Hazard, Zidane washamalizana

LINALOSEMWA ni kwamba Zinedine Zidane amempigia simu staa wa Chelsea Eden Hazard na sasa kila kitu kinadaiwa kuwa sawa kwa staa huyo wa Kibelgiji kwenda kujiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu huu.

Kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana Hazard alikuwa na uhakika wa kwenda kujiunga na Real Madrid, lakinni baada ya Zidane kuondoka kwenye timu hiyo kila kitu kilitibuka na kushindikana hivyo supastaa huyo wa zamani wa Lille aliendelea kubaki Stamford Bridge.

Sasa Zidane amerudi Real Madrid na kinachoripotiwa amempigia simu Hazard na kumweleza mipango yake kitu ambacho kimedaiwa kimeweka sawa mipango yote na mchezaji huyo atakwenda kutua Bernabeu.

Kinachoelezwa kwa sasa, Hazard mwenyewe ameshakubali kusaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Pauni 14 milioni kwa mwaka huko Los Blancos atakoenda kukipiga msimu ujao.

Real Madrid msimu huu mambo yao si mazuri kabisa na hawana uhakika wa kubeba taji lolote baada ya kuachwa pointi 12 na Barcelona kwenye msimamo wa La Liga huku wakiwa wameshatupwa nje kwenye michuano ya Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mkataba wa Hazard huko Chelsea utafika tamati 2020 na bado hataki kusaini dili jipya kwenye kikosi hicho cha London jambo linaloweka bayana amepania kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.

Hazard amefunga mabao 105 katika mechi 339 alizochezea Chelsea tangu alipojiunga mwaka 2012 akitokea Lille ya Ufaransa.