MWALIMU KASHASHA: Mlima mrefu UNATAKA gia kubwa-1

Friday January 12 2018

 

By MWALIMU KASHASHA

NI siku ya 12 ya Januari tukikuwa tayari tumeanza safari yetu ya kilomita nyingi ambazo zitatulazimisha kupita katika vituo vingi. Mazingira tofauti na hali ya hewa isiyofanana mpaka kufikia tamati ya mwaka. Ndio maisha yalivyo hivyo.

Sote tunafahamu barabara yetu siyo ya tambarare, ina kona nyingi na milima mingi tena mirefu na miteremko kidogo sana. Hivyo, tunatakiwa tujiandae vizuri ili kumudu kila aina ya changamoto na hatimaye tuweze kupata mafanikio yenye tija tutakapofika mwisho wa safari yetu ya siku 366 za mwaka huu.

Wakati unakwenda mbio, mipango iliyowekwa katika soka inaweza ikawa ni mingi katika ngazi zote na yote inalenga kubadilisha sura ya mafanikio tuliyoyapata mwaka jana ambayo hayakuwa ya kujivunia kwa sababu hayakutuachia kumbukumbu yoyote kubwa.

Vyombo vya habari, vyama vya michezo, wachambuzi wa michezo, wadau mbalimbali, mashabiki wapenzi wa soka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wameeleza mengi kwa nyakati tofauti wakionesha mitazamo yao yenye kuashiria dhamira na kiu iliyopo ya kuhitaji mafanikio zaidi katika soka la nchi hii.

Huu ni ujumbe unaoamsha ari na moyo wa kumtaka kila mtu katika nafasi yake kutimiza wajibu wake, lakini kwa kuongozwa na mipango pamoja na mikakati madhubuti yenye nidhamu ya hali ya juu na weledi mkubwa.

Kwa bahati mbaya kila kukicha neno ‘soka’ au mpira wa miguu ni sentensi, maneno yasiyoepukika kutamkwa miongoni mwa wapenzi na wadau wa mchezo huu kote duniani.

Matamshi haya yanaambatana na mijadala inayohusu matukio na shughuli mbalimbali zinazouzunguka mpira wa miguu, mfano mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji watimu zetu za Simba na Yanga, ratiba ya ligi zetu, Kombe la FA, mashindano ya kimataifa, Kombe la Mapinduzi na mengineyo.

Kimsingi shughuli ni nyingi na kila kitu kunahitaji kuendeshwa vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Uchambuzi wa mwaka mzima utagusa kila nyanja kulingana na shughuli na matukio yote katika timu zetu.

Mara nyingi tathimini ya mwisho inatuonyesha mafanikio kidogo na sehemu kubwa ni kushindwa kufanya vizuri.

Kwa msingi huo safari yetu tuliyoianza sasa inabidi tujidhatiti sana ili tusiendelee kuwa taifa linalodidimia katika soka kuanzia ndani mpaka nje (kimataifa).

Kwa mfumo wetu tayari kalenda ya matukio na shughuli za ndani zimeanza kwa Ligi za Wilaya, Mikoa, Daraja la Pili (SDL) na hata la kwanza (FDL) pamoja na Ligi Kuu, sambamba na Kombe FA. Je, nini kinaonekana huko? Pia, Ligi ya Wanawake inaendelea, kwa jumla viwanja vyetu nchi nzima vina hekaheka nyingi.

Wakati tukiwa tunashuhudia ofisi za shirikisho na watendaji wakuu wanatoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya usimamizi na utekelezaji kwa wasaidizi wao ilikufanikisha sera zao, mwaka umeanza na matukio yenye kuleta matumaini endapo tutaweka mbele maslahi ya soka na taifa kwa jumla.

Wahenga walisema bahati haiji mara mbili. Nchi yetu imepata bahati ya kuwa mwenyeji wa  Mkutano wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Feb 22. Hii ni fursa muhimu na pekee kwa malendeleo ya soka letu.

Kwa kawaida sio rahisi kupata ugeni mkubwa wa aina hii unaojumuisha viongozi na Watendaji Wakuu wa Fifa pamoja na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa wakati mmoja, lakini pia kupokea wajumbe au viongozi wakuu wa nchi 19 wanachama wa Fifa watakaohudhuria mkutano huu.

Kwa vyovyote vile zipo sababu za msingi na vigezo vya kikanuni vilivyosababisha nchi yetu iteuliwe kuwa mwenyeji wa kikao hiki muhimu, sababu mojawapo ni nchi yetu kuwa mwanachama wa siku nyingi wa Fifa na Caf.

Kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa makongamano makubwa kama hili la Fifa, tayari agenda ama hoja zitakazojadiliwa zimewekwa hadharani kwa makusudi ili washiriki waweze kujiandaa kuchangia mawazo, ushauri na kutoa mapendekezo.

Baada ya taarifa hizi za mkutano kujulikana, kumekuwa na mitazamo na maoni chanya kutoka kwa wadau. Inawezekana sisi kama nchi hatutarajii kufaidika moja kwa moja na kwa haraka kutokana na maazimio au maamuzi ya mkutano huu, lakini nafikiri ni vizuri tukaamini kuwa tutafaidika hata kama siyo kwa sasa hivi, lakini hapo baadaye tuataona matunda yake.

Ni wazi kuwa soka letu lina matatizo mengi ya msingi kwa sababu za maana, na matatizo mengine hayana msingi hasa yake yanayosababishwa na uzembe na ubinafsi.

Ukiangalia agenda zilizotajwa za mkutano huu unabaini kuwa ni nyeti na zinayagusa moja kwa moja maisha na maendeleo ya mpira katika mataifa yote duniani hususani barani Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari ajenda zitakuwa ni; (i) fedha za mgao kutoka Fifa kwa ajili ya maendeleo ya soka (ii) mashindano mbalimbali ya vijana na wanawake kwa ngazi ya vilabu (iii) usajili wa wachezaji kwa njia ya mtandao (TMS) na  (iv) matukio muhimu katika kalenda ya Fifa.

Kimsingi na kimantiki hoja hizi zimefanyiwa utafiti wa kutosha na Fifa kabla ya kuzichagua ili zije zijadiliwe na wajumbe wa nchi 19 zitakaoshiriki katika kongamano hili, kwa namna yoyote ile ni hoja zinazotatiza, kuchelewesha, kuathiri na kodhoofisha hatua mbalimbali za kusukuma maendeleo ya soka duniani katika viwango tofauti.

Sote tunafahamu kuwa mpira unahitaji pesa za kutosha kama tunataka kupata maendeleo makubwa katika soka la ushindani. Ukiangalia katika mataifa mengi duniani timu nyingi hazina mifumo mizuri ya vyanzo vya mapato vya uhakika, hali ambayo inawalazimu wasimamizi wa soka kuendesha kwa taabu na kwa kutumia nguvu nyingi.

Hii ni moja ya sababu hapa nyumbani timu kongwe za Simba na Yanga zinafikiria kuachana na mfumo wa kizamani wa kuwa tegemezi.

Itaendelea Ijumaa Ijayo