu zaidi kwa sasa ndani ya Ligi Kuu. Ni Geofrey Mwashiuya? Yusuf Mhilu? Ama nani?

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mawinga wenye spidi msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

EMMANUEL MARTIN (YANGA)

Tangu amesajiliwa na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar, amekuwa na kiwango kizuri ndani ya kikosi cha Jangwani.

Makosa madogo madogo ndio yalikuwa yakimgharimu na kujikuta akisugua benchi lakini sasa yuko vizuri.

Martin ni miongoni mwa mawinga wenye spidi ndani ya Ligi Kuu. Mara zote amekuwa akinufaika na kasi yake.

Yupo vizuri pia katika umiliki wa mpira ndani ya kikosi hicho.

Uchezaji wake wa spidi na upiganaji, umemfanya kuingia ndani ya orodha hii ya mawinga ambao wanaspidi wanapokuwa uwanjani.

PETER MAPUNDA (MAJIMAJI)

Achana na ufupi wake. Peter Mapunda ni kati ya wachezaji ambao wanakimbia vilivyo ndani ya kikosi cha Majimaji FC ya mjini Songea.

Mapunda anatumika kama mchezaji wa kupeleka mashambulizi, chenga zake za dharau na kuwaboa mabeki wa timu pinzani, zimezidi kumuweka katika kikosi cha kwanza.

Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City ana spidi kubwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.

NICHOLAS GYAN (SIMBA)

Wakati anajiunga na klabu ya Simba, kwenye mchezo wa Simba Day alionyesha kiwango kikubwa na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo washindwe kuficha hisia zao juu yake.

Lakini baadae alianza kupotea kutokana na kupata muda mchache wa kucheza, mpaka pale kocha msaidizi Masoud Djuma, alipoamua kumbadilisha na kucheza kama beki wa kulia wa kutegemewa.

Spidi ambayo anayoionyesha hivi sasa ni kubwa. Mara kwa mara magoli mengi huwa yanaanzia katika upande wake wa kulia.

Mfumo wa 3-5-2 umemfanya acheze kama winga baada ya kocha wa timu hiyo kuwafanya mabeki wa pembeni kutumika kama mawinga kama ilivyo kwa beki wa kushoto Asante Kwasi.

IDD KIPAGWILE (AZAM)

Wenyewe walianza kumuita motto Iddi. Ni kama kumtia nakshi tu wakitumia jina la wimbo wa Sir Nature ‘Mtoto Iddi’ ambaye anaimbwa kama amezua balaa. Kipagwile alizua balaa baada ya goli lake kuitoa Simba katika kombe la Mapinduzi.

Winga huyu anaingia katika orodha hii kutokana na spidi yake uwanjani. Katika kikosi cha Azam huwa anatumika kama mtu wa kuokoa jahazi pale mambo yanapokuwa magumu.

Kipagwile katika michezo ambayo huwa anaingia, mara kwa mara huwa analeta madhara.

Huwa analazimisha kuingia ndani 18 kwa spidi lakini pia chenga zake za maudhi (kufinya), muda mwingine huzaa penalti kutokana na mabeki kushindwa kuendana na kasi yake.

SHIZA KICHUYA (SIMBA)

Tangu asajiliwe na Simba akitokea Mtibwa Sugar, amekuwa na misimu mizuri ndani ya kikosi cha Simba.

Kichuya amekuwa na msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Simba kutokana na spidi yake.

Kasi yake ni ile ile kila siku. Pia uwezo wake wa kukimbia kwa spidi na kupiga mashuti umekuwa na msaada mkubwa.

Licha ya kwamba hivi sasa anaongoza Okwi kwa mabao, lakini Kichuya huwa anahusika katika magoli ambayo yanapatikana katika klabu hiyo.