Mo Salah awakalisha Torres, Suarez huko Anfield

SUPASTAA, Mohamed Salah amekuwa mchezaji aliyefunga mabao 50 ya Ligi Kuu England kwa haraka zaidi katika historia ya kikosi cha Liverpool.

Fowadi huyo wa kimataifa wa Misri, Mo Salah imemchukua mechi 69 tu za Ligi Kuu England kufikisha idadi hiyo ya mabao baada ya kuwapiga bao matata kabisa Southampton juzi Ijumaa. Bao hilo limemfanya Mo Salah kumpiku Fernando Torres, aliyekuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao 50 chapchap kwenye ligi baada ya kucheza mechi 72. Lakini, Salah sasa amefikisha idadi hiyo akiwa nyuma kwa mechi tatu.

Luis Saurez yeye alifikisha idadi hiyo ya mabao baada ya kucheza mechi 86, wakati Robbie Fowler alihitaji mechi 88 kufikisha hiyo nusu karne ya mabao kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England kwenye kikosi cha wababe hao wa Anfield.

Mo Salah alisema: “Nadhani hili ni bao langu la 50 kwenye ligi nikiwa na Liverpool, likiwa la kwanza baada ya mechi tisa. Lakini, Henderson naye amefunga bao lake la kwanza katika mechi 30, hivyo sote tutakuwa watu wenye furaha.”

Kabla ya bao hilo la Ijumaa, mara ya mwisho Mo Salah kufunga ilikuwa Februari 9 na hapo katikati zimepita mechi sita za Ligi Kuu England na mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya.