Rais wa TFF, Karia aongoza makumi kumzika Mwanahabari Asha Muhaji

Muktasari:

Mbali na viongozi hao wa TFF, pia kulikuwa na uwakilishi wa klabu mbalimbali za soka ikiwemo Simba ambayo marehemu aliitumikia.

Dar es Salaam.Wadau mbalimbali wa mpira wa miguu, ndugu, jamaa na marafiki wamejitokeza kushiriki mazishi ya aliyewahi mhariri wa michezo wa gazeti Rai na Afisa Habari wa Simba, Asha Muhaji.

Mwanahabari huyo alifariki dunia jijini Dar es Salaam juzi katika Hospitali ya Hindu Mandal alipokuwa akitibiwa maradhi ya TB ngozi.

Mazishi hayo yalifanyika katika Makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni jijini Dar es Salaam leo Alhamis Machi 26, na miongoni mwa waliohudhuria ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na katibu wake Wilfred Kidao pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.

Mbali na viongozi hao wa TFF, pia kulikuwa na uwakilishi wa klabu mbalimbali za soka ikiwemo Simba ambayo marehemu aliitumikia.

Miongoni mwao ni wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again', Wakili Hussein Kitta na Seleman Haroub.

Wadau wengine waliojitokeza ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetileh Osiah, Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Emmanuel Mpangala, aliyekuwa meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, maofisa habari wa Yanga, Azam, Simba na Ruvu Shooting, Zaka Zakazi, Hassan Bumbuli, Haji Manara na Massau Bwire.

Akimzungumzia marehemu, mwandishi wa habari mkongwe, Eric Nampesya alisema kuwa marehemu alikuwa kioo cha uandishi wa habari za michezo nchini.

"Nimefahamiana na marehemu kwa muda mrefu na kwa mara ya kwanza nilikutana naye Mwanza takribani miaka 20 iliyopita. Kiufupi alikuwa ni mtu ambaye alikuwa mwanamichezo hasa," alisema Nampesya